Jopo la majaji watatu likiongozwa na Eric Ogola aliyeshirikiana na Anthony Mrima na Freda Mugambi, lilifutilia mbali amri hiyo iliyomzuwia naibu wa rais mteule Kithure Kindiki kuapishwa rasmi na kuanza majukumu yake mapya.
Jopo hilo liliamuru kuwa ofisi ya naibu wa rais ikiendelea kuwa wazi itasababisha mkwamo wa kikatiba jambo linalokiuka matakwa ya umma.
Agizo hilo lililotilia guu uapishwaji wa Kithure Kindiki kuwa naibu mpya wa rais lilitolewa na Mahakama Kuu ya Kerugoya wiki mbili zilizopita pindi baada ya Rais William Ruto kumteua waziri huyo wa usalama wa taifa kuchukua nafasi ya Rigathi Gachagua.
Endapo amri hiyo ingeongezewa muda, basi ofisi ya naibu wa rais ingesalia wazi kwani haikujumlisha Gachagua kurejeshwa kazini na kuendelea na majukumu yake ya naibu wa rais, limefafanua jopo hilo la majaji watatu.
Njia ni wazi kwa Kindiki kuapishwa
Jopo hilo lililoongozwa na Jaji Eric Ogola lilisisitiza kuwa tofauti na wajibu wa naibu wa rais katika mazingira ya katiba mpya ya 2010, makamu wa rais kama ilivyoelezea katiba ya 1963, hana uwezo wa kutimiza majukumu ya rais, spika wa bunge la taifa au mwengine yeyote hivyo basi ofisi hiyo kamwe haiwezi kuendelea kuwa wazi.
Kimsingi, ofisi hiyo ikiendelea kuwa wazi kwani naibu mpya wa rais hajaapishwa rasmi, hali hiyo inakiuka katiba. Kwa upande mwengine, chama cha United Democratic Alliance, UDA cha Rais Rutokinajiandaa upya baada ya naibu kiongozi wao Rigathi Gachagua kutimuliwa. Kwa mujibu wa katibu mkuu Hassan Omar Hassan, mipango mipya inasukwa.
Harakati za Gachagua za kusitisha mchakato wa ofisi ya naibu wa rais kujazwa zimekuwa zikiambulia patupu tangu alipokosoa uamuzi wa naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu wa kuteua jopo la majaji watatu.