AKILI ZA KIJIWENI: Kwa Pacome Tuweke akiba ya maneno

PACOME atabaki Yanga kwa kuongeza mkataba mpya au ataondoka na kujiunga na timu nyingine ndivyo tunavyojiuliza hapa kijiweni.

Jamaa mmoja kibabe anatamba kuwa Pacome hawezi kuondoka kirahisi pale mitaa ya Twiga na Jangwani. Huyu anayesema hivi ni shabiki wa kulialia wa Yanga na hapa huwa tunamtania kuwa amekunywa maji ya bendera ya Yanga.

Mwanayanga huyu anasema kuwa kwa sasa timu yake ina mzigo wa kutosha wa kuweza kumfanya Pacome aongeze mkataba kama ilivyofanya kwa Stephane Aziz Ki na pia projekti yake inashawishi mchezaji wa daraja hilo kuwepo kwa vile inaukaribia ubingwa wa Afrika.

Jamaa anaongezea kwamba maisha ya Tanzania ni matamu hasa kwa mchezaji staa na ndani Pacome ana hadhi hiyo kutokana na kile ambacho amekifanya katika muda ambao ameichezea timu hiyo.

Pembeni kuna shabiki aliyekunywa maji ya bendera ya Simba amemua kumbishia jamaa na  anampiga mkwara kabisa kuwa timu yake ipo chini ya Mtanzania tajiri kuliko wote hivyo akiamua kuonyesha jeuri ya fedha kumpata Pacome hashindwi.

Huyu Mwanasimba yeye anaamini kwamba Pacome katoka kwao Ivory Coast kuja Tanzania kwa ajili ya kutafuta fedha na masuala ya mapenzi ya timu au kukubalika na mashabiki wa Jangwani wala sio kipaumbele kwake.

Kiuhalisia hiki kinachotokea , atakayenufaika zaidi ni Pacome mwenyewe maana hizi hisia za mashabiki wa timu hizo hapa kijiweni hazipishani sana na kile ambacho kipo vichwani mwa viongozi wao.

Simba wataweka dau nono ili kuhakikisha Pacome wanampata na hilo litaifanya hata Yanga kutumia kiasi kikubwa cha noti ili kuzuia mchezaji wao kipenzi asiende kwa watani wao wa jadi.

Vita ya panzi furaha kwa kunguru ndio kama ilivyo kwenye hili la Pacome. Vigogo vya Kariakoo vikipimana ubavu, yeye ndio anavuta mamilioni ya fedha.

Related Posts