Serikali kuwaanda wataalamu wa ndani utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati

Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Edward Mpogolo amesema Serikali imeendelea kuwajengea uwezo wataalamu wake wa ndani kwa kuwashirikisha kwenye miradi mikubwa kupitia Wizara ya Ujenzi.

Mpogolo amesema hayo leo Oktoba 29, 2024 alipomwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa tano wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).

Amesema Serikali inaendelea kutoa hamasa kwa wataalamu wa ndani kuchangamkia fursa za kazi katika miradi mikubwa inayoendelea hivi sasa hapa nchini.

Mpogolo amesema kuwa miradi ya Serikali inatekelezwa kwa gharama kubwa, hivyo Serikali imefanya jitihada za kuboresha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na kwamba sheria hiyo imeweka upendeleo mahususi na kuongeza ushiriki wa wazabuni wa ndani kutekeleza miradi mikubwa.

Aidha, Mpogolo amewataka wataalamu na kampuni za ndani kushiriki katika michakato yote ya zabuni za miradi mikubwa ili hatimaye kujijengea uwezo wa kitaaluma na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje kwa kazi za ujenzi pamoja na matengenezo.

Related Posts