Sengerema. Naibu Waziri Mkuu Dk Dotto Biteko amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini kuboresha huduma za afya nchini kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Dk Biteko ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 1, 2024 alipokuwa akizindua jengo jipya la upasuaji kwenye Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema lililogharimu Sh5.4 bilioni, zikijumuisha na vifaatiba.
Amezihakikishia taasisi za dini kuwa Serikali itaendelea kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya hapa nchi, huku akiwataka watoa huduma za afya kuwahudumia wagonjwa ipasavyo wanapofika hospitalini.
“Serikali inathamini michango ya taasisi mbalimbali za dini hasa zinapowekeza katika sekta muhimu ya kuboresha huduma za afya, ndiyo maana leo tuko hapa kuzindua jengo hili,” amesema Biteko.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Sista Mery Jose amesema wanashirikiana na Serikali kutoa huduma za afya kwa pamoja katika hospitali hiyo.
Amesema kuzinduliwa jengo hili la kisasa la upasuaji kutaongeza huduma bora za upasuaji na madaktari wamejipanga kuzitoa.
Hospitali ya Sengerema ilianzishwa mwaka 1965 na masita sita kutoka uholanzi walianzisha kama kituo kidogo cha kuhudumia wagonjwa wa ukoma.
“Kwa sasa hospitali yetu inahudumia wagonjwa 80,000 kwa mwaka na inalaza wagonjwa 22,000 kwa mwaka tunendelea kutoa huduma bora za afya kila kukicha na kuokoa maisha ya watu,” amesema Sista Mery Jose.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na taasisi za dini kuwahudumia wananchi.
Amesema hospitali ya Sengerema inahudumia wagonjwa wanaotoka maeneo mbambali ikiwemo Geita, Buchosa, Nzera, Chato na maeneo mengine hivyo kuboresha miundombinu ya afya kutaongeza idadi ya watu wanaokuja kupata huduma ya afya.
“Jengo hili la upasuaji limejengwa na marafiki wetu wa Uholanzi ambao wamegharamia ujenzi wote kwa asilimia 100 tunawashukuru amesema Kasala,” amesema.
Baadhi wa wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameiomba Serikali iongeze nguvu kuajiri watoa huduma za afya ili kuwasaidia wananchi.