Kona ya Maloto: Polisi wanavyotengeneza mashujaa wa upinzani

Boniface Jacob, Meya wa zamani wa Ubungo na Kinondoni, Dar es Salaam, alikamatwa Septemba 18, 2024, akiwa mwanachama wa kawaida wa Chadema, aliachiwa kwa dhamana Oktoba 7, 2024, akiwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani.

Boniface, maarufu Boni Yai, wakati anakamatwa, alikuwa kwenye mchakato wa kugombea uenyekiti wa Kanda ya Pwani. Alikuwa ameshajaza fomu na kuzirudisha. Hakufanya kampeni. Siku 19 alizokaa mahabusu, zilimjengea sifa ya ushujaa wa kisiasa.

Kisiasa, kiharakati na kihistoria, kitendo cha Boni kushikiliwa mahabusu, kilikuwa na manufaa makubwa kwake kuelekea uchaguzi Kanda ya Pwani, kuliko angekuwa uraiani. Ufafanuzi upo ndani ya kitabu “Dance in Chains: Political Imprisonment in the Modern World” – “Dansi kwenye Minyororo; Kifungo cha Kisiasa katika Ulimwengu wa Kisasa.”

Kitabu kimeandikwa na mwandishi wa Marekani, Padraic Kenney, baada ya utafiti mkubwa. Majibu ni kuwa watu siku zote katika harakati za upinzani, hujenga mshikamano na kuwatukuza makomredi wao wanaokuwa vifungoni jela au mahabusu. Huwaona ni alama ya mapambano dhidi ya ukandamizaji na utetezi wa haki za binadamu.

Hili ndilo limetokea kwa Boni, lilimjenga Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, kwa kiasi kikubwa. Limeendelea kumfanya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuwa alama kuu ya mageuzi. Kila mwanasiasa wa upinzani anapokamatwa, umaarufu huongezeka. Polisi wanajua, dunia inafahamu.

Boni alipokamatwa, ghafla habari kuu ya kisiasa ikalizunguka jina lake. Ndivyo ilivyokuwa kila Lema alipokamatwa, au Mbowe anapowekwa mahabusu. Haihitaji utafiti kutambua kuwa Makamu Mwenyekiti Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, aligeuka nembo ya ulimwengu ya mapambano ya demokrasia kutoka Tanzania, Afrika, mara alipopigwa risasi.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi “Sugu”, alipopigwa na polisi na kuumizwa, kisha kulazwa hospitali, Balozi wa Marekani Tanzania, Michael Battle na mabalozi wengine, walimtembelea kumjulia hali. Ujumbe ukafika mbali. Mitandao ilitikiswa na habari ya Sugu kuumizwa.

Mwandishi Padraic Kenney, ametolea mfano mkubwa kuhusu Rais wa kwanza wa Afrika Kusini ya kidemokrasia, Nelson Mandela. Kabla hajakamatwa na kufungwa jela, jina la Mandela halikuwa kitovu cha mapambano dhidi ya mfumo kandamizi wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

Mandela hakuwa nembo ya uongozi, isipokuwa mwasi, aliyeanzisha kikosi cha uMkhonto we Sizwe (Mkuki wa Taifa), ambacho kilikuwa idara ya kijeshi ya chama cha ANC (African National Congress). Askari wa serikali ya kikaburu, walivamia shamba la Liliesleaf, Rivonia, kwa sababu palikuwa makao makuu ya uMkhonto we Sizwe (MK), vilevile maficho ya makamanda wa MK.

Wakati wa uvamizi Rivonia, Mandela alikuwa jela, alikohukumiwa kifungo cha miaka mitano Agosti 5, 1962, kwa kosa la kuhamasisha mgomo wa wafanyakazi. Hata hivyo, nyaraka zilizokutwa kwenye shamba la Liliesleaf, zilithibitisha kuwa Mandela siyo tu alikuwa mwanzilishi wa MK, bali pia mbeba maono ya uasi mkubwa dhidi ya serikali ya kikaburu.

Ndipo, Mandela aliunganishwa na makamanda 13 wa MK, wakasomewa mashitaka manne ambayo unaweza kuyaweka kwenye makundi mawili; ugaidi na kushirikiana majeshi ya kigeni dhidi ya serikali. Hukumu iliyokuwa inasubiriwa kwao ni kifo. Hotuba ya Mandela “I Am Prepared to Die” – “Nimejiandaa Kufa”, aliyotoa mahakamani Aprili 20, 1964, ilibadili upepo wote.

Ilidhaniwa Mandela angeonesha unyenyekevu mahakamani, kwa kuomba huruma, kwamba ana mke na watoto au mama mzazi mzee. Haikuwa hivyo. Mandela alitoa utetezi mahakamani kwa saa nne. Akajenga utetezi wa kile alichokuwa anakisimamia kuwa na jamii yenye usawa na inayoishi pamoja kwa maelewano bila ubaguzi wa Weupe na Weusi. Akasema katika hilo, alikuwa tayari kufa.

Baada ya utetezi huo, kila kitu kuhusu mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, kilielekezwa kumzunguka Mandela. Umaarufu wa Mandela ulimfunika hadi Mwenyekiti wa ANC, Albert Luthuli. Maneno “Free Mandela”, yalikuwa kauli mbiu kuu ya mapambano. Nguvu ya Mandela ilisababisha achaguliwe kuwa Naibu Rais wa ANC mwaka 1985 akiwa jela.

Hali hiyo pia ipo Cuba. Shujaa wa wakati wote wa Taifa la Cuba, Fidel Castro, alipaa viwango vya kisiasa, alipotoa hotuba mahakamani ya dakika 240, Oktoba 16, 1953, iliyobeba kichwa; Historia Itaniweka Huru (The History Will Absolve Me).

Wakati Castro anatoa hotuba hiyo alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 27. Aliyekuwa na moyo mkubwa wenye upendo kwa nchi yake. Aliyemwona na kumtamka aliyekuwa Rais wa Cuba wakati huo, Fulgencio Batista kuwa ni msaliti na kibaraka wa Marekani.

Castro alitoa hotuba hiyo akiwa jela baada ya kukutwa na hatia ya kuongoza vijana wenzake 137 kulipua kambi namba mbili kwa ukubwa Cuba, Moncada Barracks. Ni shambulizi hilo lililoanzisha vuguvugu la mapinduzi ya kumng’oa Batista, kilele chake kikiwa Januari 3, 1959.

Alipokamatwa, alipotakiwa kutoa utetezi mahakamani, alishusha maneno makali ambayo ndiyo yameitwa hotuba “Historia Itaniweka Huru”. Baada ya hotuba hiyo, nguvu ya kisiasa ya Castro haikumithilika.

Kutoka ushindi wa Boni Yai kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, au aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, marehemu Chacha Wangwe, aliposhinda udiwani Tarime, Mara akiwa gerezani. Ushindi wa Mandela kuwa Naibu Rais wa ANC akiwa jela. Jumlisha mifano mingine.

Jambo moja ni sahihi kabisa, polisi Tanzania wamekuwa wakijenga haiba za kisiasa za viongozi wa upinzani bila kujua. Wanapowakamata, wanapowafungulia mashitaka, wanapowaweka mahabusu na kupambana wasipate dhamana, wanapowapiga na kuingia kwenye mapambano mahakamani, ndivyo huwajenga kisiasa na kuzidi kuwafanya wawe wakubwa.

Related Posts