Kilio cha dawa kwa wenye changamoto ya afya ya akili

Dar es Salaam. Wakati takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la wanaougua magonjwa ya akili nchini, hali ya upatikanaji wa dawa kwa kundi hilo bado ni changamoto kutokana na gharama kubwa zinazohitajika.

Wagonjwa wa akili wanaoishi kwa kutumia dawa, hutumia kati ya Sh30,000 mpaka Sh60,000 kila mwezi kununua dawa kulingana na tatizo walilonalo na hizo ni dawa zilizo katika mfumo wa vituo vya umma.

Kwa wale waliopo katika mfumo wa kuendelea na tiba wakiwa nyumbani, wamelalamikia kununua dawa hizohizo kwa gharama ya juu zaidi, hali inayowafanya wengi wao kushindwa kuzimudu.

“Nilipata changamoto ya afya ya akili, kuna dawa ambazo nilipaswa kutumia na zingine naendelea kuzitumia kama Cariprazine, Carbamazepine na nyinginezo, zipo ninazopaswa kunywa kila siku na zinauzwa ghali,” anasema Neema John (26) mmoja kati ya maelfu ya wagonjwa wanaopitia changamoto hiyo nchini.

Hata hivyo, gharama zilizopatikana kwenye vituo vya tiba hiyo zinasema gharama hutofautiana kulingana na aina ya bima ya afya anayomiliki mgonjwa na kwa wale wasio na bima, hulipia gharama kulingana na tatizo lililobainika.

“Kweli gharama ipo, lakini wengine wanahitaji kupatiwa elimu ya saikolojia na wakarejea katika hali ya kawaida, lakini wengine wanapaswa kuwa katika uangalizi wa kupata tiba na kuhifadhiwa katika kituo maalumu au hospitali,” anasema daktari mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji.

Mtaalamu wa saikolojia, Saldin Kimangale anasema wagonjwa wanaopatiwa matibabu nyumbani hutumia takriban Sh30,000 kwa mwezi.

Kwa mgonjwa mwenye sonona, gharama inaweza kufikia Sh45,000 ikitegemea na dozi, kwa sababu wapo wanaohitaji dozi kubwa zaidi.

“Anayetumia miligramu moja hatalingana na anayetumia miligramu mbili; hata hivyo, gharama inaweza kufikia Sh60,000 kwa dozi ya juu,” anaeleza Kimangale.

Anasema kuna uchaguzi katika aina za dawa. Wagonjwa wengine huamua kutumia za gharama nafuu zinazopatikana hospitalini, wakati wengine hupendelea dawa maalumu ambazo bei zake ni kubwa zaidi.

Kwa upande wa watoto wenye changamoto za akili, kama vile wenye usonji, Kimangale anasema gharama zao ni kubwa zaidi. “Kundi hili halihitaji dawa pekee; linahitaji tiba mbalimbali kama vile mazoezi, tiba ya kuzungumza, na huduma zingine za kisaikolojia. Wengine hawatumii kabisa dawa, lakini wanahitaji huduma nyinginezo,” anasema Kimangale

Waziri Kivuli wa Afya wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dk Elizabeth Sanga anasema mgawanyo wa fedha za Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024-2025 haujatoa kipaumbele kwa huduma za afya ya akili.

Anabainisha kuwa hakuna sera ya afya ya akili na sheria ya afya ya akili ya mwaka 2008 imepitwa na wakati na haikidhi mahitaji ya sasa.

Akijibu suala hilo, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu anasema kila halmashauri hutakiwa kutenga asilimia 50 ya fedha zake za mapato kwa ajili ya matumizi ya dawa. Alifafanua kuwa mfumo ni uleule kwa dawa zote, lakini changamoto ya takwimu na kushindwa kufanya makadirio sahihi husababisha uhaba wa dawa.

Dk Ubuguyu anasema changamoto wanazokutana nazo wagonjwa wa afya ya akili ni upatikanaji wa dawa za madaraja ya juu, ambazo hazipatikani katika vituo vya afya vya halmashauri wala hospitali za rufaa za mkoa.

“Dawa za afya ya akili zinauzwa kwa bei ya chini, lakini zipo za madaraja ya juu ambazo zinahitaji kuzingatiwa kwenye utaratibu wa bima. Bima inaweza kukataa kugharamia dawa fulani kama haimo kwenye daraja la mgonjwa. Kwa mfano, dawa inayotakiwa kutolewa Muhimbili ikitolewa katika hospitali ya kawaida kama Mbagala Rangi Tatu, bima haitalipa kwa sababu wanalipia kulingana na mwongozo,” alisema Dk Ubuguyu.

Kuhusu gharama kwa wagonjwa wanaonunua dawa nje ya hospitali za umma, alisema: “Maduka au hospitali binafsi zitauza dawa kwa bei ya juu zaidi, hasa kwa dawa za kisasa ambazo wagonjwa wanahitaji.”

Kwa kuwa takriban asilimia 60 ya muda wa watu wazima hutumika kazini, wataalamu wa afya wanasisitiza haja ya uwepo wa wataalamu wa afya ya akili katika maeneo ya kazi. Mipango thabiti inahitajika kuwekwa ofisini ili kuimarisha afya ya akili ya wafanyakazi na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ripoti za kimataifa, umuhimu wa kulinda afya ya akili kazini umeongezeka. Mtaalamu wa Saikolojia, Charles Kalungu, anasema changamoto za afya ya akili nchini bado ni kubwa, huku Serikali ikishindwa kutilia mkazo suala hilo.

Alisema akili isipozingatiwa, mafanikio kwa mtu binafsi na shirika yanaweza kuwa finyu, akisisitiza kuwa kuwepo sera ya kusimamia afya ya akili ni muhimu.

Kalungu ametoa wito kwa Serikali kuanzisha vituo vya afya ya akili maofisini, kwa kuwa kuna watu wengi ambao huficha matatizo yao ya akili, wakihofia unyanyapaa.

Alisema wataalamu wa saikolojia wanahitaji kupewa nafasi ili kutekeleza wajibu wao na elimu zaidi ipelekwe vijijini.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ubongo, Edward Kija, alisema huduma za afya ya akili zinapaswa kusogezwa karibu na jamii ili kupunguza unyanyapaa na kurahisisha watu kupata huduma.

Kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk Ahmad Makuwani alisisitiza kuwa sehemu za kazi ni muhimu kwa maisha ya binadamu, hivyo utambuzi na matibabu ya mapema ni muhimu kwa usalama wa afya ya akili.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dk Hamad Nyembea alieleza mikakati ya Serikali kufikisha huduma za afya ya akili hadi ngazi ya halmashauri ifikapo mwaka 2030, ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi.

Kupitia bajeti ya Wizara ya Afya 2024/2025, Serikali ilisema imekamilisha andiko la mapendekezo ya Hati Idhini (Instrument) kwa ajili ya kuipandisha hadhi Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe kuwa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili ili kuimarisha utoaji wa huduma hizo nchini.

Lengo la hatua hiyo ni kuimarisha huduma za kinga, tiba, miundombinu, kuimarisha mfumo wa kitaasisi, kuongeza ubunifu na ufanisi, kukuza taaluma na tafiti zinazohusiana na huduma za afya ya akili, huduma za ubingwa na ubingwa bobezi na kuimarisha Tiba Utalii katika eneo la huduma za afya ya akili.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts