Mshtakiwa wa kesi ya ubakaji, Damas Gwimile ameangua kilio katika Mahakama ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani wakati akisomewa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela pamoja na viboko 12.
Gwimile, ambaye ni mkazi wa Kidimu wilayani Kibaha, alihukumiwa baada ya Mahakama kuthibitisha pasipo shaka kwamba alitenda kosa la kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 19 (jina limehifadhiwa).
Mbali na adhabu hiyo, Mahakama pia imemwamuru Gwimile kulipa faini ya Sh200, 000 na fidia ya Sh1,000,000 kwa binti huyo.
Hukumu hiyo imesomwa leo, Novemba mosi, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Emmael Lukumay, ambaye alisema Mahakama imesikiliza ushahidi wa pande zote na kujiridhisha kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Katika hukumu hiyo, hakimu alisema, “Hukumu ni ndefu siwezi kuisoma yote ila kwa kuzingatia mwenendo wa ushahidi uliotolewa na pande zote, ikiwemo binti aliyebakwa ambaye hatuwezi kutaja jina lake, Mahakama imebaini kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.”
Kabla ya hukumu hiyo kusomwa, mshtakiwa aliulizwa ikiwa yuko tayari kwa hukumu, na alikubali kwa sauti ya upole.
Hakimu alibainisha kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulikuwa na nguvu, licha ya mshtakiwa kuleta mashahidi kadhaa, akiwemo mkewe.
“Ushahidi umetolewa pande zote, hata hivyo, mahakama imeuona ushahidi wa upande wa mashtaka una nguvu kwa kuzingatia taswira na mkusanyiko wa mambo mengi,” amesema.
Baada ya kutoa maelezo hayo, mshtakiwa alianza kulia kwa sauti ya chini huku akifuta machozi.
Hakimu aliwaamuru mshtakiwa pamoja na ndugu waliokuwepo kutoka nje ya Mahakama ili hukumu iweze kusomwa baada ya muda mfupi.
Baadaye, mshtakiwa huyo alirudishwa mahabusu iliyopo mahakamani hapo, huku akiendelea kulia kwa sauti na kutaja majina ya watu likiwemo jina la mwanamke akisema “umenifunga wakati nilikusomesha.”
Baada ya muda, hakimu aliagiza mshtakiwa huyo aitwe ili kuendelea na hatua inayofuata ambapo alirejea akisindikizwa na askari polisi huku akiendelea kulia
Baada ya kuingia ndani ya chumba cha Mahakama hakimu kabla ya kusoma hukumu alimpa nafasi ya kujitetea, ndipo mshtakiwa aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana mzigo wa familia, au apewe kifungo cha nje.
“Mheshimiwa naomba ikikupendeza nipunguziwe kifungo au nifungwe kifungo cha nje, lakini mimi sijaridhika na adhabu hii, nitakata rufaa naomba nipate nakala ya hukumu,” alisema Gwimile.
Pia, aliomba binti aliyemshtaki kusimama mbele ya Mahakama kuthibitisha kama alimbaka, lakini Hakimu alimjibu kuwa muda wa uthibitisho umepita, na sasa ni wakati wa hukumu.
Baada ya utetezi wake, hakimu alimhukumu kifungo cha miaka 30, faini ya Sh200,000, fidia ya Sh 1,000,000 na viboko 12.
Katika kesi hiyo ilielezwa kuwa Gwimile alitenda kosa hilo Februari 23, 2024, nyumbani kwao Kidimu.
Inadaiwa kuwa alikuwa akiishi na binti huyo kama mwanafamilia kwa sababu ana undugu na mkewe na siku ya tukio alimpeleka mkewe hospitalini kujifungua na aliporudi, ndipo alipomkuta binti huyo na kufanya kitendo hicho.