Lebanon. Kiongozi mpya wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon, Naim Qassem amesema yuko tayari kuendeleza mpango wa vita ulioachwa mtangulizi wake aliyeuawa na Israel, Hassan Nasrallah.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa wiki hii, Qassem amesema: “Mpango wangu wa utekelezaji wa vita ni mwendelezo wa kiongozi wetu, Sayyed Nasrallah.”
Aidha, katika taarifa hiyo, Hezbollah imesema Qassem alichaguliwa kushika wadhifa huo kutokana na uaminifu wake kwa kanuni na malengo ya kundi hilo.
Imeongeza kuwa kundi hilo litamwomba Mungu aliongoze katika dhamira hiyo ‘tukufu’ ya kuongoza Hezbollah dhidi ya wapinzani wake.
“Mpango wangu wa utekelezaji wa vita ni mwendelezo wa kiongozi wetu, Sayyed Nasrallah,” amesema Qassem.
Qassem amechaguliwa ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja baada ya kifo cha Nasrallah na kiongozi mwingine wa ngazi ya juu wa Hezbollah, Nabil Kaouk.
Israel ilitangaza imemuua Nasrallah kwa shambulio la anga wakati wakiwa kwenye mkutano wa viongozi wa kundi hilo makao makuu huko Dahiyeh, kusini mwa Beirut.
Taarifa hiyo imrsema kiongozi huyo aliuawa pamoja na kamanda wa kikosi cha kusini cha kundi hilo, Ali Karki na makamanda wengine.
Hata hivyo, kauli ya Qassem inakuja wakati mapigano Kusini mwa Lebanon na Kaskazini mwa Israel yakiendelea kati ya jeshi la Israel, IDF na wapiganaji wa Hezbollah.
Qassem alizaliwa Februari 1953 huko Basta al-Tahta mjini Beirut. Ameoa na ana watoto sita, wavulana wanne na wasichana wawili. Baba yake Muhammad alizaliwa katika mji wa Kfar Fila katika eneo la Iqlim al-Tuffah, kusini mwa Lebanon.
Qassem alisoma hadi ngazi ya juu ya masomo ya kidini, chini ya wanazuoni mashuhuri wa Kishia huko Lebanon. Kando na elimu ya kidini pia alihitimu Shahada ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Lebanon mwaka 1971, kwa mujibu wa BBC.
Pia, alitunukiwa Shahada ya Uzamili ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Lebanon mwaka 1977. Alifanya kazi kama mwalimu kwa madarasa ya sekondari ya umma kwa miaka sita, baada ya kuhitimu katika Chuo cha Ualimu kilichohusishwa na Wizara ya Elimu.
Qassem mwenye (71) amekuwa akijulikana kama kiongozi namba mbili wa Hezbollah akiwa ni mmoja wa wasomi wa kidini walioanzisha kundi hilo mwanzoni mwa miaka ya 1980 na ana historia ndefu katika shughuli za kisiasa za Shia.