Hizi hapa ahadi za TRA kwa wafanyabiashara

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewaahidi wawekezaji kuwa katika utendaji kazi wake wa kila siku haitakuwa juu ya sheria, bali itahakikisha inaweka mazingira mazuri ya biashara.

Pia imesema akaunti za wafanyabiashara hazitashikiliwa bila taratibu kufuatwa, huku ikiendelea kuwasikiliza ili kupata mrejesho utakaosaidia ufanyaji wa biashara.

Hayo yalisemwa jana Alhamisi Oktoba 31, 2024 jijini Dar es Salaam katika mkutano uliowakutanisha wawekezaji kutoka nje ya nchi ulioratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na TRA.

Kamishna wa TRA, Yusuph Mwenda amesema wanalenga kuhakikisha mazingira ya kodi na udhibiti nchini Tanzania yanakuwa rafiki kwa biashara kwa kadri iwezekanavyo, ili kuchochea uwekezaji mpya, upanuzi wa biashara na ushirikiano wa muda mrefu.

“TRA tutahakikisha hatuko juu ya sheria, tutatii sheria na tutafuata taratibu zinazostahili katika kutekeleza sheria za kodi,” amesema.

Mwenda amesema anatambua moja ya jambo linalowapa wasiwasi wawekezaji ni namna ya kurejesha madeni ya kodi za nyuma, hivyo watawasaidia kuhakikisha hawana madeni.

“Tutatoa elimu ya kodi ili kuhakikisha unalipa kodi kwa wakati na pale ambako kuna kodi ambazo hazijalipwa, tutafuata taratibu zinazostahili ili kuzikusanya,” amesema.

Amesema ukusanyaji kodi ulilalamikiwa kwa nyakati tofauti kutokana na utaratibu unaohusisha mtu wa tatu (Agency Notices).

Agency Notices ni maagizo yanayotolewa na TRA mara nyingi kwa benki au taasisi za kifedha zinazoitaka kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya mlipakodi, ili kulipia madeni ya kodi yaliyosalia. Agizo hilo hutumiwa kama njia ya mwisho wakati mlipakodi ameshindwa kulipa kodi zake kwa muda uliopangwa.

“Nimesema mara nyingi na ninataka kurudia hapa kwamba, kwetu matumizi ya Agency Notices ni hatua ya mwisho. Kabla ya kufikiwa tutahakikisha tumefanya kila kinachotakiwa kufanywa kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Amesema ili kutekeleza utaratibu huo, ni lazima kupeleka notisi ya madai kwa walipakodi, isipojibiwa mdaiwa atakumbushwa, ikiwa bado wataitwa na kukaa na TRA ili kuwasikiliza na kuwapa fursa ya kulipa kidogo-kigogo.

Amesema hilo likishindikana huwaandikia barua ya nia ya kutumia benki kama mawakala, na haiwezi kutumika iwapo kamishna mkuu hajathibitisha kuwa taratibu zimefuatwa.

Mbali na hilo, Mwenda amesema Serikali imeboresha mfumo wa forodha utakaopunguza mwingiliano wa watu, hasa kwenye tathmini ya bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi, jambo litakalochochea utozaji wa ushuru sahihi na ulipaji wa kodi stahiki.

“Serikali inawekeza sana kwenye mifumo ya uendeshaji ili kurahisisha ufanyaji biashara ndani ya nchi yetu. Yote haya yanalenga kuhakikisha mnatumia muda wenu mwingi kufanya biashara, kupata faida kubwa na kulipa kodi zinazostahili,” amesema.

Amewaasa wawekezaji wanaojihusisha na vitendo vya ukwepaji kodi kuhakikisha wanafuata sheria.

“Tuna baadhi yenu wanaokwepa kodi, wanapunguza thamani ya bidhaa zinazoagizwa, hili halikubaliki kutoka kwa wawekezaji wanaoheshimika kama ninyi. Dhamira yangu ni kwamba hatutavumilia hili. Tunaimarisha timu zetu za ukaguzi na uchunguzi na pale watakapokamatwa, hakutakuwa na maelewano yoyote kwao,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema jukwaa hilo linasaidia ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wawekezaji na kuyawasilisha kwa mamlaka husika.

“Tutashirikiana na wenzetu katika wizara, ikiwemo ile ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji na sehemu mbalimbali za Serikali kuhakikisha ujumbe mnaotupa leo (jana), tunaupeleka kwa mtu anayeweza kufanya jambo kuhusu hilo. Lakini pia ni jukwaa kwa ajili yetu kuwaeleza kuhusu huduma zetu mpya, vivutio tunavyotoa,” amesema.

Amesema matarajio yake ni jukwaa hilo kuwapa mwanga kuhusu fursa zilizopo zinazoweza kuwasaidia si tu kuanzisha na kukuza biashara, bali kupanua walizonazo.

“Tutakuwa nanyi kila hatua ya safari yenu, kuanzia wakati unapofikiria kuanzisha biashara yako, kama ulivyofanya miaka mingi iliyopita na baadhi yenu hivi karibuni hadi kwenye shughuli zako za kila siku, sisi ni mshirika wa ukuaji. Tanzania ni nchi yenye fursa na tunakusaidia kuzitumia fursa hizo kwa manufaa ya watu wa Tanzania na kampuni zote za uwekezaji tulizonazo kutoka kote duniani,” amesema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga amesema awali kulikuwa na changamoto ambazo wafanyabiashara walizipitia hasa katika eneo la kodi upande wa TRA.

Amesema kupitia majukwaa yanayofanyika kumekuwa na mabadiliko katika ukusanyaji kodi.

“Moja ya eneo ambalo TPSF inashukuru ni kuundwa kwa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Kodi na sisi tupo pale kuhakikisha mapendekezo ya kodi ya wafanyabisahara yanasikilizwa, kufanyiwa kazi na kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi stahiki, ya haki ili biashara ikue na kuleta maendeleo katika uchumi,” amesema.

Amesema moja ya malalamiko makubwa ni matumizi ya Agency Notice ambayo yalifanya wafanyabiashara wengi kufungiwa akaunti zao au mashine za risiti za kielektroniki (EFD), jambo lililowaumiza katika utendaji wa kila siku.

“Jambo hili tumeona TRA imefanyia kazi, imesitisha baadhi ya utolewaji wa hizo agency notice,” amesema.

Related Posts