Kivumbi Marekani, wagombea wakabana koo uchaguzi ukikaribia

Uchaguzi wa Rais wa Marekani unatarajiwa kufanyika Novemba 5, 2024, Zikiwa zimesalia wiki chache tu, kinyang’anyiro kati ya wagombea wawili wakuu, Kamala Harris wa Chama cha Democratic na Donald Trump wa Chama cha Republican, kimechukua sura mpya, huku tafiti zikionyesha kuwa umaarufu wa Harris umepungua kidogo, jambo linalozua maswali juu ya nani ataibuka mshindi.

Kwa muda mrefu, Harris alionekana kuongoza dhidi ya Trump, lakini tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa pengo kati ya wawili hao limepungua, na ushindani sasa ni mkali zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hali hii imeibua hofu miongoni mwa wanachama wa chama cha Democratic na wapiga kura wake.

Harris alikuwa anaongoza lakini sasa hali imebadililika.

Kwenye uchunguzi wa mwezi uliopita wa ABC News/Ipsos, Harris anaongoza kwa asilimia 50 dhidi ya asilimia 48 za Trump kwa kura za maoni zilizokwishapigwa. Mgombea wa chama cha Democrat alikuwa anaongoza kwa asilimia 52 dhidi ya asilimia 46 kwenye uchunguzi huo huo mwezi uliopita.

Uchunguzi mwingine wa CBS News/YouGov ulionyesha kuwa Harris anaongoza kwa asilimia 51 dhidi ya asilimia 48 miongoni mwa wapiga kura wanaotarajiwa kupiga kura, ikilinganishwa na alipokuwa mbele kwa pointi nne mwezi uliopita.

Matokeo yanayoonyesha kupungua kwa uungwaji mkono yanajitokeza huku kukiwa na wasiwasi miongoni mwa wanachama wa Democrats kwamba Harris anashindwa kuimarisha hali ya kuungwa mkono na Wamarekani wenye asili ya Kihispania na wale wenye asili ya Afrika ambao ni makundi mawili muhimu kwa chama hicho.

Ingawa Harris anaongoza miongoni mwa wanawake wa jamii zote, amekumbana na changamoto ya kuhamasisha ari miongoni mwa wanaume, wakiwamo Wamarekani wenye asili ya Afrika na Wamarekani wenye asili ya Kihispania ambao katika miaka ya karibuni wamekuwa wakimuunga mikono zaidi Trump.

Katika kura za maoni za The New York Times/Siena College zilizotolewa Jumamosi na Jumapili iliyopita, Harris alikuwa anaungwa mkono kwa asilimia 78 ya wapiga kura Weusi na asilimia 56 ya wapiga kura wa asili ya Kihispania – ambayo ni idadi ndogo ikilinganishwa na asilimia zilizopatikana za wagombea wa Democrats kwenye chaguzi za 2020 na 2016.

Alhamisi iliyopita, Rais wa zamani, Barack Obama aliwalaumu wanaume weusi kwa kutokuwa na ari kubwa ya kumuunga mkono Harris kama walivyokuwa na shauku wakati wa kampeni zake za 2008 na 2012.

“Mnatengeneza sababu na visingizio vya kila aina, na nina tatizo na hilo,” Obama alisema katika mkutano wa kampeni huko Pittsburgh, Pennsylvania, moja ya majimbo saba muhimu yanayotarajiwa kuamua matokeo ya uchaguzi.

“Kwa sababu sehemu ya hili inanifanya nifikirie – na ninazungumza moja kwa moja na wanaume – sehemu ya hili inanifanya nifikirie kwamba, huenda hampendi wazo la kuwa na mwanamke kama Rais, na mnatafuta mbadala na sababu nyingine kwa hilo.”

Harris na Trump Jumapili waliendelea kuelekeza kampeni zao kwenye majimbo yenye ushindani mkali, wakifanya mikutano huko North Carolina na Arizona.

Kwenye mkutano wa kampeni huko Greenville, North Carolina, Harris alimshutumu Trump kwa kueneza taarifa za uongo kuhusu mwitikio wa serikali kuhusu vimbunga vya karibuni.

“Tatizo la hili ni kwamba inafanya kuwa vigumu zaidi kwa watu kupata taarifa zinazoweza kuokoa maisha ikiwa wanaaminishwa kuwa hawawezi kuamini,” alisema Harris.

Trump, kwa upande mwingine, alitumia mkutano wa kampeni huko Prescott Valley, Arizona kuhamasisha ajira ya maofisa 10,000 wa ziada wa ulinzi mpakani (Border Patrol).

“Baada ya kushinda urais, nitaomba Congress iidhinishe mara moja ongezeko la asilimia 10 la mishahara, hawajapata ongezeko kwa muda mrefu.”

Uchaguzi wa 2024: Je, Harris atashinda?

Uchaguzi wa Rais wa Marekani wa mwaka 2024 unatajwa kuwa uchaguzi wa 60 tangu kuanzishwa kwa taifa hilo mwaka 1789. Katika historia ya Marekani, kila uchaguzi umekuwa na umuhimu mkubwa, ukionyesha mabadiliko ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi. Uchaguzi wa mwaka huu unakuja wakati wa changamoto nyingi zinazowakabili Wamarekani, zikiwemo masuala ya uchumi, usalama, na mabadiliko ya hali ya hewa.

Suala la kama Kamala Harris ana nafasi ya kumshinda Donald Trump linategemea mambo mengi, yakiwemo uungwaji mkono wa wapiga kura wa makundi muhimu kama Wamarekani wenye asili ya Afrika na wale wa asili ya Kihispania. Hali ya kisiasa na uchumi nayo ina nafasi kubwa ya kuathiri maamuzi ya wapiga kura.

Kwa sasa, tafiti za maoni zinaonyesha kuwa ushindani kati ya wagombea hawa wawili ni mkali, huku Harris akiwa mbele kwa tofauti ndogo dhidi ya Trump. Lakini, kama inavyofahamika, uchaguzi wa Marekani hauamuliwi kwa kura za moja kwa moja, bali kwa mfumo wa wajumbe maalum (Electoral College), ambapo wagombea wanahitaji kupata kura 270 za wajumbe maalum ili kushinda urais.

Hali ilivyokuwa miezi iliyopita

Miezi kadhaa kabla ya uamuzi wa Biden kujiondoa kwenye kinyang’anyiro, kura za maoni mara kwa mara zilionyesha akiwa nyuma ya Rais wa zamani Trump. Ingawa wakati huo ilikuwa kama kiashiria, kura nyingi za maoni zilipendekeza Harris hangefanya vyema.

Lakini kinyang’anyiro hicho kiliimarika baada ya Harris kuibuka kidedea kwenye kampeni na kupata uongozi mdogo dhidi ya mpinzani wake katika wastani wa kura za maoni za kitaifa ambazo amedumisha tangu wakati huo. Wastani wa hivi punde wa kitaifa wa kura za wagombea hao wawili umeonyeshwa katika jedwali zifuatazo.

Katika chati hizi za ufuatiliaji wa kura hapa chini, mwelekeo unaonyesha jinsi wastani huo umebadilika tangu Harris aingie kwenye kinyang’anyiro na nukta zinaonyesha kuenea kwa matokeo ya kura binafsi.

Harris alifikia 47% wakati wa kongamano la siku nne la chama chake huko Chicago, ambalo lilimalizika Agosti 22 kwa hotuba ya kuahidi “mwanzo mpya wa kusonga mbele” kwa Wamarekani wote. uungwaji mkono wake umesonga kidogo tu tangu wakati huo.

Wastani wa uungwaji mkono wa Trump pia umesalia kuwa thabiti, ukizunguka karibu 44%, na hakukuwa na ongezeko kubwa licha ya kuidhinishwa na Robert F Kennedy, ambaye alijiondoa kama mgombea huru mnamo Agosti 23.

Ingawa kura hizi za maoni za kitaifa ni mwongozo muhimu wa jinsi mgombeaji anavyojulikana kote nchini kwa ujumla, si lazima kuwa njia sahihi ya kutabiri matokeo ya uchaguzi.

Hii ni kwa sababu Marekani hutumia mfumo wa wajumbe maalum kumchagua rais wake, hivyo kushinda kura nyingi zaidi kunaweza kuwa na umuhimu mdogo kuliko pale watakaposhinda. Kuna majimbo 50 nchini Marekani lakini kwa sababu wengi wao karibu kila mara hupigia kura chama kimoja, kwa kweli kuna majimbo machache ambapo wagombea wote wana nafasi ya kushinda. Haya ndiyo maeneo ambayo uchaguzi utashinda na kushindwa na yanajulikana kama majimbo yenye ushindani mkali.

Majimbo Yenye Ushindani Mkali

Katika uchaguzi wa Marekani, majimbo yanayojulikana kama “swing states” au majimbo yenye ushindani mkali yana nafasi kubwa ya kuamua mshindi wa uchaguzi. Kwa sasa, Pennsylvania, Michigan, Wisconsin, Arizona, Georgia, North Carolina, na Florida ni miongoni mwa majimbo ambayo wagombea hawa wawili wanapigania kwa nguvu zote.

Kwa sasa, kura za maoni zinaonyesha ushindani mkali katika majimbo saba, ambayo inafanya kuwa vigumu kujua ni nani hasa anaongoza kinyang’anyiro hicho. Kuna kura chache za kura za majimbo kuliko kura za kitaifa kwa hivyo tuna data ndogo na kila kura ina nakisi ambayo inamaanisha kuwa nambari zinaweza kuwa juu au chini.

Kama ilivyo, kura za maoni za hivi majuzi zinaonyesha kuwa wagombea hao wawili wamepishana kwa chini ya asilimia moja katika baadhi ya majimbo. Hiyo inajumuisha Pennsylvania, ambayo ni muhimu kwa kuwa ina idadi kubwa zaidi ya kura za wajumbe maalum ambao humuwezesha mshindi kufikia kura 270 zinazohitajika.

Majimbo ya Pennsylvania, Michigan na Wisconsin ambazo zimekuwa ngome za chama cha Democratic kabla ya Trump kuzigeuza kuwa nyekundu kwenye harakati zake za kushinda uchaguzi wa urais 2016. Biden aliyachukuwa tena mwaka wa 2020 na ikiwa Harris anaweza kufanya vivyo hivyo mwaka huu basi atakuwa na nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi.

Related Posts