Familia yabainika kuzika mwili usio wa ndugu yao

Moshi. Mwili wa Richard Shoo (31) uko wapi? Hilo ni swali ambalo wanafamilia wanajiuliza, baada ya mwili waliokuwa wameuzika awali kubainika kuwa si wa ndugu yao, bali ni wa Jackson Joseph (29).

Ni siku 57 zimepita, tangu mwili huo uliokuwa ukigombaniwa na familia mbili kufukuliwa kwa amri ya Mahakama kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) na sasa majibu yametoka kuwa mwili huo haukuwa wa Richard Shoo, ulizikwa kimakosa na familia ya katika Kitongoji cha Dungi, Kijiji cha Kibosho Kindi, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mwili huo ambao awali ulidhaniwa wa Richard Shoo aliyefariki Juni 16, 2024 na kuzikwa Juni 25, ulifukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na vipimo vya DNA Septemba 4, 2024, baada ya familia ya Jackson Joseph kuibuka ikidai mwili uliozikwa sio wa Shoo bali wa kijana wao, Jackson Joseph.

Baada ya vipimo hivyo, majibu yametoka yakionyesha mwili huo ni wa Jackson Joseph na hivyo familia yake imekabidhiwa mwili kwa ajili ya taratibu za maziko, huku familia ya Shoo ikibaki na maswali kichwani kuhusu alipo Richard au mwili wake.

Mbali na kukosa majibu ya maswali hayo, familia ya Shoo imetilia shaka majibu ya vipimo na kuendelea kuamini ulikuwa mwili wa Shoo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtagwa alipoulizwa kuhusuana na suala hilo, ameomba apewe muda kulifuatilia ndipo atoe taarifa.

Familia ya Jackson yasimulia

Akizungumza leo Ijumaa Novemba 1, 2024, baada ya kupewa majibu ya DNA, Mama mzazi wa Jackson, Agness Ollomi amesema anashukuru kwa mwili wa kijana wake kupatikana na kwamba sasa wanaenda kujiandaa na taratibu za mazishi.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Huyu mtoto wangu alifariki Juni 16, 2024 akazikwa Kibisho Kindi katika mazingira ya kutatanisha Juni 25, 2024 na mimi nilipata taarifa za kifo chake kwa kuchelewa, nikaanza utaratibu wa kwenda polisi na hospitali kumtafuta, nikamkosa.

“Lakini baadaye tukaambiwa mwili ulizikwa Kibosho Kindi, tukafuatilia. Baadaye tukaenda mahakamani na kupewa kibali cha kuufukua mwili na ukapelekwa Hospitali ya KCMC kuhufadhiwa na sisi tukaambiwa tusubiri majibu ya vipimo ili kujua mwili ni wa nani,” amesema.

Amesema baada ya majibu sasa wanajiandaa kwa maziko yatakayofanyika Jumatatu, huko Msitu wa Tembo, mkoani Manyara.

Mama huyo ameeleza kuwa enzi za uhai wake, kijana alikuwa akiishi na mama yake mkubwa mjini Moshi na kwamba kwa mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa Mei mwaka huu.

Neema Silas ambaye ni dada wa marehemu amesema walikuwa wakiishi na Jackson eneo la Pasua Manispaa ya Moshi na kwamba taarifa za kifo chake walizipata baada ya wiki mbili kupita tangu auawe.

“Wakati tunafuatilia kuuluzia tukaambiwa kuna kijana alipigwa na alifariki,” amesema.

Ameeleza kuwa baada ya kupewa taarifa za kifo walifuatilia polisi na kuambiwa mwili huo ulishachukuliwa na kuzikwa Kibosho.

Familia ya Shoo yaibua utata

Korodius Shoo ambaye ni baba mzazi wa Richard Shoo amesema hawana imani na majibu ya DNA kwa kuwa wao wana uhakika mwili ni wa kijana wao.

Baba huyo akiwa na baadhi ya wanafamilia akiwemo mama mzazi wa kijana huyo ambao walionekana kuwa na uchungu na mawazo nje ya kituo kikuu cha polisi Mkoa wa Kilimanjaro mjini Moshi, alidai kuwa kijana wao alikuwa akiishi na mama yake mdogo Manispaa ya Moshi na baada ya kupewa taarifa za kifo chake walifika polisi ambapo walifuata taratibu zote na kukabidhiwa mwili ambao walikwenda kuuzika Juni 25 mwaka huu.

“Tulipewa taarifa kijana wetu aliuawa tukachukua mwili tukaenda kuzika, baadaye ilikuja hiyo familia nyingine na kudai tuliyemzika ni mtoto wao, mwili ulifukuliwa na leo tumeitwa polisi kuambiwa mwili ule si wetu, hatujui cha kufanya maana mpaka sasa hivi ninavyoongea mtoto wangu hayupo kabisa.

“Siamini kama mwanangu yupo hai maana baada ya nwili kufukuliwa tumemtafuta sana bila mafanikio na huwa hakai mjini muda mrefu bila kufika nyumbani kila baada ya wiki mbili,” amesema.

Akizungumzia kaburi walilokuwa wamemzika na baadaye kufukuliwa, amedai kuwa walilifunika kusubiri majibu ya vipimo na kwamba kwa sasa anakwenda kukaa na wazee ili kujua nini cha kufanya.

Mama mzazi wa Richard Shoo, Anna Kimaro ambaye awali alidai aliuangalia mwili na kujiridhisha ni wa mwanaye, leo ameshindwa kuzungumza na kuonekana akibubujikwa machozi.

Septemba mosi mwaka huu, polisi wakiambatana na madaktari wawili, walifika katika familia ya Shoo kwa ajili ya kufukua mwili huo, lakini ilishindikana baada ya familia kudai kutoshirikishwa na kutaka kuonyeshwa kibali cha mahakama cha kufukua mwili, ambacho hawakuwa nacho.

Septemba 4, 2024, familia zote mbili, zilifika mahakamani na amri ilitolewa kwa mara nyingine kaburi likafukuliwe ili mwili huo utolewe na kupimwa DNA, kujiridhisha ni wa nani.

Baada ya amri hiyo, askari polisi wakiambatana na madaktari wawili na familia ya Jackson, akiwemo mama yake mzazi, walifika nyumbani kwa Shoo kwa ajili ya kufukua kaburi hilo, ambapo pia kuliibuka vurugu za wananchi na familia wakionyesha hawajaridhishwa na kilichotaka kuendelea.

Hata hivyo baada ya mvutano huo uliochukua zaidi ya dakika 30, wananchi hao walitulia lakini wakagoma kutoa vifaa vya kufukua kaburi, hali iliyomlazimu mkuu wa upelelezi wilaya kutoa fedha na kuagiza kununuliwa machepeo mawili na shughuli hiyo kufanyika.

Baada ya kaburi hilo kufukuliwa, polisi waliondoka na jeneza lenye mwili na  kuupeleka kuuhifadhia katika Hospitali ya rufaa ya KCMC kwa uchunguzi na kuhifadhiwa hadi sasa unaposubiri taratibu za mazishi yatakayofanyika Novemba 4, 2024.

Related Posts