Zeit Online
Zeit Online limeangazia tahadhari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kuhusu madhara ya ongezeko la machafuko nchini Sudan. Limemnukuu Guterres akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema kuwa, wahusika wa vita vya Sudan wanachochea vurugu na mataifa ya kigeni yanauzidisha mzozo. Raia nchini humo wanaishi katikati ya mauaji ya kutisha na ukatili usioelezeka ukiwemo ubakaji, magonjwa ya kuambukiza yanayosambaa kwa kasi na mapigano ya kikabila.
Zaidi gazeti hilo la mtandaoni limemnukuu Guterres akisema kuwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao Kaskazini mwa Darfur, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na baa la njaa.
Katika siku za hivi karibuni, kulikuwa na ripoti za kutisha kuhusu mauaji ya kimbari na ukatili wa kingono katika vijiji kwenye mkoa wa Al Jazeera. Takwimu za Umoja wa Mataifa na shirika moja la kitabibu zinaonesha kuwa zaidi ya watu 120 waliuwawa katika shambulio lililofanywa na wapiganaji wa kundi la RSF katika mkoa huo.
Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa linasema watoto kadhaa ni miongoni mwa waliouwawa na watoto wasiopungua 43 walijeruhuwa. Vita nchini Sudan viliibuka Aprili 2023 kutokana na mivutano kati ya jeshi rasmi la taifa hilo na wapiganaji wa kundi la RSF. Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia mizozo la Armed Conflict Location and Event Data zaidi ya watu 24,000 wameshauwawa tangu vilipoibuka vita hivyo. Wengine zaidi ya milioni 11 wamelazimika kuyakimbia mapigano na milioni tatu kati yao wamekimbilia mataifa jirani.
die tageszeitung
die tageszeitung limeandika kuhusu hatua ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya kutaka kuzuia ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, MONUSCO usiondoke Kongo kinyume na ilivyokuwa imepangwa hapo awali.
Aidha gazeti hili limemnukuu waziri wa mambo ya kigeni Therese Kayikwamba Wagner, aliyezungumza akiwa mjini London siku ya Jumanne akisema kuwa kuondoka kwa vikosi hivyo Kongo kutakuwa suala gumu kutokana na hali ya kiusalama ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa makubaliano ya sasa, uwepo wa wanajeshi hao wa kulinda amani nchini humo utafikia kikomo Desemba 20 mwaka huu. Tangu mwezi Mei, wanajeshi hao wamekuwepo katika mikoa ya mashariki ya Kivu Kaskazini na Ituri inayokabiliwa na machafuko.
Wagner amesema kuna haja ya wanajeshi hao kuendelea kuwepo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na madai ya uwepo wa wapiganaji 4,000 kutoka Rwanda wakiwa upande wa waasi wa M23 huko Kaskazini mwa Kivu. Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wanawasaidia wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, wanaoshirikiana na serikali kukomesha uasi.
Juhudi za kidiplomasia zinazofanywa na Angola ili kuutatua mzozo kati ya serikali ya taifa hilo na waasi wa M23 hadi sasa hazijazaa matunda na waasi wamekuwa wakiendelea kusonga mbele tena Kivu Kaskazini.
Neue Zürcher,
Juma hili Neue Zürcher limekimulika kilio cha mashirika ya kiraia nchini Tunisia yanayolalamika kubanwa na serikali ya Rais Kais Saed.
Linaeleza kuwa, kwa mara nyingine Kais Saied alishinda kwa kishindo katika uchaguzi wa hivi karibuni. Hata hivyo, matumaini ya watu wengi ya kutengamaa kwa hali ya kisiasa yamefifia. Mashirika hasa yasiyo ya kiserikali yanahisi kuwa yananyanyaswa na mamlaka.
Mkuu wa kituo cha demokrasia cha Al Kawakibi nchini humo Amine Ghali amenukuliwa na gazeti hili akieleza kuwa kwa bahati mbaya mashirika hayo yana haki ya kuwa na hofu. Anasema hukumu nyingi za vifungo jela kutokana na kuwasaidia wahamiaji, uchunguzi dhidi ya mashirika ya kutetea haki za inadamu na demokrasia, na mijadala dhidi ya mashirika hayo viko katika kiwango cha juu zaidi serikalini.
Ghali amesema hayo yanajiri licha ya kwamba kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya asasi za kiraia na sekta ya umma nchini humo kwa kipindi cha muongo mmoja .
Neuer Zürcher linakwenda mbali zaidi na kusema kuwa hivi sasa mashirika mengi ya kiraia yako katika shinikizo kubwa na mara nyingi hayako tayari kulizungumzia wazi suala hilo.
Siwar Gmati wa shirika la I Watch ameeleza namna mamlaka zilivyoliandama shirika hilo. Wamewahi kuitwa wakitakiwa kujieleza kwa mamlaka mara 16 katika mwaka mmoja uliopita. I Watch ambalo kimsingi linapambana na rushwa linafahamika kuwa moja kati ya mashirika tata yenye sauti kali.
Mwanzoni mwa mwezi Septemba, Tume ya Uchaguzi nchini humo, ISIE ilitangaza kuwa shirika hilo na jingine linalofuatilia uchaguzi kuwa hayakupewa vibali vya kufuatilia uchaguzi huo kwa kuwa yalipokea fedha zenye utata kutoka nje ya nchi ili kuvuruga masuala ya taifa hilo. Uamuzi huo, kulingana Amine Ghali wa kituo cha demokrasia cha Kawabiki ulikuwa na athari katika uwazi kwenye uchaguzi. Kwa kawaida kulikuwa na waangalizi wa uchaguzi 20,000, lakini kipindi hiki walikuwepo waangalizi 1,700 pekee katika vituo karibu 5,000 vya kupigia kura.
Gazeti hilo limeandika mengi kuhusu hali hiyo lakini linamalizia kwa kuandika kwamba, kumekuwa na majaribio yanayojirudia rudia ya kupitisha sheria dhidi ya mashirika. Rasimu iliyovuja na rasimu rasmi zina jambo moja linalofanana. Zote, zinalenga kuyawekea vizuizi mashirika ya kiraia ambayo Tunisia ilikuwa na matumaini nayo baada ya mapinduzi ya mwaka 2011.