Mnamo Jumatano, Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, aliibua hisia za watu alipoonekana akiingia kwenye gari la taka lilioandikwa jina lake katika mkutano wa kampeni wa chama chake huko Green Bay, Wisconsin. Trump, aliyekuwa amevaa vest ya usalama yenye rangi ya machungwa na njano, alitumia tukio hilo kujibu matamshi ya Rais Joe Biden aliyosema kuwa “wafuasi wa Trump ndio taka taka pekee ninayoiona.”
Akiwa ndani ya gari hilo la taka, Trump aliuliza waandishi, “Mnaonaje gari langu la taka? Hii ni kwa heshima ya Kamala na Joe Biden.” Kauli hiyo imeibua mjadala, hasa ikizingatiwa kwamba Trump alitumia fursa hiyo kuendeleza mashambulizi dhidi ya wapinzani wake wa chama cha Democrats.
Biden, baada ya matamshi yake kuhusu “taka,” alijaribu kufafanua kuwa alilenga kupinga jinsi Trump alibyokuwa akiwadhalilisha Wamarekani wenye asili ya kilatino, akisisitiza kuwa hiyo haionyeshi maadili ya taifa hilo. Hata hivyo, Trump aliendelea kujibu kwa njia ya dhihaka, akitoa kauli zake akiwa ndani ya gari hilo la taka na kuonyesha kutoshughulishwa na matamshi ya Biden.
Baada ya muda mfupi, Trump aliondoka kwenye gari hilo na kuelekea jukwaani kwa mkutano huo wa kampeni huku bado akiwa amevaa vest yake ya machungwa, akiendeleza ujumbe wake kwa wapiga kura wake.