Na WMJJWM, Dodoma.
Serikali imejidhatiti kutatua changamoto zinazowakumba vijana balehe kwa kuweka mazingira salama na rafiki kwa vijana kupitia afua mbalimbali zinazowawezesha vijana kufikia malengo yao na utimilifu wao kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera ,Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi akifungua mkutano wa wadau wanaotekeleza Afua za Vijana Balehe nchini (NAIA)kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum unaofanyika kuanzia 31 Oktoba hadi 01 Novemba ,2024 Mkoani Dodoma.
Dkt Yonazi amefafanua kwamba Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe nchini iliyozinduliwa Aprili 17,2021 ilikua na lengo ni kuharakisha utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele vinavyohusu afya na maendeleo ya vijana balehe katika Mikoa 13 yenye viashiria visivyoridhisha kuhusu afya na maendeleo ya vijana balehe nchini.
“Utekelezaji wa Ajenda umejikita katika nguzo kuu 6 za ambazo ni kuzuia maambukizi ya VVU, kutokomeza mimba za utotoni, kutokomeza ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia, kuboresha hali ya lishe, kuhakikisha wavulana na wasichana wanabaki shule kukamilisha mzunguko wao wa elimu, na kuwaendeleza vijana katika ujuzi na ufundi ili wapate fursa ya kujiari na kuajiriwa.” amesema Dkt. Yonazi
Vile vile Dkt. Yonazi ametoa rai kwa wadau wote wanaohusika na masuala ya vijana balehe kufahamu kwamba ili kuwa na Taifa imara la leo na baadae ni vema kuwekeza katika kutatua changamoto za vijana balehe leo ikiwa na maana ya kutatua changamoto za vijana kwa ajili ya kupata taifa imara.
“Kaulimbiu ya mkutano huu inayosema Utatuzi wa Changamoto za Vijana balehe kwa taifa imara inachechemua utekelezaji wa Ajenda hii kwa upana wake kwa kuwa ndiyo pekee yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo za vijana kwa sasa hivyo ni matumaini yangu kuwa kupitia mkutano huu, mtapata fursa ya kujadili kwa undani kuhusu changamoto zinazohusu vijana balehe kwa kutumia uzoefu wa utekelezaji wa Ajenda hii kwa kipindi cha miaka mitatu.” amesema Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ametambua juhudi za Mashirika ya Kimataifa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyoanzisha miradi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Vijana Balehe wanapata huduma rafiki za afya, elimu ya afya ya uzazi na kupata ujuzi na maarifa ya kuwafanya vijana wamudu maisha yao.
“Mafanikio haya hayajaja hivi hivi, bali ni jitihada kubwa mlizofanya ninyi Wadau wa Maendeleo kwa kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeunda Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, hivyo nachukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati kwa ushirikiano huo mlioonesha na kufanikisha malengo ya Ajenda hii.” amesema Wakili Mpanju
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahela amewakumbusha vijana kujitunza kwa kuzingatia mila na tamaduni za kitanzania zinazofaa na kuepukana kuiga kila wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa niaba ya wadau, Mwakilishi kutoka Shirika linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF), Edgar Lungu ameishukuru Serikali kwa kuwezesha wadau kuweza kutekeleza afua zao na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kufanikisha kusudio la Serikali kuwa na taifa lililo na vijana imara na taifa imara.