Jinsi ya kutambua kama una tatizo la afya ya akili

Dar/Mikoani. Wakati wagonjwa wa afya ya akili wakiongezeka kila mwaka nchini, wataalamu wa saikolojia tiba wametaja viashiria vinavyoweza kumfanya mtu agundue kuwa tayari anaanza kupata changamoto katika afya yake ya akili.

Ikiwa unakosa usingizi, unasahau baadhi ya mambo, uzito umeongezeka ghafla au unashindwa kufanya vitu kwa usahihi, unapaswa kuwaona wataalamu wa afya mapema kwa kuwa hizo ni miongoni mwa dalili za tatizo la afya ya akili.

“Tabia ya kutokuwa na uhakika kama kitu umefanya au la, mfano umetoka nyumbani na umefunga mlango, lakini unajiuliza mara mbilimbili kama umefunga au la, kiasi cha kulazimika kurudi kugusa kitasa ni moja ya dalili za tatizo la afya ya  akili,” anasema Mtaalamu wa saikolojia tiba na afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Isaac Lema.

Anafafanua kuwa wapo wengi anapofunga mlango wazo lake halipo kwenye kufunga mlango, sasa wazo linapokuja ‘hivi nilifunga mlango’ asiye na changamoto ya afya ya akili atakumbuka haraka nilifunga.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mwaka 2023 ilibainisha kuongezeka kwa watu wenye changamoto hiyo. Ripoti hiyo iliyolenga hali ya afya ya akili kwa mwaka 2020, ilionyesha  changamoto hiyo imechangia asilimia 8.15 ya  vifo vya kujinyonga kwa kila watu 100,000.

Vivyo hivyo, mwaka 2022 ripoti ya Wizara ya Afya ilieleza kuwa mzigo wa maradhi ya afya ya akili umepanda kutoka wagonjwa 386,358 mwaka 2012 hadi 2,102,726 kufikia mwaka 2021 mtawalia, likiwa ni ongezeko la asilimia 82.

Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi 2024 waliohudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa shida ya magonjwa ya afya ya akili walikuwa 293,952 ikilinganishwa na 246,544 kwa kipindi cha mwaka 2022/23.

Katika kipindi hicho waliolazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya wenye magonjwa ya afya ya akili walikuwa 19,506 ikilinganishwa na 13,262 mwaka 2022/23.

‘Nitajuaje kuwa nina changamoto ya afya ya akili?’ Ni swali linalojibiwa na Dk Lema, akisema changamoto ya afya ya akili humpata mtu aliyekata tamaa au kuvunjika moyo, wakati huo huwa kwenye kiwango cha juu cha msongo wa mawazo. “Ili kuwaepushia hali kama hii, ndiyo sababu wengi hukimbilia kuwafariji walio na changamoto za misiba au kupotelewa na wapendwa wao.”

“Ukifiwa watu wanajitoa kuja kukuona, kukufariji na wafanyakazi hupewa wiki mbili kama ni mtu wako wa karibu, kwa kuwa huwa na kiwango cha juu cha msongo.

“Ukisikia lugha hizi kwenye jamii mtu anasema nimevurugwa, nimepigwa na kitu kizito unaelewa nini? Katika hali ya kawaida mtu hakubali kuvurugwa kama amekubali kiwango chake cha msongo kipo juu, ni matatizo ya afya ya akili,” anasema.

Dk Lema anasema matatizo ya afya ya akili si ugonjwa wa akili, akitolea mfano wa mtoto kuchukua kitu bila ruhusa ya mzazi. Kitendo hicho kikamsababishia mzazi uchungu na ghadhabu na kumkata mkono, huu uchungu na ghadhabu kupitiliza ni tatizo la afya ya akili.”

“Kama nimezaliwa kwenye familia yenye tatizo la ugonjwa wa akili basi vinasaba vyangu vina ugonjwa wa akili na mazingira yangu yakiwa ni yale ya kuonyesha ukatili, unyanyasaji inachochea kwenye mfumo wa akili kuleta mabadiliko ambayo baadaye tutaona, mwitikio wa mwili pamoja na fikra zangu haziko sawa.”

Dk Lema anasema kusikia sauti ambazo wengine hawazisikii ni dalili za ugonjwa wa akili, akitoa angalizo kuwa hiyo ni tofauti na imani za kidini.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Chris Mauki anasema, dalili za awali ni kukosa usingizi vizuri kunakosababisha wengine kuchukua hatua za kunywa kilevi au dawa ili alale, kukosa hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake na wanaume nayo ni dalili mojawapo.

Machi mwaka huu, CAG Charles Kichere kwenye ukaguzi wa ufanisi aliitaja Wizara ya Afya kama mfano wa ufanisi mdogo kwenye eneo la afya ya akili, akidai wizara imekuwa ikishughulika na watumiaji wa dawa za kulevya, wazee na wenye mimba za utotoni, huku ikiliacha kundi kubwa kwenye jamii likikosa huduma hiyo.

CAG alipendekeza kuongeza fedha kwa ajili ya huduma ya afya ya akili, huku Rais Samia Suluhu Hassan akisema “umeleta ombi jipya,” na kuiagiza Wizara ya Afya ifanyie  kazi mapungufu yaliyopo.

Akizungumzia utekelezaji wa agizo la Rais, Meneja Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu anasema tayari wizara imeandaa mkakati wa afya ya akili.

“Mkakati upo katika hatua za mwisho kukamilika, nadhani mwishoni mwa mwaka huu utakuwa umekamilika kabisa na umeanza kutumika, kwa sasa tupo na waratibu wa mikoa yote tunapitia ili kukamilisha hatua za mwisho,” anasema.

Dk Ubuguyu anasema pamoja na hayo wameshusha huduma mpaka ngazi za halmashauri kuanza kutibu na kulaza wenye changamoto hizo na wameshapokea maelekezo na kutekeleza uimarishaji wa huduma za utengamao nchi nzima, kwa sasa tayari hospitali za rufaa za mikoa zinatoa angalau huduma tatu za utengamao.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel anasema: “Serikali imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya kuboresha huduma za utengamao, Sh3 bilioni zitatumika kwenye miundombinu na Sh2 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa, pia teknolojia ya juu zaidi itatumika katika huduma hizo.”

Takwimu za watu wanaoripotiwa kuugua magonjwa ya afya ya akili zinaongezeka katika vituo mbalimbali vinavyotoa tiba ya afya ya akili nchini.

Katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH) imeelezwa kuongezeka kwa kipindi cha mwaka 2018/2023 kufuatia mfumo wa maisha na mwamko wa jamii kupeleka wagonjwa kupata tiba na kuondokana na mila potofu za kuhusisha tatizo hilo na ushirikina.

Daktari Bingwa wa afya na magonjwa ya akili hospitalini hapo, Stephano Mkakilwa anasema ongezeko hilo linatokana na wastani wa wagonjwa wa nje 2,500 mpaka 3,400 kwa kipindi cha mwaka 2018/2023

Kwa wagonjwa wa ndani limeongezeka kutoka 180 mpaka 250, sawa na asilimia 40, huku asilimia 70 ya wagonjwa ni wanaume na wanawake ni asilimia 30 pekee.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Venna Karia, hospitali hiyo hupokea wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili 360 hadi 400 kwa mwezi.

“Katika Hospitali ya Mawenzi, kwa mwaka tunapokea wagonjwa 4,700 hadi 5,000.”

“Kwa mwaka huu 2024 kuanzia Januari hadi Septemba tumepokea wagonjwa 3,305,” anasema.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Afya ya Akili Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC), Matiko Mwita wanapokea wagonjwa wa afya ya akili zaidi ya 50 kila wiki.“Tunawaona hapa kliniki na ni watu wa rika zote, kuna watoto, watu wazima hadi wazee.”

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917  

Related Posts