Dar es Salaam. “Hakuna mfanyabiashara anayetamani kupata hasara’. Hii ni kauli ya Emmanuel Mkinga (29) mkulima wa mazao ya biashara wilayani Bagamoyo mkoani Pwani akielezea namna gharama za kuendesha shamba zinavyochangia kupunguza faida kwa mkulima.
Mkinga anasema: “Unavyofanya kilimo cha biashara kama mimi, lazima uhitaji uhakika wa umwagiliaji ambao mara nyingi tunatumia mafuta katika kuendesha mitambo yetu, gharama yake ni kubwa, hii inapunguza hata faida tunazozipata.”
Hata hivyo, mbadala wa matumizi wa nishati ya mafuta katika kilimo, wataalamu wanataja kuwa ni matumizi ya teknolojia ya umeme jua katika uzalishaji wa tija, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukwepa gharama kubwa za uendeshaji.
Kwa mujibu wa Takwimu za Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Sekta ya Kilimo nchini inachangia asilimia 26 katika Pato la Taifa.
Mtaalamu wa kilimo, Adili Panja akizungumza na Mwananchi anasema matumizi ya umeme jua katika sekta hiyo muhimu katika uchumi wa nchi kwa sasa ndio msingi wa kilimo hasa kwa maeneo ya vijijini ambako nishati ya umeme haijafika. Pia inatumika katika ukaushaji bora wa mazao.
“Utafiti unaonyesha asilimia 70-80 ya uanikaji mazao usio sahihi huathiri na hupoteza viinilishe, hivyo umeme wa sola husaidia kulinda mazao na mazingira,” anasema Panja.
Wakati Tanzania bado mwamko wa matumizi ya umeme jua ukiwa haujashika hatamu, tovuti ya Statista imezitaja nchi tano zinazoongoza kwa matumizi ya nishati hiyo jadidifu pamoja na faida wanazozipata.
“Kwa ripoti ya mwaka 2023, nchi zinazoongoza kwa matumizi ya umeme jua katika nyanja mbalimbali ikiwamo kilimo ni pamoja na: China, Marekani, India, Japan na Ujerumani,” imesema ripoti hiyo.
Mbali na suala la matumizi yake katika kukaushia mazao kama ilivyoelezwa na Panja, pia tovuti ya ‘Public of Solar’ katika Makala yake iliyochapishwa mwaka 2023 yenye kichwa cha habari; ‘Kuchunguza Matumizi ya Nishati ya Jua Katika Kilimo na Umwagiliaji’ imesema:
“Matumizi ya nishati ya jua katika kilimo endelevu yanaweza kusaidia kupunguza athari za mazingira ya kilimo huku ikiongeza mavuno ya mazao na kuboresha faida shambani.
“Pia, inaweza kutumika katika umwagiliaji kwenye kuwasha pampu za umwagiliaji na mifumo ya umwagiliaji kwa njia ya matone, ambayo inaweza kusaidia kupunguza upotevu wa maji na kuongeza mavuno ya mazao,” imesema tovuti hiyo.
Pia imesema, yapo maghala yanayotumia nishati ya jua katika kuimarisha mifumo ya udhibiti wa halijoto, lakini pia inatumika katika ‘green houses’ pamoja na kuruhusu wakulima kupanda mazao mwaka mzima na kupanua msimu wa kilimo.
Akizungumza na Mwananchi, Mchumi Mack Patrick anasema matumizi ya teknolojia mara nyingi yanapunguza gharama za uzalishaji hivyo kuongeza faida.
“Katika fomula ya kawaida tu ni kwamba teknolojia mara zote ni mkombozi hivyo, unavyoitumia vyema unakuwa katika nafasi ya kupunguza gharama za matumizi katika uzalishaji hasa katika masuala ya kilimo.
“Unavyopunguza matumizi ya uzalishaji, moja kwa moja unasababisha kuongezeka kwa wigo wa faida, hali hii pia itawafaidisha wakulima wanaotumia nishati ya umeme jua,” amesema Patricvk.
Aidha, Patrick amesema jambo lingine litakalosaidia ni kupunguza muda wa uzalishaji (time factor) ambapo kutokana na matumizi ya teknolojia muda wa kufanya uzalishaji utapungua huku ufanisi ukiongezeka zaidi.
Licha ya nishati hii kutoenea katika maeneo mengi nchini lakini msimamo wa Serikali ya Tanzania ni kuwa hadi kufikia mwaka 2025, matumizi ya nishati jadidifu yataongezeka kwa asilimia 80.
Hayo yalisemwa na Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika Mkutano wa 27 wa Kimataifa wa Tabianchi (COP-27) uliofanyika Sharm el-Sheikh nchini Misri Novemba 2022.
“Tutaendelea kuongeza vyanzo vya nishati jadidifu kutoka asilimia 60 mwaka 2015 mpaka asilimia 80 mwaka 2025,” alisema Rais Samia.