Hivi ndivyo ajali, kifo cha Sokoine kilivyotokea

Katika makala haya ya mwisho ya uchambuzi wa kitabu cha tawasifu cha “Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake,” tutaangazia namna ajali ya kiongozi huyo ilivyotokea hadi kusababisha kifo chake.

Vijana wengi waliozaliwa miaka ya 1980, hawakushuhudia msiba wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine baada ya kufariki dunia kwa ajali ya gari mkoani Morogoro.

Sokoine alifariki dunia Aprili 12, 1984 kwa ajali ya gari wakati akitoka Dodoma kuhudhuria mkutano wa Bunge akielekea Dar es Salaam.

Kitabu hicho kinaanza kwa kueleza saa tisa alasiri, Aprili 12, 1984, ghafla Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD – sasa TBC), redio ya Taifa na pekee Tanzania Bara wakati ule, inakatisha matangazo ya vipindi vyake vya kawaida, na kuwekwa wimbo wa Taifa, Mungu Ibariki Tanzania.

Kila mtu anashituka. Kwanza, kupigwa wimbo wa Taifa siku zote kuliashiria kujiri kwa jambo kubwa la kitaifa. Pili, halikuwa jambo la kawaida kwa wimbo wa Taifa kupigwa alasiri; kawaida wimbo huo ulipigwa jioni baada ya taarifa ya habari ya saa mbili usiku wakati wananchi wengi wako majumbani kwa ajili ya matangazo maalumu ya kitaifa, hasa hotuba za Rais Julius Nyerere.

Wimbo unamalizika, na sauti iliyozoeleka sana kwa wananchi, lakini zamu hii ikiwa na utulivu mkubwa, inaanza kuelezea taratibu tena kwa majonzi , ikisema: “Ndugu wananchi, leo mnamo saa saba mchana, ndugu yetu na kijana wetu, Edward Moringe Sokoine, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipokuwa anarudi Dar es Salaam kutoka Dodoma, gari yake ilipata ajali. Amefariki dunia.”

Kama kuna sentensi mbili tu zilizochukua chini ya dakika moja kutamkwa na Rais Nyerere katika maisha yake ya uongozi, lakini zikawa na kishindo, ni zile za kutangaza kifo cha Sokoine.

“Kifo kile kilikuwa ni msiba wa pili mkubwa wa kitaifa uliopata kutokea katika historia ya Tanzania; msiba wa kwanza wa kitaifa ulikuwa ni kuuawa kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Abeid Amani Karume, Aprili 7, 1972,” kinaeleza kitabu hicho.

Kitabu hicho kinaeleza kwamba, katika makala iliyochapishwa siku 11 baada ya kifo cha Sokoine, Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu, Accadoga Chiledi (sasa marehemu) anasema mwendo wa magari yaliyoandamana katika msafara huo ulikuwa wa kawaida, kati ya kilomita 110 na 130 kwa saa kwa sehemu zilizonyooka.

Chiledi alikaa katika gari lake la kawaida, mbele ya lile la Waziri Mkuu. Gari lililotangulia, la kusafisha njia, lilikuwa la Jeshi la Polisi, aina ya Peugeot 504, likifuatiwa na gari la maofisa wa usalama, na la tatu lilikuwa ni la Waziri Mkuu, Mercedes Benz.

Baada ya gari la Waziri Mkuu likafuata gari jingine la maofisa wa usalama na baadaye gari la wasaidizi wengine. Kwa sababu gari la polisi lilikuwa linaongoza msafara wa Waziri Mkuu hapakuwa na wasiwasi wa usalama, magari yote waliyokutana nayo yaliegeshwa pembeni mwa barabara.

Chiledi anasema: “Hata hivyo, dakika tano baada ya kuvuka Mto Wami, kiasi cha kama kilomita 40 hivi kutoka Morogoro, nilisikia kishindo kikubwa kikitokea nyuma yetu, kishindo cha mgongano wa vyuma. Gari la Waziri Mkuu lilikuwa limegongana na gari aina ya Toyota Landcruiser la kubeba mizigo. Sokoine hakuchukua muda. Alipoteza maisha muda mfupi baadaye kutokana na majeraha makubwa ambayo alikuwa ameyapata ya kichwani na kifuani.”

Tawasifu hiyo inabainisha kuwa, yapo maelezo mengi, mengine yakikinzana, kuhusu sababu za kifo cha Sokoine. Lakini cheti chake cha kifo nambari 10971, kilichotolewa Aprili 12, 1984 katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam, kinaeleza kuwa Sokoine alipoteza maisha yake kutokana na kuvunjikavunjika kwa viungo mbalimbali vya mwili wake (multiple fractures).

Cheti kilitiwa saini na mtaalamu wa patholojia, Profesa James Shaba, ambaye aliuchunguza mwili wa marehemu kufuatia ajali hiyo. Profesa Shaba alifariki dunia mwishoni mwa 2023.

Baadaye ilikuja kujulikana kuwa gari lile la Toyota Landcruiser la kubebea mizigo lilikuwa linaendeshwa na kijana wa Afrika Kusini, mpigania uhuru wa Chama cha African National Congress (ANC), Dumisani Dube, aliyekuwa na umri wa miaka 23. Chama cha ANC kilikuwa kinaendesha mapambano dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi zilizokuwa sera rasmi ya watawala Wazungu wachache huko Afrika Kusini.

Wakati huo ANC ikiendesha mapambano hayo kutokea makao makuu ya ugenini ya chama hicho yaliyokuwa Tanzania, na kilikuwa na shughuli zake katika makambi kadhaa, yakiwamo ya mkoani Morogoro. Dube hakuwa peke yake kwenye gari hilo; alikuwa na vijana wenzake wawili, Boycen Moyer na Percy George.

Naye Renata Mwanga, aliyekuwa msaidizi wa Sokoine amenukuliwa katika kitabu hicho akisema:

“Msafara ulikuwa unakwenda vizuri hadi tulipofika Wami -Dakawa, siyo mbali na Morogoro. Sikujua nini kilichokuwa kinatokea hadi niliposikia ghafla kishindo kikubwa… Nakumbuka gari letu liliacha njia na kwenda porini… tulipojizoazoa na kuamka na kuangalia mbele kwenye gari la Waziri Mkuu, nikamuona Waziri Mkuu amejeruhiwa vibaya…”

Mwanga pia anasema dereva wa Sokoine, Ali Abdallah, naye alikuwa amejeruhiwa katika ajali hiyo. Anasema hana uhakika kama Sokoine alifariki dunia papo hapo kwenye tukio la ajali ama wakati anakimbizwa kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, ama hospitalini kwenyewe.

“Katika ajali hiyo, mlinzi wake mmoja, Yusto Chuma, naye aliumia vibaya kiasi cha kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Waliompokea kwenye hospitali hiyo walidhani kuwa tayari alikuwa amekufa. Alizinduka akiwa kwenye chumba hicho cha kuhifadhi maiti,” kitabu hicho kinabainisha.

Wengine walioumia katika ajali hiyo ni Dube mwenyewe na vijana wenzake wawili aliokuwa nao kwenye gari. Sokoine ndiye alikuwa wa kwanza kuokolewa ama kuondolewa kwenye eneo la ajali. Aliwekwa kwenye gari la polisi la doria na kukimbizwa hospitali Morogoro, ambako madaktari walithibitisha kuwa alikuwa amekwishafariki.

Baadhi ya wasaidizi wa Sokoine waliingiwa na fadhaa kubwa baada ya kuwasili hospitalini Morogoro na kujulishwa kuwa bosi wao alikuwa amefariki dunia, na kuwa mwili wake ulikuwa chumba cha kuhifadhia maiti.

Kwa mfano, kumbukumbu za Mwanga kuhusu tukio hilo zinakoma baada ya kuwasili kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, alikozimia alipopata habari za kifo cha Sokoine.

Alipata fahamubaadaye mjini Dar es Salaam, alipojikuta nyumbani kwa Waziri Mkuu ambako maombolezo yalikuwa yakiendelea.

“Hakuna taarifa kamili ya jinsi ajali hiyo ilivyotokea. Jambo linaloonekana kukubaliwa na wengi ni kwamba gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser, likiendeshwa na Dube, liliingia barabara kuu ghafla na kwa kasi likitokea njia ya pembeni likiwa linapishana na msafara wa Sokoine.

“Lilikuwa likielekea Dakawa, inadhaniwa kwenye kambi ya ANC, likitumia Barabara Kuu ya Morogoro – Dodoma. Dube, kama wapigania uhuru wenzake wa ANC, alikuwa anaishi kwenye kambi yao iliyokuwa Dakawa, ambayo sasa imefanywa kuwa Chuo cha Ualimu kinachoandaa walimu wa kufundisha shule zinazofuata mtaala wa Kiingereza nchini,” kinasimulia kitabu hicho.

Dube alikuwa muuguzi katika kituo cha afya kwenye kambi hiyo. John Malecela, aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi (na baadaye Waziri Mkuu), anathibitisha kuwa Sokoine hakufunga mkanda wakati wa ajali hiyo. Wakati huo, kwa kweli, ufungaji mikanda ya magari haukuwa jambo lililozingatiwa sana.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts