SERIKALI kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF)kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na hasa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF) wamezindua Mpango wa Stawisha Maisha kwa lengo la kuimarisha hali za lishe kama sehemu ya kukabiliana na changamoto ya utapiamlo kwa kaya masikini ambazo ziko kwenye mpango wa TASAF.
Uzinduzi wa Mpango huo umefanyika Oktoba 29,2024 katika Wilaya ya Mkuranga mkoani hiyo na kuhudhuriwa na viongozi, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi ambao ndio walengwa wakuu ambapo kupitia mpango huo wa Stawisha jamii wananchi watahamasisha kuhusu lishe bora sambamba na kupatiwa mafunzo na kubadilisha uzoefu kupitia katika vikundi ambavvyo wameavianzisha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliofanyika Kijiji cha Mkiu wilayani Mkuranga mkoani Pwani uliokwenda sambamba na kukabidhi redio zinazotumia nguvu za juu kwa vikundi vya walengwa Stawisha Maisha, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray amesema kwamba moja ya sababu ya kuanzishwa kwa mpango huo ni kukabiliana na changamoto ya udumavu ambayo kimsingi inayosababishwa kwa utapiamlo kwa sehemu kubwa.
“Athari za janga hili ni kubwa ikiwemo kuongezeka vifo vya Watoto , matatizo ya akili, matatizo ya kiafya ya kudumu ambayo yanaweza kuwafuatia Watoto hawa hadi umri wa utu uzima zikifunguka kaya nzima zinazozunguka kwa umasikini. Changamoto hizi husababisha madhara zaidi ikiwemo kuendeleza mzunguko wa umasikini ambao sio tu unawaathiri watu binafsi bali na kaya nzima kwa ujumla.
“Ili kukabiliana na changamoto ya udumavu, Serikali kupitia TASAF kwa kushirikiana na Washirika wa maendeleo hususani UNICEF umeanzishwa Mradi wa Stawisha Maisha ambao utasaidia jamii kubadili tabia.Mradi huu ni sehemu ya mtandao wetu mpana wa kunusuru kaya masikini ambao tunautekeleza lakini lengo ni kupunguza utapiamlo kwa watoto hasa kwa kaya ambazo zipo katika hatari zaidi zilizopo kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini.”
Mziray amesema kupitia mpango huo wanalenga kukuza maendeleo ya rasilimali watu na kuziwezesha kaya kujiweka huru kutoka katika mnyororo mzima wa umasikini kwa kuzingatia elimu na msaada kuhusu lishe kwa akina mama , Watoto wachanga , Watoto wadogo , sit u tunatatua matatizo ya kiafya yaliyopo sasa pia tunawekeza katika siku zijazo za taifa letu.
Amesema mpango wa Stawisha Maisha umeundwa kwa vipengele kadhaa muhimu ambavyo wanaamini vitaleta mabadiliko katika jamii na kufafanua wanavyo vipindi vya redio vyenye kuelimisha na kuburudisha kila wiki katika kipindi cha miezi sita na vipindi hivyo vitatoa elimu muhimu kuhamasisha jamii kushiriki katika mijadala muhimu kuhusu kuimarisha lishe.
“Usambazaji wa redio zinazotumia nguvu ya jua kusambaza katika kaya hizo tunalenga pia kuongeza majadiliano katika vikundi vitakavyokuwa vinasimamiwa na walengwa wenyewe ambapo watajifunza na kuhamaishana kutatua matatizo kwa pamoja.Mkazo wetu ni kwenye kaya zenye watoto chini ya miaka mitano , akina mama wajazito na wasichana wenye umri balee.
Kwa upande wake Mwakilishi wa UNICEF nchini Lawrence Oundo amesema utampamlo ni tatizo kubwa na linasababishwa kwa kiasi kubwa na watu walio katika umasikini. “Tunahitajika kutumia njia mbalimbali katika mapambano dhidi ya utapiamlo. Lengo ni kuondoa tatizo hilo kwa jamii na kupata lishe bora” amesema na kuongeza “Leo tunazindua mpango muhimu wa Stawisha Maisha. Huu ni mpango ambao UNICEF kwa kushirikiana na TASAF wamekuja nao kuutazama umaskini na kuhakikisha wanaoundoa katika jamii.”
Amesema Serikali ya Tanzania inayo mipango mingi ikiwemo Dira ya Taifa 2025-2050 inayokuja ambayo inautazama umaskini katika nyanja mbalimbali na kwamba Stawisha Maisha ni mpango muhimu kati ya TASAF na UNICEF kuhakikisha wanapunguza umaskini kwa watanzania na kukuza uchumi wa wananchi kupitia mbinu mbalimbali za stadi za maisha.
Awali Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Omari Mwanga ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo amesema mpango wa Stawisha Maisha katika wilaya hiyo unalenga kuboresha maisha ya wanananchi na kwamba mpango wa Stawisha Maisha katika wilaya hiyo ulianza Agosti 2014 kwa kuunda vikundi vya Stawisha maisha katika Kata 13 na vijiji 19,jumla ya vikundi 30 vimeundwa na vikundi hivyo vitakuwa vikikutana mara moja kwa wiki kwa lengo la kumsikiliza vipindi vya redio vyenye maudhui yanayolenga kuelimisha na kuhamasisha umuhimu wa kujali Lishe Bora kwa watoto , wajawazito na wasichana balee.
“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kupitia wadau wa maendeleo kutupatia Mpango wa Stawisha maisha kwa ajili ya kuimarisha lishe kwa wananchi wa Mkuranga.Tunakila sababu ya kutoa shukrani kwasababu katika mwaka wa fedha 2024/2025 tumeanza mchakato wa kuibua miradi ya kutoa ajira za muda.
“Jumla ya miradi 122 imeibuliwa katika vijiji 125 .Katika miradi iliyoibuliwa 83 ni ya upandaji miti, miradi 27 ya barabara za mitaa ,miradi 10 ya vivuko vya waenda kwa miguu ,mradi mmoja wa Bwawa kwa ajili ya umwagiliaji na mradi mmoja wa kisima kifupi.Miradi yote itagharimu Sh.170,731,100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa gharama za ujira kwa walengwa ni 640,080,000.”
Hata hivyo amesema kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Septemba 2024 jumla ya watoto 167,680 walifanyiwa uchunguzi wa hali ya lishe Kati ya hao waliokuwa na hali nzuri ya lishe ni asilimia 55.3 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.3 kutoka lile la mwaka 2022 .Waliokuwa na uzito pungufu ni asilimia 10.0 toka 13.3 ,ukondefu asilimia 4.6 toka asilimia 4.9 wakati upungufu wa damu asilimia 20.3 toka asilimia 23.