UFUNGUZI WA BWENI LA WASICHANA-SITALIKE:HATUA MPYA KUELEKEA KUIMARISHA ELIMU NA USALAMA KWA MTOTO WA KIKE

Na. Jacob Kasiri – Sitalike

Furaha ni kupokezana inaweza kuwa kwa watu wa jamii mbili tofauti kwa wakati mmoja, tukio hili limejiri leo tarehe 29 Oktoba, 2024 wakati maafisa na askari wa Hifadhi ya Taifa Katavi pamoja na wadau wa uhifadhi na utalii wakisherehekea kilele cha miaka 50 zilienda sanjari na vifijo na ndelemo za wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Sitalike baada ya kukabidhiwa bweni lao lililozinduliwa leo katika hafla ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Sitalike – Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.

Wakiwa na furaha na bashasha ya kuanza kutumia bweni hilo, wanafunzi hao walisema, Bweni hilo litapunguza utoro na visababishi vya mimba vinavyotokana na vishawishi vya barabarani wakati wa kwenda na kutoka shule.

Akikata utepe kuashiria uzinduzi wa bweni hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi aliwahasa wanafunzi kutumia nafasi hiyo kushirikiana kusoma kwa bidii tofauti na awali kila mwanafunzi alikuwa nyumbani kwao.

“Lengo la mabweni ni kuwaunganisha pamoja ili msome kwa kushirikiana, na mnapomuona mwenzenu analegalega msisite kumuhamasisha ili aendane na kasi yenu, TANAPA na TEA inawajali ili mtimize malengo yenu na baadae muwasaidie wazazi wenu”, alisema Mhe. Buswelu.

Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA na Mkuu wa Kanda ya Kusini Steria Ndaga kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA aliwataka wanafunzi hao kulitunza bweni hilo ili litumike kwa muda mrefu, huku pia akiwaonya kutotumia vifaa vinavyoweza kusababisha moto. Moto husababisha hasara kubwa kwa wanafunzi, kwa shule na taifa kwa ujumla.

Akisoma ripoti ya mradi huo wa bweni Mkuu wa Shule ya Sekondari Sitalike Samson Kaitira Mafwolo alisema, “Mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 190 ambapo TANAPA ilichangia zaidi ya milioni 77, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilichangia zaidi ya milioni 97 na DED Wilaya ya Nsimbo akichangia milioni 15.”

Kulingana na adha waliokuwa wakipata wanafunzi hao, Aneth J. Marko kutoka Kidato cha nne alisema, “Bweni hilo licha ya kutuepusha na vishawishi vya barabarani, pia litatukinga dhidi ya wanyamapori wakali kwani sehemu kubwa ya makazi yetu yamezungukwa na hifadhi hii.”

Sherehe hizo za Miaka 50 ya Hifadhi ya Taifa Katavi licha ya uzinduzi wa bweni hilo pia ziliambatana na uzinduzi wa ujenzi wa nyumba 12 za watumishi wa hifadhi chini ya ufadhili wa benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), burudani mbalimbali, na ukataji wa keki kuashiria mwanzo mpya wa hifadhi hiyo huku ikihitimishwa na ziara ya viongozi na wageni waalikwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha na kujione shughuli za uhifadhi, utalii na maeneo ya iwekezaji.

Related Posts