AKILI ZA KIJIWENI: Marefa wanashindana kufanya makosa

KUIGA kitu kizuri sio jambo baya na hasa kile kinachoigwa kinagusa moja kwa moja umma kwa hisia chanya badala ya hasi.

Ukiwauliza swali marefa wengi wa kibongo kwamba wanataka kuwa kama nani basi utaorodheshewa majina ya marefa wakubwa wanaofanya vizuri duniani.

Hao marefa wakubwa duniani hawajapata huo umaarufu kwa bahati ya mtende bali uchezeshaji wao mzuri na kuepuka ufanyaji makosa ya mara kwa mara ambayo yanaweza kuwafanya wapoteze kuaminika na kukosa fursa ya kuchezesha mashindano makubwa.

Tunategemea kuona waamuzi wetu kwa vile maroli modo wao ni hao marefa wakubwa ambao wanaepuka kufanya makosa ya mara kwa mara pindi wanapochezesha basi na wao wangewaiga kwa kufanya hivyo.

Hatusemi kwamba wasifanye makosa kwani wao ni binadamu hawajakamilika na hata hao waamuzi maarufu huwa wanakosea ila isiwe mara kwa mara sasa kama wetu huku wanavyofanya.

Imefika hatua hawa marefa wetu ni kama wanashindana kutoa maamuzi yasiyo sahihi hadi wanatupunguzia uhondo wa ligi yetu ambayo kwa sasa inashika nafasi ya sita kwa ubora barani Afrika.

Unakuta mechi ya jana refa katoa penalti ya mchongo, refa wa leo anakataa bao halali la timu, kesho anashindwa kutoa kadi kwa mchezaji aliyefanya faulo au kosa linalostahili kadi na keshokutwa timu fulani inaadhibiwa kwa kuotea huku ikiwa haijafanya hivyo.

Katika hali ya kushangaza kuna marefa wamekuwa wakirudiarudia makosa iwe wameadhibiwa au hata wakiwa hajaadhibiwa hadi inaonekana kama wanafanya makusudi kwa yale wanayoyaamua.

Wabadilike aiseeh maana dunia ni kama kijiji na ligi yetu inaonekana hivi sasa hivyo watu wengi wanaifuatilia hadi mabosi wao huko Caf na FIFA.

Related Posts