Kabila hili bila ‘kukonyeza’ hujapata mke au mume

Unajua Kabila la Waberber au Amazighs wana mila ya harusi ya ajabu, vijana wa kike na kiume hukusanywa pamoja na kucheza muziki usiku huku wakikonyezana kwa ridhaa ya wazazi wao?

Ni tamasha linalokutanisha takribani watu 30,000 la kijana kupata mke na binti kupata mume.

Ni mwendo wa kutaniana, kuchumbiana na kuoana, lugha ya mawasiliano kwenye muziki ni kutikisa kichwa na kukonyezana.

Waberber wanapatikana zaidi Afrika Kaskazini, kwenye nchi za Algeria, kaskazini mwa Mali, Morocco, Mauritania, kaskazini mwa Niger, Libya, Tunisia na sehemu ya magharibi ya Misri.

Jina Amazighs linaaminisha “watu huru” au “watu wa heshima”, wakati jina Berber linatokana na neno la Kimisri la “mgeni.”

Moja ya hafla maarufu za kimila za Berber ni tamasha la harusi la Imilchil.

Kila Septemba ya kila mwaka koo za wenyeji hukusanyika katika milima ya Atlas, ili kuruhusu vijana wa kiume na kike kukutana na kuoana katika tamasha la harusi.

Tamasha hilo linatokana na simulizi ya zamani inayohusishwa na sherehe hiyo kuhusu wapenzi wawili ambao hawakuweza kuoana kwa sababu ya familia zao zenye ugomvi.

Kijiji cha Imilchil kunakofanyika tamasha la ndoa kiko juu katika uwanda wa ziwa wa milima ya Atlas nchini Morocco.

Katika kijiji hiki cha ajabu kuna koo za Kabila la Berber ambao wana hisia kali za utamaduni na mila ambayo imehifadhiwa kwa miongo kadhaa.

Mila hiyo ni tamasha la ndoa ya Imilchil ambayo hufanyika Septemba ya kila mwaka.

Tamasha hili, pia linajulikana kama Septemba ‘Romance’ likihusisha utamaduni wa ndoa ya pamoja ya kila mwaka mabinti hutafuta na kuchagua waume wao.

Ni wakati ambao wasichana wenye bikra huvaa mapambo yao, vito vyao vya kifahari vya fedha na kucheza muziki kwa saa nyingi usiku chini ya mwanga wa nyota.

Kinachofanyika wakati wa kucheza muziki ni kutikisa kichwa na kukonyeza kama lugha ya mawasiliano kati ya vijana wa kiume na kike, kama mmoja amempenda mwenzake.

Vijana wa kiume kwa kawaida husaidiwa na marafiki katika kuchagua binti na kuondokana na aibu yoyote.

Mara wanapopokea ishara kutoka kwa binti, ikiwa wanakubali, wanaweza kushikana mikono kuonyesha nia, lakini kuachilia mkono mmoja huashiria kukataliwa.

Ikiwa bibi harusi anasema maneno kama: “Umekamata ini langu au ini langu liko kwa ajili yako”, ina maana amepata upendo wake.

Ini inachukuliwa kuwa eneo la upendo wa kweli kwa sababu katika utamaduni wa Berber inaaminika kuwa ini lenye afya husaidia usagaji chakula na kukuza ustawi.

 Iwapo kuna kibali kwa pande zote mbili, wanandoa hukutana na familia zao kwenye hema na maswali huulizwa na majadiliano hufanyika.

Baadaye, ndoa itapangwa kwa umakini zaidi katika kijiji cha nyumbani kwa wanandoa, ikiwa ndoa haina furaha, talaka inaruhusiwa.

Muziki ni sehemu kuu za tamasha, wanamuziki wa kienyeji hucheza nyimbo za kitamaduni za Kiberber kwa kutumia ala kama vile gumbri (aina ya lute) na bendir (ngoma ya mkono).

Muziki huunda hali ya uchangamfu na mara nyingi watu hujiunga kwenye miduara ya dansi ili kusherehekea pamoja.

Chimbuko la tamasha la ndoa

Tamasha hili lilizaliwa kutokana na simulizi inayohusisha vijana wawili, Isli na Tislet waliotaka kuoana lakini ikashindikana.

Kulingana na simulizi hiyo, Tislit alikuwa msichana mrembo wa kuvutia kutoka koo ya Ait Azza huko Imilchil.

Siku moja alipokuwa akitembea milimani, alikutana na Isli, kijana aliyekuwa akichunga mifugo kutoka koo ya jirani ya Aït Brahim.

Isli na Tislit waliunganishwa na hisia za mapenzi, walizungumza kwa saa kadhaa, na wakapendana.

Baada ya majaribio mengi bila mafanikio ya kushawishi koo zao kubariki ndoa kushindikana, walipoteza matumaini ya kuwa mke na mume.

Usiku mmoja wenye mwanga wa mbalamwezi, walikutana kwa siri kwenye mlima unaotenganisha makabila yao mawili.

Huzuni yao ilikuwa kubwa, walilia na machozi yao inaaminika ndiyo yaliunda maziwa mawili, ambayo sasa yanajulikana kwa majina yao.

Ziwa moja lilikuwa “Isli”, likimaanisha bwana harusi na lingine “Tislit”, likimaanisha bibi harusi.

Kukata tamaa kwao kulikuwa kukubwa sana; walijiua kwa kuzama kwenye maziwa hayo mawili.

Huzuni ilitawala miongoni mwa wanakijiji, kwa hiyo mila ilibadilishwa na familia zote zilitoa uhuru kamili kwa watoto wao kuolewa na yeyote waliyemchagua.

Ndio mwanzo wa tamasha la harusi ambapo koo za jirani hukusanyika pamoja karibu na maziwa hayo na mabinti huchagua waume zao.

Related Posts