TENGENI BAJETI KABLA YA KUTWAA ARDHI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema taasisi yoyote ambayo inahitaji kutwa ardhi ambapo wananchi wanaishi au wanafanya shughuli mbalimbali za maendeleo lazima iwe imetenga bajeti ya kuwafidia kabla ya kufanyika kwa zoezi hilo ili kuondoa usumbufu.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 31, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kusini, Ali Kasinge ambaye alitaka kujua kwa nini Serikali isione uwezekano wa kuruhusu watu waliofanyiwa tathmini kwa ajili ya kutwali maeneo yao wasiruhusiwe kuyaendeleza wakati wakisubiri kulipwa fidia.

“…Utwaaji huo unapaswa kuzingatia sheria, nitoe wito kwa taasisi zote ziwe za umma au sekta binafsi pale ambapo wanafikiria kuanzisha mradi na mradi huo unagusa maeneo ya wananchi ni lazima wajipange kwanza kibajeti kabla hawajaenda kufanya tathmini ili wanapokwenda kufanya tathmini ukipata gharama unalipa mara moja na wananchi waweze kupisha na kwenda eneo lingine.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa na Mabaraza ya madiwani wazifuatilie Halmashauri ili kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye mwongozo wa fedha wa sheria ya Serikali za Mitaa inayoelekeza utengwaji wa fedha zinazopatikana kwenye mapato ya ndani ya halmashauri na kuzitumia kwenye utekelezaji wa miradi.

Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI inapofanya ufuatiliaji ijiridhishe moja kati ya ajenda ni kufuatilia upelekaji wa fedha za maendeleo zilizotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ili wananchi waweze kupata maendeleo wanayoyahitaji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Asia Halamga aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu halmashauri ambazo hazifuati takwa la kisheria la kupeleka asilimia 20 ya mapato ya ndani katika vijiji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Related Posts