Ajira 203,280 zazalishwa Zanzibar | Mwananchi

Unguja. Katika kipindi cha miaka minne Zanzibar imezalisha ajira 203,280 zilizo rasmi na zisizo rasmi ndani na nje ya nchi.

Ajira hizo ni sawa na asilimia 68 ya ajira 300,000 zilizoahidiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipoingia madarakani Novemba 2020.

Hayo yameelezwa jana na Waziri Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff alipokuwa akizungumzia  mafanikio katika sekta ya kazi, ajira, usalama na afya kazini, uwezeshaji wananchi kiuchumi na uwekezaji ikiwa ni shamrashamra za kuelekea kutimiza miaka minne ya uongozi wa Rais Mwinyi.

“Kati ya ajira hizo za  wanaume ni 98,166 sawa na asilimia 48.2 na wanawake ni 105,114 sawa na asilimia 51.7,” amesema.

Amesema ajira za nje ya nchi ni 8,769, wanaume wakiwa 1,179 na wanawake 7,590 zimepatikana kutoka nchi tofauti zikiwamo za Oman, Qatar na Dubai, Saudi Arabia, Maldives, Sychelles, Kuwait na U.A.E.

Ajira hizo amesema zimepatikana kwa kushirikiana na Taasisi za Uwakala Binafsi Zanzibar.

Kuhusu usimamizi wa viwango vya kazi, amesema wameratibu utekelezaji wa sheria za kazi ambapo jumla ya taasisi 1,442, Unguja zikiwa 992 na Pemba 450 zimefanyiwa ukaguzi kwa lengo la kusimamia na kulinda haki na masilahi ya wafanyakazi, kuratibu ulipaji kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi kutoka Sh300,000 hadi Sh347,000 na kwa taasisi ndogo kutoka Sh180,000 hadi Sh250,000.

Kwa wafanyakazi wa majumbani alisema ni kutoka Sh80,000 hadi Sh100,000 na Sh120,000 kwa wanaokwenda na kurudi majumbani mwao.

Shariff amesema katia kipindi hicho, mikataba ya kazi 37,455, kati ya hiyo Unguja 33,298 na Pemba 4,157 imethibitishwa kwa wafanyakazi wazawa.

Ndani ya kipindi hicho, amesema migogoro 636 ya kazi imesuluhishwa na kutolewa uamuzi kati ya 743 iliyopokewa katika kitengo cha usuluhishi na uamuzi wa migogoro.

Amesema vibali vya kazi 10,558 vimetolewa kwa wafanyakazi wa kigeni wanaofanya kazi nchini, huku ukusanyaji wa mapato kupitia masuala ya kazi ukiongezeka kutoka Sh7.119 bilioni hadi kufikia Sh9.158 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 129 ya makadirio.

Akizungumzia mafanikio katika sekta ya usalama na afya kazini, Shariff amesema kanuni tatu zinazohusu usalama katika nyanja ya afya zimeandaliwa, ambazo ni kanuni ya huduma ya kwanza kazini, na ya kuripoti matukio ya ajali na maradhi yatokanayo na kazi.

Amesema sehemu za kazi 785, kati ya hizo 561 za Unguja na 224 za Pemba zimefanyiwa ukaguzi wa usalama na afya kazini. Pia kufanya uchunguzi wa matukio ya ajali 15 za sehemu za kazi na maradhi yatokanayo na kazi.

Amesema umefanyika usajili wa maeneo ya kazi 434, yakiwamo 280 ya Unguja na Pemba 154 kwa ajili ya usalama na afya kazini.

Uwezeshaji wananchi kiuchumi

Amesema mikopo  yenye thamani ya Sh33.192 bilioni imetolewa kupitia programu ya Inuka kwa wananchi 21,689.

Katika utoaji wa mafunzo kwa wananchi na wajasiriamali, wafugaji wa nyuki 542 wamenufaika kupitia kituo cha Kizimbani, Unguja na 620 wakifunzwa kupitia kituo cha Pujini, Pemba.

Amesema ili kuwezesha upatikanaji wa viwango vya ubora vya bidhaa, huduma na masoko, gharama kwa bidhaa za wajasiriamali zimepunguzwa kutoka Sh700,000 hadi Sh50,000 kwa kusaini mkataba na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS).

Kuhusu uwezeshaji kupitia uanzishaji na mabadiliko ya utendaji kwa vyama vya ushirika, amesema Serikali imewaunganisha wazalishaji na wajasiriamali 4,115 kupitia vyama miamvuli vya sekta ya uvuvi, ushoni, uanikaji dagaa, uzalishaji wa maziwa na uzalishaji wa mpunga na kufaidika na mafunzo, mikopo na masoko ya pamoja.

Katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo ya vyama vya ushirika, amesema umeimarishwa na kusajili vyama 5,951.

Vyama vya ushirika 4,350 vyenye wanachama 29,711 vimepatiwa mafunzo, huku ukifanyika ukaguzi wa vyama 2,649.

Amesema migogoro 27 iliyojitokeza kwenye vyama vya ushirika imetatuliwa.

Wakizungumza mafanikio hayo baadhi ya wajasirimali licha kupongeza hatua hiyo, wamesema bado kuna changamoto katika upatikanaji mikopo.

“Kwenye mikopo bado hakujawa na utaratibu mzuri, hata elimu inahitajika kwa wananchi kwani kuna mzunguko mkubwa ambao unakatisha tamaa,” amesema Idd Khamis Juma, mjasirimali eneo la Kibandamaiti.

Related Posts