Benki ya Dunia yaridhisha maradi wa HEET chuo Kikuu Mzumbe

Benki ya Dunia imeonesha kuridhishwa na hatua za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo ya kisasa pamoja na kituo cha kuendeleza ubunifu (incubation center) katika Chuo Kikuu Mzumbe. Mradi huu, unaogharimu shilingi bilioni 13.2, unalenga kusaidia kukuza elimu ya juu kwa kuongeza fursa za udahili na kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunza chuoni hapo.

Mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mpango wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ukiwa na lengo la kuboresha miundombinu muhimu kwa ufundishaji na utafiti wa kisasa. Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ya juu nchini kwa kuboresha mazingira ya kupata elimu na kuhamasisha ubunifu miongoni mwa wanafunzi.

Akizungumza katika hafla ya kukagua maendeleo ya mradi huo, mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bi. Roberta Malee, alisema mradi huo ni moja ya juhudi za benki hiyo kuimarisha elimu ya juu barani Afrika kwa kuboresha vifaa vya kufundishia na kukuza utafiti unaoendana na mahitaji ya kiuchumi ya sasa. Aliipongeza timu ya usimamizi wa mradi kwa hatua iliyofikiwa na akabainisha kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha malengo ya mradi huo.

Kwa upande wake, Profesa William Mwegoha, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, alisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kuimarisha elimu na kuongeza nafasi za udahili kwa vijana wanaotamani kupata elimu ya juu. Alisema, kukamilika kwa mradi huo kutaboresha mazingira ya kujifunza, hivyo kuwandaa wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.

Aidha, mkandarasi mkazi wa mradi huo, Bw. Fadhili Msemo, alieleza kuwa kazi ya ujenzi inaendelea vizuri na ipo katika hatua za mwisho. Amesema kuwa timu yake inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaohitajika ili wanafunzi wapate fursa bora za kujifunza na kujiendeleza. Bw. Msemo aliongeza kuwa, mradi huu ni fursa kwa jamii inayozunguka chuo, ikizingatiwa kuwa baadhi ya wafanyakazi kwenye mradi huo wanatoka katika maeneo ya karibu.

Related Posts