HESLB yatangaza awamu ya Nne ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Shahada na Stashahada

*Wanafunzi 9068 wapangiwa mikopo ya Sh bilioni 27.5 awamu ya Nne

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza Awamu ya Nne ya ugawaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2024/2025. Jumla ya wanafunzi 9,068 wa shahada ya awali na stashahada wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 27.52.

Kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliodahiliwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini kwa shahada za awali, jumla ya wanafunzi 4,400 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 13.74.

Aidha, wanafunzi 2,646 wanaoendelea na masomo yao ya shahada ya awali lakini wanapokea mikopo kwa mara ya kwanza (first-time continuing) wamepangiwa mikopo ya Sh bilioni 8.37.

Awamu hii pia imehusisha wanafunzi wapya 2,022 wa stashahada wa mwaka wa kwanza, ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS bilioni 5.41. Wanafunzi hawa wamejiunga na programu za kipaumbele katika vyuo vya kati nchini Tanzania.

Ruzuku ya Samia Scholarship kwa Wanafunzi wa Sayansi na Teknolojia

Kiasi cha Sh bilioni 3.14 kimetolewa kwa ajili ya ruzuku kwa wanafunzi 625 wa mwaka wa kwanza wanaonufaika na ‘Samia Scholarship’ kwa mwaka huu wa masomo. Hadi sasa, wanafunzi 588 wamepangiwa ruzuku katika awamu ya kwanza, 11 katika awamu ya pili, na 26 katika awamu ya tatu. Mpango huu wa ruzuku unalenga kusaidia wanafunzi wa shahada ya awali katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati, na Tiba.

Dirisha la Rufaa kwa Wanafunzi Wasioridhika na Viwango vya Mikopo

HESLB imefungua dirisha la rufaa kwa wanafunzi ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa au ambao hawajapangiwa mikopo kabisa. Wanafunzi hao wanashauriwa kukata rufaa kuanzia Jumatatu, Novemba 4 hadi Jumapili, Novemba 10, 2024.

Hatua hii ina lengo la kuwapa wanafunzi fursa ya kuomba marekebisho katika upangaji wa mikopo kwa kuzingatia mahitaji yao binafsi na hivyo kuhakikisha kwamba wote wanapata fursa ya kuendelea na masomo yao kwa ufanisi.

Related Posts