Bakita yatembelea Chuo Kikuu Pedagogica De Maputo kuimarisha Kiswahili

IMaofisa wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Edward Nnko na Arnold Msofe, walifanya ziara rasmi nchini Msumbiji, wakiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kukuza lugha ya Kiswahili. Ziara hiyo iliwahusisha kutembelea Shule ya Kimataifa ya Maputo, ambapo kwa kushirikiana na Ofisa wa Ubalozi ndugu Chacha walikutana na Mkurugenzi wa shule hiyo, Prof.Lucas Mkuti.

Lengo kuu lilikuwa kukagua mazingira ya kuanzisha kituo cha kufundisha Kiswahili na utamaduni katika shule hiyo, pamoja na kufanya maandalizi ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya ushirikiano baina ya BAKITA na Shule ya Kimataifa ya Maputo.

 

Wakiwa shuleni hapo, maofisa hao walikutana na walimu na wanafunzi wanaojifunza Kiswahili, na kushuhudia juhudi kubwa zinazofanywa katika kujenga umahiri wa lugha hiyo. Pia walikagua miundombinu ya shule hiyo kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kufundishia Kiswahili na utamaduni, ambacho kinatarajiwa kuwa kiungo muhimu cha kukuza lugha ya Kiswahili na utamaduni wake nchini Msumbiji na nchi za jirani kama Eswatini na Madagascar.

Aidha, BAKITA pia ilitembelea Chuo Kikuu cha “Pedagogica de Maputo,” ambapo walifanya mazungumzo na Prof. Paulino Paulo Fumo, Mkuu wa Kitivo cha Lugha, Sayansi, Mawasiliano na Sanaa. Katika mazungumzo yao, walikubaliana kuwa waanze kuwatumia waalimu wa Tanzania waliopata mafunzo ya ya kuimarisha stadi za kufundisha wageni, wakati mipango ya kuwapata walimu wa kudumu ikiendelea kwa kwa kushirikiana na BAKITA na Ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Makubaliano hayo na ziara hiyo kwa ujumla ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kubidhaisha Kiswahili, na kwamba yanatarajiwa kuimarisha juhudi za kukuza na kueneza Kiswahili kama lugha ya kimataifa, huku serikali ya Tanzania kupitia BAKITA ikichangia katika kufanikisha azma ya Msumbiji kuimarisha ufundishaji wa Kiswahili katika ngazi mbalimbali.

Related Posts