Benki ya NMB yajizatiti kuwezesha makampuni ya Korea Kusini yanayotekeleza miradi nchini – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

 

Na Mwandishi Wetu

Benki ya NMB Plc imesisitiza kuendelea kutekeleza dhamira yake ya kuyawezesha makampuni kutoka Korea Kusini yenye nia ya kuwekeza hapa nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuchangia ukuaji wa uchumi endelevu.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Miamala Benki ya NMB Linda Teggisa wakati ya semina ya ‘2024 Korea – Tanzania Project Plaza’ iliyofadhiliwa na Benki ya NMB jijini Dar es Salaam jana na kukutanisha zaidi ya kamuni 100 jijini Dar es Salaam na mtandaoni.

“Dhamira yetu iliimarishwa zaidi baada ya kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Shirika la Korea Kusini linalojihusisha na kufadhili miradi katika sekta ya ujenzi la Korea Finance for Construction (K-FINCO) miezi michache iliyopita. Kupitia ushirikiano huu, tunalenga kupanua masuluhisho yetu ya kifedha zaidi kwa kupitia ufadhili wa vifaa ili kusaidia utekelezaji wa miradi,” alisema.

Tegessia aliongeza, “Tunatarajia kupanua wigo wetu kwa kutoa huduma zingine ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili wa mitaji, ufadhili wa mali na masuluhisho ya miamala ili kuongeza mnyororo mzima wa thamani wa miradi,”

 

 

Alibainisha kuwa Benki ya NMB itaendelea kuwa mdau madhubuti katika ufadhili wa miradi ya kimlalati kupitia ubia na taasisi kubwa za fedha duniani huku akiipongeza kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara.

“Mfumo imara kwa kiasi kikubwa umechangia ukuaji wa sekta ya benki na fedha katika miaka ya hivi karibuni. Sekta ya benki imeshuhudia ukuaji mkubwa katika utoaji wa mikopo kutoka shilingi trilioni 34.6 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 46 kwa mujibu wa ripoti,” alisema.

Alibainisha kuwa benki yake itaendelea kuchukua jukumu kuu katika kukuza ushirikishwaji wa kifedha kama sehemu ya juhudi za kuziba pengo kwa wasio na akaunti za benki.

Tegessia wakati wa hafla hiyo alipongeza uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Korea Kusini na kuongeza kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea kukuza maendeleo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri wakati wa hafla hiyo rai kwa makampuni zaidi ya Korea Kusini kuja kuwekeza hapa nchini.

“Kuna sababu lukuki za kwanini makampuni ya Korea Kusini kuja kuwekeza Tanzania. Mbali na uhusiano wa muda mrefu wa nchi hizi mbili ambao nchi zote mbili zinaendelea kufurahia, Tanzania kwa miongo miwili iliyopita imeweka sera nzuri na thabiti za kiuchumi ambazo zimesababisha ukuaji wa wastani wa takriban asilimia 7 kwa mwaka,” alisema.

 

 

Teri alibainisha kuwa Tanzania ina fursa mbalimbali za uwekezaji huku akisisitiza kuwa kwa kuwa Tanzania n mwanachama wa jumuiya mbalimbali, basi wawekezaji pia watanufaika moja kwa moja na jumuiya.

“Kutokana na hilo, makampuni ya Korea Kusini yanayofanya shughuli hapa nchini yatakuwa katika nafasi nzuri ya kupata masoko katika jumuiya hizo,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Korea Kusini nchini hapa Eunju Ahn wakati wa tukio hilo alipongeza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili akisisitiza dhamira ya nchi yake kuendeleza ukuaji wa pamoja.
“Nchi yangu imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali. Nina imani kuwa uhusiano wetu utaimarika zaidi katika miaka ijayo,” alisema.

Semina hiyo ilikutanisha makampuni mbalimbali ya Korea Kusini yanayojishughulisha na miradi ya mafuta na gesi, maji, madini, utengenezaji wa meli, viwanda, na miundombinu.

MWISHO

Related Posts