Afya ya akili tishio kwa watoto wa kike

Dar es Salaam. Oktoba 11, Tanzania ilipoungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya mtoto wa kike, ilielezwa kuwa kundi hilo liko kwenye hatari kubwa ya kupata matatizo ya afya ya akili kutokana na kupitia vitendo vya ukatili hasa wa kingono na kimwili.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Msichana Initiative imeonesha kuwa kwa asilimia 75 wasichana wanaokutana na vitendo vya ukatili wako hatarini kupata matatizo ya afya ya akili kutokana na kutopata msaada na huduma za kisaikolojia baada ya matukio wanayopitia.

Utafiti huo uliolenga kuangalia haki na ustawi wa wasichana ulifanyika katika mikoa 20 ya Tanzania Bara ukihusisha wahojiwa 346.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mtafiti kiongozi Wakili Fundikira Wazambi alisema suala la afya ya akili limeonekana kuwa tishio zaidi kwa watoto wa kike kwa kuwa wanakutana na matukio mengi ya ukatili na hawapati tiba za kuwajenga kiakili na kisaikojia.

Wazambi alieleza kuwa asilimia 75 ya watu waliohojiwa kwenye utafiti huo walikiri kwamba tatizo hilo limeanza kuonekana kwenye jamii ikiwa ni matokeo ya kuficha vitendo vya ukatili vinavyofanyika bila kujua vinaacha madhara makubwa kisaikolojia kwa waathirika.

Akichambua takwimu hiyo Wazambi alisema asilimia 43 ya wahojiwa walieleza kuwa changamoto ya afya ya akili kwa watoto wa kike ni tatizo kubwa huku asilimia 32 wakieleza wanafahamu kwamba hilo ni tatizo la kati.

“Kilichopo ni kwamba wasichana wanakutana na aina mbalimbali za ukatili wa kingono ikiwemo ubakaji, ulawiti, ndoa za utotoni sasa haya yote yanapofanyika lazima itamletea shida kisaikolojia.

“Sasa kama hatopata huduma za kisaikolojia na kwenye jamii yetu wengi hawapati, tunasikia mtoto kabakwa kesi zinaisha ndani ya familia au mtuhumiwa anakamatwa lakini hakuna kinachonyika kumuweka sawa yule mtoto,” alisema Wazambi.

Mtafiti huyo alieleza kuwa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambako kulikuwa na njia moja ya ukatili sasa watoto wa kike ukatili kwa njia ya mitandao ambako wanaingizwa katika mitego ya kutuma picha zao za utupu na kutishiwa kusambazwa wasipotoa ushirikiano.

“Jamii inaweza kuona kwamba kitendo kimeshafanyika hivyo maisha yanaendelea, haiko hivyo kwenye kichwa cha mtoto kwani kile kitendo kinaacha alama anaweza kuwa na msongo wa mawazo na ndiyo hiki kinachoonekana kwenye utafiti huko mbeleni hatari zaidi inakuja,” alisema.

Mbali na hilo utafiti huo umeonesha kuwa licha ya Serikali kutoa fursa sawa kwa watoto wote kupata elimu, watoto wa kike wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali kuifikia fursa hiyo.

Alivitaja vikwazo hivyo ni umaskini kwa asilimia 75, ndoa za utotoni asilimia 67, wazazi kuwashawishi wasiendelee na masomo asilimia 65 na ukatili asilimia 58.

Vikwazo vingine ni kukosa elimu ya afya ya uzazi, kukosekana kwa miundombinu muhimu shuleni ikiwemo maji na vyumba vya kujistiri hali inayowafanya kukosa masomo wakati wa hedhi asilimia 58.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, mwanaharakati Dk Hellen Kijo Bisimba alisema msingi wa changamoto zote anazokutana nazo mtoto wa kike ni kukosa elimu.

Dk Hellen alieleza kuwa endapo mtoto wa kike atapata haki ya elimu ni rahisi kwake kujikomboa kifikra na kukabiliana na aina zote ukandamizaji.

“Ili msichana aweze kujiamini na kukataa mambo yasiyofaa ni lazima awe na elimu, zawadi kubwa ambayo unaweza kumpatia mtoto wako wa kike ni kuhakikisha anapata elimu kwa kuwa itamsaidia katika maisha yake yote.

“Jitihada nyingi zimefanyika, hatuwezi kulinganisha Tanzania ya sasa na ya miaka ya 90 kwenye suala zima la haki wa wanawake na watoto wa kike lakini bado kuna mengi yanahitajika kufanyika ili kuwa na fursa sawa na kutengeneza jamii imara,” alisema Dk Hellen.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) Martha Makalla alisema licha ya Serikali kutoa mwongozo wa kurudi shule kwa watoto waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito bado kuna changamoto katika utekelezaji wa mwongozo huo.

Alisema changamoto hizo zinachangia wasichana wengi kutoitumia fursa hiyo kwa sababu mbalimbali ikiwemo hofu ya unyanyapaa na kutotengenezewa mazingira wezeshi kwa wao kurudi hasa katika mfumo rasmi wa elimu.

“Kuna kundi kubwa la wasichana wanakatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba na ndoa za utotoni. Kuwarudisha hawa ni muhimu hili suala liwe la kisheria siyo matakwa ya mtu hii itasaidia kuwa na uendelevu na usimamizi wake utakuwa mzuri,” alisema Martha.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts