Askofu Lugendo atoa ushahidi dhidi ya Kanisa la Anglikana

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mbeya, Julias Lugendo (64) ameieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, kuwa Katiba ya Kanisa la Anglikana ya mwaka 1970 pamoja na Katiba ya Dayosisi ya Dar es Salaam ya mwaka huo zilibariki Askofu Mkuu wa kwanza wa kanisa hilo, marehemu John Sepeku apewe ekari  20 kama zawadi, baada ya kustaafu nafasi hiyo.

Lugendo ametoa ushahidi huo leo, Novemba mosi, 2024, katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na mtoto wa Sepeku, Bernardo Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa kanisa hilo pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Bernado, amefungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Askofu Sepeku inadaiwa alipewa zawadi na kanisa hilo ambayo ni nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo, kama askofu wa mkuu wa kwanza kanisa hilo.

Hata hivyo, mdaiwa wa tatu katika kesi hiyo, Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd, hajawahi kufika mahakamani hapo tangu kesi hiyo ilipofunguliwa licha ya kupokea wito wa kuitwa mahakamani hapo na wala hakupeleka mwakilishi.

Katika kesi hiyo, Bernardo anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.

Pia anaomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambazo zingepatikana baada ya kukomaa mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.

Akitoa ushahidi wake, mbele ya Jaji Arafa Msafiri, Askofu Lugendo ambaye ni pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Kanisa hilo, amedai kuwa kifungu cha 21 cha katiba ya kanisa la Anglikana na kifungu cha 23 cha katiba ya Dayosisi ya Dar es Salaam, vinaeleza wazi kuwa Bodi ya Wadhamini haina mamlaka ya kutengua maamuzi au kutoa mali iliyopitishwa na kikao cha Sinodi.

“Maamuzi yaliyofanywa au yanayofanywa na sinodi yana thamani kubwa na bodi ya wadhamini haina mamlaka ya kubadilisha chochote kilichopitishwa na kikao hicho,” alisema askofu Lugendo.

Lugendo alidai kuwa alitawazwa kuwa padri wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Machi 1985 na baada ya hapo alifanya kazi Dayosisi ya Dar es Salaam kwa miaka 30 kama padri kwenye parokia mbalimbali.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Deogratias Butawantemi, Lugendo amedai kuwa anafahamu kama Sepeku alipewa zawadi ya shamba lenye ukubwa wa ekari 20 kupitia mkutano mkuu wa Sinodi uliofanyika mwaka 1980.

Amesema mkutano huo ndio uliopendekeza Sepeku apewe nyumba na kiwanja.

Lugendo ambaye ni shahidi wa tatu wa upande wa mlalamikaji, amedai kuwa Agosti 7, 2024 alisajili ushahidi wake kwa njia ya maandishi mahakamani hapo kwa ajili ya kesi iliyopo mahakamani hapo.

Hata hivyo, maelezo hayo ya ushahidi aliomba mahakama iyapokee kama kielelezo katika kesi hiyo, ombi ambalo lilikubaliwa na Jaji Msafiri.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, Wakili wa mdaiwa wa kwanza na wa pili katika kesi hiyo, Dennis Malamba amemuuliza maswali ya dodoso shahidi na hii ni sehemu tu ya baadhi ya maswali hayo.

Wakili: Shahidi wewe ni mmoja wa wadhamini wa Kanisa la Anglikana?

Wakili: Na kazi yako kubwa kama wadhamini ni kulinda mali za kanisa, si ndiyo?

Wakili: Je, uwepo wako hapa mahakamani huoni unakinzana na kiapo chako ulichotoa wakati unatoa ushahidi?

Shahidi: Haukinzani na kiapo chochote.

Wakili: Ujio wako umekuja kama mdhamini wa Kanisa la Anglikana au kama shahidi wa kawaida?

Shahidi: Shahidi wa kawaida.

Wakili: Hilo eneo ambalo lipo katika mgogoro lina ukubwa gani?

Shahidi: Ekari zisizopungua 20

Wakili: Na eneo zima? Lina ukubwa gani

Shahidi: Shamba lina ekari 430.

Wakili: Na sio ekari 410?

Wakili: Kwenye hizo ekari 430, wewe umejimilikisha ekari moja na kitu, si ndiyo?

Shahidi: Sijajimilikisha, nimepewa na ni ekari 1.8

Wakili: Na eneo hilo umekodisha watu unachukua hela kwa maana ya kodi, ni kweli?

Shahidi: Ndio, nina mpangaji mmoja.

Wakili: Kwa nafasi yako wewe, unajua eneo lote lile ni la kanisa?

Shahidi: Nitafsirie vizuri

Wakili: Nasema hivi, lile eneo ulilopewa ni la kanisa?

Shahidi: Dayosisi ya Dar es Salaam.

Wakili: Kiutaratibu, wewe mpaka sasa upo katika bodi ya wadhamini ya kanisa la Anglikana, sasa utaratibu wa mali nani anatakiwa akupe?

Shahidi: Mali inatolewa na dayosisi, halafu dayosisi inaitaarifu bodi ya wadhamini.

Wakili: Je, hizo ekari 410 zilishawahi kuwa chini ya umiliki wa mtu mwingine kabla ya kuwa chini ya bodi ya wadhamini?

Wakili: Shahidi jibu ndio au hapana, ndio majibu ninayotaka hapa.

Jaji: Shahidi sikiliza swali vizuri, halafu jibu, haya wakili uliza tena swali lako.

Wakili: Shahidi nimekuuliza, hizo ekari 410 zilishawahi kuwa chini ya umiliki wa mtu mwingine kabla ya kuwa chini ya bodi ya wadhamini?

Wakili: Nikisema hilo shamba ni mali ya Kanisa la Anglikana Tanzania nitakuwa sahihi?

Shahidi: Ni mali ya kanisa.

Wakili: Na hiyo ekari 1.8 ambayo unayo wewe, huoni kama unalidhulumu kanisa?

Shahidi: Sidhulumu kanisa na wala haihitaji maelezo.

Wakili: Umekuja kutoa ushahidi kwa sababu na wewe una miliki eneo ambalo ni la kanisa?

Shahidi: Sina maana hiyo.

Wakili: Katika maelezo yako, inaonekana wewe ndio umehudumu kwa muda mrefu kuliko maaskofu wengine, ni sahihi?

Wakili: Kanisa la Anglikana Tanzania lina dayosisi 28, hebu tuambie mchakato ukoje kama mali inataka kutolewa na kupewa mtu mwingine, huwa mnafanyaje?

Shahidi: Mali inatolewa baada ya kupitishwa na mkutano mtakatifu wa Sinodi na sio vinginevyo.

Related Posts