Diaspora wapewa mafunzo ya Kiswahili Msumbiji ili wawafundishe wageni

Baraza la Kiswahili la Taifa BAKITA, limeendelea kuteleleza Mpango wa Taifa wa Ubidhaishaji wa Kiswahili nje ya Nchi ambapo kupitia Wataalamu wake Edward Nnko na Arnold Msofe ( Wachunguzi Lugha) limetoa mafunzo maalumu ya kuimarisha stadi ya kufundisha Kiswahili na Utamduni kwa Diaspora na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania Nchini Msumbiji.

Kupitia mafunzo hayo, Washiriki wamepata uwezo wa kufundisha Kiswahili kwa Wageni, wakitumia uelewa wao wa lugha ya Kireno ili kufikia Jamii pana ya Watu wa Msumbiji, na Nchi nyingine zinazotumia lugha hiyo Duniani.

Baada ya mafunzo hayo, Balozi wa wa Tanzania nchini Msumbiji, Balozi Phaustine Martin Kasike amewatunuku Washiriki 43 vyeti vya utambuzi, vinavyowatambulisha rasmi kuwa Wakufunzi wa Kiswahili kwa wageni na nje ya Nchi ambapo amewasihi Washiriku kutumia fursa hiyo muhimu kuonesha uzalendo wao kwa kufundisha na kueneza lugha ya Kiswahili nchini humo na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kubidhaisha Kiswahili.

Katika hatua nyingine BAKITA imekitambua Kituo cha Kiswahili na Utamaduni cha Ubalozi wa Tanzania, Maputo – Msumbiji kwa kukabidhiwa cheti na BAKITA na (Arnold Msofe -Mchunguzi Lugha ) kwa Balozi Phaustine Martin Kasike

Balozi ameipongeza BAKITA kwa kutambua kituo Kiswahili na Utamaduni cha Ubalozi wa Tanzania, Maputo ambapo ameeleza kuwa utambuzi wa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Taifa wa kubidhaisha Kiswahili, ambapo kitachangia kueneza na kufundisha Kiswahili na utamaduni wa Kitanzania kwa jamii ya Msumbiji na ulimwengu mzima, kituo hiki kitakuwa daraja la kiutamaduni na kielimu, kikilenga kukuza lugha ya Kiswahili na kutoa fursa kwa wananchi wa Msumbiji na mataifa mengine kujifunza na kushiriki katika urithi wa Kiswahili, hivyo kusaidia lugha hii kuwa na nafasi zaidi katika jukwaa la Kimataifa.

Related Posts