Dar es Salaam. Licha ya mpangilio maalumu wa kula ‘diet’ wenye lengo la kupunguza uzito wa mwili au unene kuwa na faida, wataalamu wa afya wanasema si kila mtu anashauriwa kutumia njia hiyo, wakiwemo wagonjwa wa vidonda vya tumbo.
Wataalamu wanasema mgonjwa wa vidonda vya tumbo anapofanya diet ya kujinyima chakula, husababisha kuta za tumbo zilizopata athari kuchimbika zaidi kutokana na asidi inayomwagika tumboni kwa lengo la kulainisha chakula.
Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji na magonjwa ya mfumo wa chakula na ini kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Andrew Swalo anasema, “asidi inatengenezwa ndani ya tumbo, inachujwa na kuja katika nafasi ya wazi ya tumbo inakaa pale, yenyewe ina kazi maalumu ya kuua vijidudu vyote vinavyoingia na chakula. Kinapokaa chakula ile asidi haigusani kabisa na seli zilizotengenezwa. Tumbo likiwa tupu inakwenda moja kwa moja kwenye kuta za tumbo na kama kuna mchubuko au kidonda inachimba zaidi.”
Hata hivyo, Dk Samuel Shitta anasema iwapo diet isipozingatia kanuni za afya, inaweza kuchangia kupata vidonda vya tumbo.
“Mfano kama mtu anashinda njaa muda mrefu bila kula kitu, ili tu kupunguza mwili, hapa anakuwa amekiuka kanuni za afya. Kwa sababu kushinda njaa muda mrefu si njia sahihi ya kudhibiti uzito wa mwili.
“Kwa sababu tumbo likiwa tupu mara kwa mara huwa na kawaida ya kutiririsha tindikali na juisi za tumboni ambayo inaharibu utando laini wa kuta ya tumbo, hatimaye kutengeneza kidonda au vidonda. Hivyo, hii inaweza kumweka mtu katika hatari ya kupata vidonda zaidi au kama tayari kuna vijimchubuko basi itaongeza ukubwa wa tatizo,” anasema.
Dk Shitta anasema vidonda vya tumbo vinaweza kusababisha kifo kutokana na utumbo kupasuka na kuvujisha damu, endapo kidonda hicho kipo katika eneo ambalo kuna mishipa mikubwa ya damu.
Anasema uvujaji damu tumboni ni jambo la dharula na lisipodhibitiwa mgonjwa atapoteza maisha kutokana na damu kuvuja kwa wingi.
“Sababu ya pili ya kifo kama vidonda vikipasuka ndani ya mfumo wa chakula huwa ni bakteria rafiki, kukitokea mpasuko hupata nafasi ya kuhamia eneo lingine na huko husababisha shambulizi kali katika moja ya tando ya mfumo wa chakula linalojulikana kama ‘Peritonitis’. Hili ni tatizo la dharula, nalo lisipodhibitiwa husababisha kifo. Ingawa ni tatizo linajitokeza mara chache sana,” anasema.
Anasema vidonda vya tumbo ni jereha linalosababisha uwepo wa kidonda, “ukuta wa tumbo una tabaka nne na mgonjwa husemekana kuwa na ugonjwa wa vidonda vya tumbo wakati kidonda kinapofikia safu ya tatu.”
Mtaalamu wa mazoezi ya afya na mkufunzi kutoka Chuo cha American Sports Medicine ACSM, Dk Waziri Ndonde anasema changamoto kubwa wengi huitumia diet kwa lengo la kupungua uzito na kukonda na hivyo huanza kujinyima chakula.
Dk Ndonde anasema baadhi ya diet zinapunguza makundi fulani ya vyakula, ambayo inaweza kusababisha mwili kukosa virutubishi muhimu kama vitamini, madini au nyuzinyuzi.
Anasema nyingine zinazopunguza sana kalori zinasababisha njaa, uchovu na kupoteza nguvu mwilini. Hii inaathiri uwezo wa kufanya kazi za kila siku na mazoezi.
“Diet zinazoondoa vyakula fulani au kupunguza ulaji wa mafuta kwa kiasi kikubwa zinaathiri homoni zinazohusiana na njaa, uchovu na kusababisha matatizo ya afya ya muda mrefu,” anasema.
Hata hivyo, anasema baadhi yake ni vigumu kuzifuata kwa muda mrefu na mara nyingi uzito unarudi tena baada ya kuacha, lakini pia inaathiri afya ya akili.
“Kufuatilia diet kali kwa muda mrefu kunaweza kusababisha msongo wa mawazo, kujiona vibaya au kuwa na wasiwasi juu ya chakula unachokula, lakini pia kupunguza kalori kupita kiasi kunapunguza kasi ya mchakato wa metabolism na kufanya iwe vigumu kupunguza uzito baada ya muda fulani,” anasema.
Hata hivyo, Dk Ndonde anataja njia sahihi ya kufanya diet kupungua uzito kuwa ni pamoja na kuchagua lishe bora na yenye uwiano kwa kuepuka diet kali na zinazopunguza vyakula vya msingi kama wanga au mafuta.
“Usijinyime chakula kupita kiasi, wala kupunguza kalori kwa kiasi kikubwa, jitahidi kula kwa kiasi kwa uwiano mzuri.
“Mshirikishe mtaalamu wa afya kabla ya kuanza diet yoyote ,ni bora kushauriana na daktari au mtaalamu wa lishe ili kuhakikisha inafaa kwa mwili wako na hali yako ya kiafya,” anasema.
Dk Shita anasema kwa kawaida mfumo wa chakula huwa na tando inayozalisha ute mzito mfano wa ute wa yai, uliojitandaza na upo katika kuta za mfumo wa chakula.
Anasema kazi yake ni kuzuia na kulinda tindikali ya tumbo ambayo ni ‘Hydrochloric acid’ isikwangue tishu za kuta za tumbo kwa kuvunja vunja kikemikali tishu hizo.
“Tindikali ya hiyo kazi yake ni kuvunja vunja vyakula na vile vile kuweka mazingira rafiki ya kikemikali kwa vimeng’enya vya mfumo wa chakula kufanya kazi yake ya kuvunja vunja vyakula,” anasema.
Dk Shita anasema upungufu wa ute huo au kuharibiwa kwa ute huo kunaweza kusababisha tindikali ya mfumo wa chakula kupenya na kuvunja vunja tishu za kuta na kutengeneza vidonda.
Anasema vidonda huwa ni vijimkwanyuko au kumenyeka kwa tishu za kuta za mfumo wa chakula katika eneo la mfuko wa chakula na sehemu ya juu ya utumbo mdogo.
“Si kweli kwamba maziwa ni dawa ya vidonda vya tumbo, kupotea kwa maumivu baada ya kunywa maziwa kunatokana na maziwa kuweka kajitando kwa muda tu, lakini hapo baadaye maumivu hurudi kwa kuwa maziwa yenyewe ndani yake yana tindikali hivyo kuchochea tatizo,” anafafanua.
Pia anataja uambukizi sugu wa bakteria wa H.Pylori na matumizi holela ya dawa za maumivu, kuwa visababishi vikuu vya ugonjwa wa vidonda vya tumbo.
Bakteria hao ‘helicobacter pylori’ huingia kwenye mwili na kujificha ndani ya mfumo wa chakula ambao hushambulia safu ya ute wa tumbo ambayo kwa kawaida hulinda tumbo na utumbo mwembamba dhidi ya asidi ya tumbo.
Anataja mambo mengine yanayochochea ugonjwa huo kuwa ni uambukizi sugu wa bakteria wa H.Pylori na dawa za maumivu kundi la NSAIDS kama vile Ibuprofen, Aspirini na Diclofenac, “Hii inahusisha kwa wale wenye utumiaji holela au utumiaji kwa muda mrefu.”
Akielezea kwanini wengine wanapata vidonda na wengine hawapati, Dk Swalo anasema bakteria wa H.Pylori huingia tumboni mwa kubebwa na chakula ambacho kimeguswa na kinyesi.
“Bakteria huyu anaishi kwenye kinyesi cha binadamu. Magonjwa mengi ya tumbo ya kuharisha tunayapata kwenye vinywaji au chakula kilichochanganyika na kinyesi. Bakteria huyu akiingia tumboni anakwenda kuishi kwenye kuta za tumbo, akiingia ataharibu uwiano wa nguvu tetezi zilizopo ndani ya tumbo na akifanikiwa kuchimba asidi ikija itaingia moja kwa moja kwenye kile kidonda itachimba pale.
“Itaendelea kupachimba kwa kuwa kila siku tumbo linatengeneza asidi ya kutosha mpaka kinakuwa kidonda,” anasema Dk Swalo.
Dk Roland Kogoe ambaye ni daktari wa magonjwa ya tumbo na mtaalamu wa magonjwa kutoka Chuo Kikuu Campus mjini Lome, Togo pia anataja bakteria wa H. pylori kuwa hupatikana katika asilimia 90 ya wagonjwa wanaopata vidonda vya tumbo.
“Tunapozungumzia sababu za vidonda tutatofautisha aina mbili, kwanza ni maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori ambao tunawapata tukiwa wadogo kwa kula vitu mbalimbali ambao husababisha uzalishaji mwingi wa asidi tumboni inayoweza kusababisha kidonda,” anasema Dk Kogoe.
“Sababu ya pili ya vidonda ni tabia fulani na mambo ya maisha, ambayo yanaweza kuchangia kuongezeka kwa bakteria hao au kuzidisha vidonda vilivyopo, ikiwemo kukaa kwa muda mrefu bila kula na kutumia dawa za maumivu, hususani aspirini au ibuprofen pamoja na pombe kupita kiasi.”
Dk Kogoe anayataja mambo mengine kuwa ni matumizi ya pombe kupita kiasi, uvutaji na matumizi ya tumbaku, vyakula vyenye viungo vingi au vyenye tindikali nyingi, msongo wa mawazo au shinikizo la muda mrefu la akili, tiba za mionzi na kuugua muda mrefu au kulazwa muda mrefu.
Dk Shita anasema kisayansi, matibabu ya tatizo hili ni kutibu uambukizi wa vijidudu vya H.Pylori kwa mseto wa dawa tatu hadi nne na kwamba ndani ya dawa hizo kuna antibaotiki na dawa za kupunguza au kuzuia tindikali ya tumbo.
“Hakuna dawa mbadala au za kienyeji ambazo zimethibitishwa kuponya vidonda vya tumbo. Epuka matibabu ya dawa za mtaani na mitandaoni,” anasema.