Maajabu aliyeasisi jina la Kwa Bi Nyau

Alisifika kwa kufuga paka wengi kiasi cha kubatizwa jina la Bibi Nyau. Na haikuishia hapo, hata eneo alilokuwa akiishi watu wakaishia kulipachika jina la Kwa Bibi Nyau.

Hata hivyo, wasichojua watu wengi ni kuwa Bibi Nyau hakuwa mpenzi wa paka pekee, alikuwa na ngedere kadhaa, akiwamo yule aliyekuwa maarufu kwa jina la John.

Kwa sasa eneo la Kwa Bibi Nyau ni moja kati ya maeneo maarufu katika Jiji la Dar es Salaam.

Eneo hilo lipo pembezoni mwa barabara ya Tandale, eneo la Magomeni Makanya katika Wilaya ya Kinondoni.

Umaarufu wake unatokana na bibi huyo anayeelezwa kuwa mwenyeji wa hapo kusifika kuwa na paka wengi ambao alikuwa akiwahudumia na kuishi nao.

Akisimulia kuhusu chimbuko la eneo hilo kuitwa kwa ‘Bibi Nyau,’ Mfaume Alawi, ambaye ni mzaliwa wa eneo hilo, amesema kuwa katika kipindi cha miaka ya 1990 hadi 2000 katika moja ya nyumba iliyopo pembezoni mwa barabara katika eneo hilo kulikuwa na bibi aliyekuwa na mifugo mingi.

Alawi amesema bibi huyo ambaye awali alijulikana sana kwa jina la Bibi Kaima alikuwa akifuga paka, ngedere pamoja na kuku. Anaeleza kuwa bibi huyo hakubahatika kujaaliwa kupata mtoto katika maisha yake.

Amesema pamoja na ufugaji, pia Bi Kaima alikuwa mjasiriamali aliyejishughulisha na biashara mbambali, ikiwemo uuzaji wa mkaa pamoja na sambusa za viazi ambazo alikuwa akizifanya pembezoni mwa nyumba yake.

Chimbuko la Kwa Bibi Nyau

Alawi amesema katika mifugo iliyokuwa ikimilikiwa na bibi huyo, paka ndio waliongoza kwa kuwa wengi zaidi.

Amesema kwa makadirio paka hao waliweza kufika 50-60 na kila mmoja alikuwa akimtambua na kumtaja kwa jina lake.

“Baadhi ya majina aliyowapa paka wake ambayo nayakumbuka ni pamoja na Mwajuma, Salum pamoja na ngedere wake mmoja aliyempa jina la John,” amesema na kuongeza:

“Alikuwa akiwahudumia yeye mwenyewe na kuhakikisha wanapata huduma zote muhimu, ikiwemo chakula na maji.’’

Anaeleza kuwa kilichokuwa kinawashangaza wengi ni kitendo cha kutenga chakula na kula pamoja na paka hao.

“Alipendelea sana kutandika mkeka nje ya nyumba yake na kula chakula pamoja na paka wake, jambo ambalo liliwashangaza na kuwavutia watu wengi, wakiwemo waliokuwa wakipita katika barabara hiyo, hasa wale wa kwenye vyombo vya usafiri,” anasema.

Pia amesema pamoja na kuwa alikuwa akisifika kwa ucheshi, bibi huyo ambaye sasa ni marehemu, aligeuka mbogo pale mtu anapoonyesha viashiria vya kutaka kumdhuru paka au ngedere wake.

“Ukitaka kuujua upande wa pili wa Bibi Kaima chokoza ngedere au paka wake, alikuwa hataki masihara, aliwathamini sana,” anaeleza Alawi.

Anasema jambo hilo lilifanya baadhi ya watu, hasa makondakta wa daladala wanapopita katika eneo hilo kumtania kwa kumuita ‘Bibi Nyau’.

“Makondakta wa daladala wakimuona wakati wanapita walikuwa wakimtania kwa kumuita Bi Nyau, utani huo uliendelea kukua, baadaye hata abiria waliokuwa wakishuka hapo walielekeza kushushwa kwa Bibi Nyau,” ameeleza.

Anasema wengine walienda mbali na kuhusisha uwezo wake wa kukaa na kuelewana na wanyama na imani za kishirikina, jambo ambalo hata hivyo halikuwa na ushahidi wowote.

Anasema utani huo uliendelea kukua hadi kufanya eneo hilo alilokuwa akiishi kutambulika kama Kwa Bibi Nyau na hata baada ya kufariki katikati ya miaka ya 2000, ameacha jina lake hilo la utani kama urithi wa kukumbukwa kwa vizazi vijavyo.

Mzawa mwingine wa eneo hilo, Juma Yusuph anasema pamoja na paka, pia alikuwa na ngedere wake aliyempa jina la John. Anasema ngedere huyu alitikisa na kujizolea umaarufu katika eneo hilo.

Yusuph anasema ngedere huyo alipata umaarufu kutokana na kuwa mkubwa na alikuwa akimsaidia kumsogezea karibu vitu vyake vidogo vidogo alivyovihitaji.

Hata hivyo, Yusuph anasema baada ya bibi huyo kuanza kuugua alishindwa kuihudumia mifugo yake vizuri kama alivyokuwa akifanya awali.

Hivyo ilifanya ngedere huyo kuanza tabia ya wizi na udokozi katika nyumba, maduka na migahawa iliyopo jirani na eneo hilo.

“Tabia hiyo iliwachukiza wengi, hata hivyo baadaye ngedere huyo alionekana katika mazingira hayo akiwa amekufa,” anasema.

Kilichotokea kwa wanyama wake

Yusuph anasema baada ya bibi huyo kufariki dunia katika ya miaka ya 2000, wanyama hao, wakiwemo paka na ngedere, walianza kutoweka mmoja hadi mwingine.

Kiasili Bi Kaima aka Bi Nyau ni Mmanyema kwa upande wa ubabani na Mzaramo upande wa mama. Siyo ufugaji pekee, bibi huyu alisifika kwa tabia yake ya ucheshi ambayo nayo inaweza kuwa karata iliyomuongezea sifa na umaarufu kiasi cha kuacha historia.

Kijamii unaweza kusema alikuwa mtu wa watu, au kwa msemo wa kileo “hakuwa na baya”. Hilo lilijidhihirisha kwa watu wengi kujitokeza katika maziko yake yaliyofanyika katika makaburi ya Ndugumbi, eneo si mbali na alipokuwa akiishi.

Hata nyumba aliyokuwa akiishi, kulikuwa na wapangaji wanaosadikiwa kuwa wawili, ambao hawakuona tabu ya kuishi na bibi huyo ambaye wakati wa mchana baada ya mlo usingekosa kumuona akiwa kajipumzisha juu ya jamvi lake chini ya mti. Sio yeye tu, hata paka wake nao walimuunga mkono kupata mapumziko ya mchana. Na kwa nini wasifanye hivyo ilhali walikuwa sehemu ya familia yake, unaweza kuwaita wanawe!

Unaweza kujiuliza kulikoni binadamu kuishi na wanyama. Hilo liliwezekana kwa Bi Kaima ambaye pengine aliamua kutafuta faraja kupitia wanyama hao kwa ile hali yake ya kutokuwa na familia.

Inaelezwa kuwa paka waliomzunguka siyo wote walikuwa wake, wengine walilazimika kutoka viunga vya karibu na kuja kuungana na paka wa Bi Kaima, pengine walivutiwa na ukarimu wake, ukiwamo wa kula pamoja na wanyama hao.

Ukimuondoa ngedere John na mikasa yake, familia ya Bi Kaima isingetimia kama hujamtaja aliyekuwa paka wake maarufu kwa jina la Salim na dada yake Mwajuma.

Kwa sasa mahali ilipokuwa nyuma ya Bibi Nyau, pamebadilika. Ule mkeka na wanyama hawaonekani tena. Nyumba hiyo kwa sasa inatumika kuonyeshea michezo kwenye runinga.

Wenyeji na hata makondakta hawana tena mtu wa kucheka naye. Japo hayupo tena kimwili, kumbukumbu ya maisha yake itabaki katika fikra za wenyeji wengi wa eneo hilo.

Hakuacha mrithi kwa maana ya mtoto, lakini Bi Kaima ameacha urithi wa eneo litakalobaki historia kwa watu wengi.

Related Posts