Dar es Salaam. Wakati maswali yakiendelea kugonga vichwa vya watu ndani na nje ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) kuhusu nani atakuwa mgombea urais mwakani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai amesema, “Mwaka 2025 huenda kukawa na ‘surprise’ kubwa kuliko nyingine yoyote au watu wanavyotegemea.”
Jacob ambaye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ya Chadema amesema kuanzia uchaguzi wa mwaka 2005, 2010, 2015 na ule wa 2020 mgombea urais ndani ya chama hicho amekuwa hatabiriki na ndicho kinatarajiwa kutokea mwakani.
Mjumbe huyo wa kamati kuu ya Chadema amesema hayo Jumatano ya Oktoba 30, 2024 katika mahojiano maalumu na waandishi pamoja na wahariri wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) alipotembelea ofisi za kampuni zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.
Alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Meya huyo wa zamani wa Kinondoni na baadaye Ubungo, kabla ya kujibu alitafakari kwa sekunde kadhaa kisha akasema, “Sina uhakika sana, kwa muda wangu wa miaka 19 niliokaa ndani ya Chadema, ni chama chenye ‘surprise’ (kushangaza) kuhusu mgombea urais.”
Alisema Chadema haitabiriki akieleza hakuna mwaka ambao chama hicho kilisema mgombea urais atasimama mtu fulani na ikatokea vivyo hivyo.
Alitoa mfano baadhi ya watu hawakuamini kama Mbowe (Freeman- Mwenyekiti wa Chadema) angeshindana na Kikwete (Jakaya) katika mbio za urais za mwaka 2005.
Mbowe aligombea baada ya aliyetarajiwa (hakumtaja) kukataa.
Alisema mwaka 2010, ilikuwa agombee hayati Samuel Sitta (Spika wa Bunge mstaafu) lakini akakataa dakika za mwisho, badala yake aligombea Dk Willibrod Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Katika uchaguzi huo alishika nafasi ya pili baada ya kupata asilimia 27.05 dhidi ya mgombea wa CCM, Kikwete aliyekuwa na asilimia 62.83.
“Kama hiyo haitoshi, mwaka 2015 watu walijua wanamsimamisha tena Slaa ambaye alipelekwa hadi mafunzoni Marekani kwa ajili ya jukumu hilo, pamoja na mkewe kwenye mafunzo ya U-first lady lakini upepo ulibadilika akaja Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa aliyechuana na Dk John Magufuli,” alisema.
Katika uchaguzi huo, Chadema kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioundwa na vyama vya NLD, NCCR- Mageuzi, CUF na Chadema ilimuunga mkono Lowassa aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97 mbele ya Dk Magufuli aliyeibuka kidedea kwa kura milioni 8.8 sawa na asilimia 54.47.
Vivyo hivyo, mwaka 2020 Jacob anasema watu wote walijua waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu angegombea urais, lakini Tundu Lissu alirejea kutoka Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu na kuongoza jahazi hilo.
Lissu alirejea nchini kwa mara ya kwanza tangu alipoondoka usiku wa Septemba 7, 2017 kwenda Hospitali ya Nairobi, Kenya kupatiwa matibabu baada ya alasiri ya siku hiyo kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana.
Alikutana na kadhia hiyo akiwa ndani ya gari kabla ya kushuka nyumbani kwake Area D, jijini Dodoma, akitoka kushiriki vikao vya Bunge, wakati huo akiwa Mbunge wa Singida Mashariki. Alitibiwa Nairobi hadi Januari ya 2018 alipohamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi. Tanzania alirejea Julai 2020.
“Mwaka 2025 huenda kukawa na surprise kubwa kuliko nyingine yoyote au watu wanavyotegemea, tunawaza huyu au yule, lakini anatokea mtu mwingine tofauti kabisa atakayekimbiza mchakamchaka hadi pakukaa hakuna.
“Hata mimi niliye ndani ya Chadema kinanitisha, kimekuwa ni chama cha kuja na surprise, pale kinapoona kuna masilahi ya chama na wananchi au kuiondoa CCM basi kimekuwa chama kisicho na uoga wa kufanya uamuzi wa kutafuta mgombea urais mahali popote mwenye sifa,” anasema.
Jacob anasema kuna watu wanaotajwa kuwania mbio hizo kwa tiketi ya chama hicho, lakini amewataka Watanzania wasubiri muda mwafaka, huenda kukawa na surprise kuhusu jambo hilo.
Licha ya Jacob kutowataja, lakini majina ambayo kwenye viunga vya Chadema yanatajwa kuwania urais ni Lissu na Mbowe. Tayari Lissu amekwisha kuandika barua rasmi kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika kuhusu azma yake na Mnyika alithibitisha kuipokea.
Duru za siasa ndani ya Chadema zinaeleza wawili hao mmoja anaweza kupewa fursa ya kuwania nafasi hiyo. Bado Mbowe hajathibitisha kutaka kuwania nafasi hiyo kama alivyofanya Lissu.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema ni mapema kuzungumzia mchakato huo, kwa kuwa chama hicho kinakabiliwa na mambo mawili makubwa kwa siku za usoni, ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
“Ni maoni yake si mjumbe wa kamati kuu, kwa sasa chama hakiwezi kuzungumzia hilo, muda ukifika tutaeleza mchakato utakavyokuwa ila si sasa bado mapema.
“Hivi sasa uchaguzi mkuu wa ndani utakaofanyika Desemba mwaka huu na serikali za mitaa, kuhusu uchaguzi wa urais bado upo mbali tutautolea maoni wakati ukifika,” anasema Mrema.
Anavyoiona Kamati Kuu ijayo
Katika mahojiano, Jacob alizungumzia ujio wa kamati kuu, akisema baadhi ya wajumbe walioondoka walikuwa wakifitinisha viongozi wakuu wa Chadema, akitoa mfano wa taarifa kuhusu Mbowe na Lissu (makamu mwenyekiti bara) zilikuwa nyingi kuliko uhalisia wenyewe.
“Muda mwingine hakuna shida, kunaonekana kuna shida lakini hakuna chochote bali kufitinisha, anakwenda kwa kiongozi huyu anaongea neno kisha anakwenda kwa mwingine anazungumza neno hili,” anasema.
Anasema wakati anamaliza ujumbe wa kamati mwaka 2020, anasema aliacha Chadema yenye watu wenye upendo na mshikamano.
“Ni Chadema ambayo usipopatikana kwenye simu watu wanachanganyikiwa na kuulizana yupo wapi? Lakini hapa katikati kuna baadhi ya watu wachache kutokana na uroho wao, walianza kutuchonganisha kwa kutengeneza taarifa zisizo za ukweli.
“Baada ya chaguzi hizi na watu wengine kurudi, naona Chadema yenye nguvu na upendo kuliko mwanzo. Chadema asili yake ni upendo, hatugombanii madaraka, bali majukumu hili afanye nani na lile litekelezwe na nani,” anasema.
Anasema matarajio yake awamu ijayo ya Kamati Kuu hakutakuwa tena na watu wachonganishi kama ilivyokuwa awali, Chadema itakuwa yenye upendo na watu wenye uchungu na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Mikakati uchaguzi serikali za mitaa
Jacob anasema Kanda ya Pwani imejipanga vyema katika kuhakikisha wananyakua mitaa, vitongoji na vijiji, akisema hadi sasa asilimia 95 ya wagombea wamesimamishwa kuwania nafasi hizo katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 27, 2024.
“Maeneo ya mijini ndiyo ngome zetu tunatarajia katika uchaguzi huu, tutapata viti vingi hasa Mkoa wa Dar es Salaam na tupo tayari kukabiliana na kila hujuma itakayojitokeza katika mchakato huu,” anasema.
Anasema kama kuna mawazo ya kwamba watu watapiga kura mara mbili basi wao (Chadema) wanawaza vivyo hivyo. Anasema amewaambia viongozi wenzake kwamba yeye si mwenyekiti wa kondoo wa kulialia.
“Kulialia tumechoka, tunakatisha watu tamaa, kama wenzetu watatumia ujanja huu na sisi tutatumia huohuo. Tumejipanga vizuri, hakuna mtu kususa,” anasema.
Amewataka wazazi na walezi kuwazuia watoto kusogea karibu na vituo vya kupiga kura kwani watakachokutana nacho wasilaumu. Msingi wa hilo ni madai kwamba wanafunzi walio chini ya miaka 18 wameandikishwa kupiga kura.
Katika mahojiano hayo, akijibu swali iwapo atawania ubunge wa Ubungo katika uchaguzi ujao, alisema ana sababu tatu za kuwania nafasi hiyo kama alivyofanya mwaka 2020.
“Ubungo inahitaji mtu anayejua na kuwasemea kero zao, kuhamasisha shughuli za maendeleo na kuwatembelea mara kwa mara. Sifa hizo ninazo ndio maana nawania tena, licha ya mwaka 2020 kutotendewa haki katika uchaguzi huo.
“Ukiwa mbunge wa Ubungo, unakuwa mbunge na kiongozi wa kitaifa, si ubunge pakee, kwa sababu utakemea ufisadi, ukandamizaji, unyanyasaji, sheria mbovu na wizi. Jimbo la Ubungo linahitaji mbunge wa aina hii,” anasema.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Jacob alishindwa baada ya kupata kura 20,620 dhidi ya 63,221 alizozipata mgombea wa CCM, Profesa Kitila Mkumbo ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji).
Jacob anasema jimbo hilo linahitaji mtu au kiongozi atakayekuwa msaada wa kutatua changamoto za wananchi.