USIMKATIE mtu tamaa, ndio maneno ambayo unaweza kuyatumia kwenye ushindi wa Simba ikiwa ugenini baada ya kuichapa Mashujaa kwa bao 1-0, ushindi ukipatikana sekunde za mwisho huku mfungaji akiwa yule aliyekuwa anadhaniwa hawezi kuisaidia.
Simba ilipata bao hilo katika dakika ya saba kati ya sita zilizoongezwa na mwamuzi Omary Mdoe kutoka Tanga baada ya zile tisini kutimia likifungwa na mshambuliaji Steven Mukwala kwa kichwa akimalizia kona ya kiungo Awesu Awesu.
Simba ilihaha kupata ushindi katika mchezo huo lakini kumbe mpishi wa bao na hata mfungaji wote waliwasahau nje kufuatia wawili hao – Awesu na Mukwala kuanzia nje wakiingia kipindi cha pili na kutengeneza ushindi huo muhimu kwa Wekundu.
Ushindi huo wa Simba unakuwa wa saba msimu huu kwenye mechi tisa walizocheza wakifikisha pointi 22, huku wakiishusha Singida Black Stars iliyokuwa nafasi ya hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Kipindi cha kwanza Simba italazimika kulia na kipa wa Mashujaa, Eric Johola ambaye alisimama imara kulilinda lango lake akiokoa mashuti makali ya Wekundu hao yaliyokuwa yanaelekea wavuni.
Dakika ya 16 kiungo mshambuliaji Kibu Denis wa Simba aliachia shuti kali kupitia mpira wa adhabu ndogo lakini Johola alilipangua kwa umakini akiwanyima Wekundu hao kuandika bao la kwanza.
Kama haitoshi Johila tena alifanya kazi nyingine bora dakika ya 20 akiokoa shuti la Kibu tena aliyesetiwa vizuri na mwenzake Fabrice Ngoma aliyetangulia kukutana na kigugumizi cha miguu kumalizia krosi ya mshambuliaji Leonel Ateba iliyowapa shida mabeki wa Mashujaa
Wekundu wa Msimbazi hata kama wangeamua kucheza bila kipa ingewezekana kwenye mchezo huo baada ya kipa huyo kukosa kucheza shambulizi lolote la maana kutoka kwa wapinzani wao. Simba iliimiliki vizuri Mashujaa kwa mabeki wake kufanya kazi ndogo ya kukaba huku wakifanya kazi kubwa ya kupandisha mashambulizi.
Mashujaa ilikuwa inacheza nyuma ya mpira kwa muda mrefu ikicheza soka la kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza ambapo ndani ya dakika 90 ikatoka bila kupiga shuti lililolenga lango.
Mashujaa haikupoteza pointi tatu peke yake ikapoteza pia mapato ya kutosha baada ya idadi ndogo ya mashabiki walioingia kutazama mchezo huo tofauti na mechiu za nyuma baina ya timu hizo ambazo ziliingiza mashabiki wengi na kuufanya uwanja huo kufuruka, hali ikiwa tofauti jan