Tanzania na Afrika ya Kusini Zaingia Makubaliano ya Ushirikiano wa Teknolojia ya Anga

Nchi ya Tanzania pamoja na Afrika ya Kusini zimeingia makubaliano kushirikiana katika teknolojia ya anga wakati nchi ikijiandaa kurusha satelaiti yake ya kwanza mwaka 2026.

Akizungumza leo Oktoba 31,2024 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Taaluma, Dkt.Petro Ernest amesema Teknolojia ya anga inasaidia Maendeleo katika nyanja tofauti tofauti kwani inajumuisha Mambo mengi yamayohusu maisha ya mwanadamu.

“Unaweza kutumia Teknolojia ya anga ukagundua sehemu gani Kuna madini mbalimbali ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya maendeleo ya nchi na hayo maendeleo yakamgusa mtu wa sehemu husika”Amesema.

Amesema Teknolojia ya anga kwa kutumia Satelaiti inakupatia nafasi ya kuangalia mipaka ya nchi jambo ambalo linahakikisha ulinzi wa nchi.

Amesema teknolojia ya anga ni kwa ajili ya watu wote kwani hata katika masuala ya kilimo inaweza kusaidia kutambua ugonjwa ambao umevamia kwenye mazao na kukuoatia suluhisho.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Baraza la Teknolojia Dar es salaam,Mhandisi Dkt. Richard Masika ameishukuru serikali kwa juhudi zake kwani imesaidia taasisi ya teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuingia katika mchakato wa kurusha Satelaiti ya kwanza nchini.

Masika amesema ushirikiano huo unaipatia nchi fursa katika upande wa kujengewa uwezo sambamba na kuunda Satelaiti hapa nchi ambayo inatarajiwa kurushwa mwaka 2026 ambapo baada ya hapo Satelaiti zitakazofuata nchi itakuwa imepata uzoefu wa kuunda bila utegemezi.

Pamoja na hayo Dkt.Masika amesema kupitia ushirikiano huo na nchi ya Afrika kusini katika makubaliano yao wamekubali kuigawia nchi nafasi ya udhamini wa masomo kwenye masuala ya anga katika kada ya uzamili pamoja na uzamivu.

Nae Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Afrika Kusini, Dkt.Bonginkosi Nzimande amesema makubaliano hayo yatasaidia kubadilishana ujuzi kwa pande zote mbili ambapo kila sehemu itawajibika kutoa ujuzi ambao wanao.



Related Posts