Mahakama yaamuru ‘Boni Yai’ kutoa nywila, akimbilia Mahakama Kuu

Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Manispaa ya Kinondoni na Ubungo, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amekimbilia Mahakama Kuu kupinga amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, inayomtaka kulipatia Jeshi la Polisi Kinondoni nywila za simu zake.

Jacob, maarufu kama Boni Yai, katika kesi hiyo, anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao ya kijamii, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Kufuatia kesi hiyo, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RCO), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) David Msangi aliwasilisha maombi mahakamani hapo akiomba amri dhidi ya mshtakiwa Boni Yai kutoa nywila za simu zake mbili za mkononi kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.

Maombi hayo yalisikilizwa na kuamuriwa upande mmoja na Mahakama ilitoa amri kwa Boni Yai kufika ofisi ya RCO na kutoa nywila kufungua simu zake mbili za mkononi Samsung Galaxy S20 Ultra SG na Samsung Galaxy S23 Ultra.

Hata hivyo, Boni Yai kupitia Wakili wake Hekima Mwasipu amefungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama Kuu dhidi ya amri hiyo ya Mahakama ya Kisutu, chini ya hati ya dharura.

Kwa mujibu ya hati hiyo ya dharura wakili Mwasipu amesema kwa maoni yake uamuzi wa shauri hilo la mapitio unahitaji uharaka mkubwa.

Amasema mwombaji, Boni Yai ameamuriwa kuripoti kwa RCO kufungua simu zake kwa amri ya mahakama iliyotolewa upande mmoja na Mahakama ya Kisutu bila kumpa haki ya kusikilizwa.

Pia anadai kesi ya jinai namba 26918 iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu si halali kwa kuwa imefunguliwa bila kukamilisha upelelezi kama inavyotakiwa na sheria.

Vilevile anadai kuwa mwombaji, Boni Yai amekuwa akihudhuria katika Mahakama ya Kisutu, kitendo ambacho kimsingi kinampunguzia muda wa kufanya kazi kutokana na mashtaka yaliyoko mahakamani hapo isivyo halali.

Kwa mujibu wa hati ya maombi ya faragha ya shauri hilo, Boni Yai  anaiomba Mahakama Kuu iitishe kwa ajili ya kukagua, kurejea na kufuta hati ya mashtaka ya Septemba 19, 2024 katika kesi hiyo ya jinai namba 26918 baina ya Jamhuri dhidi yake.

Pia anaiomba Mahakama Kuu itengue amri ya Mahakama ya Kisutu iliyotolewa upande mmoja katika shauri la maombi mchanganyiko ya jinai namba 29695/2024 iliyomwamuru kufungua simu zake hizo za mkononi.

Vilevile anaiomba Mahakama Kuu kumzuia RCO Kinondoni au wakala anayefanya kazi chini ya maelekezo yake kutokutekeleza amri hiyo ya Mahakama ya Kisutu inayomtaka kufungua nywila za simu zake hizo, ambayo anadai kuwa si halali na alipwe gharama za shauri hilo.

Boni Yai anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Katika shtaka la kwanza inadaiwa kuwa, Septemba 12 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mafwele.

Taarifa hizo zinasomeka kuwa: “Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa moja katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey”.

Katika shtaka la pili hatui ya mashtaka inaeleza kuwa Boni Yai alitenda kosa hilo Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam akidaiwa kuchapisha taarifa za uwongo zinazowahusisha wakuu wa upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.

Ujumbe huo inasomeka kuwa:

“Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu … bali Ma-RCO waliokuwa kuteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi.

Related Posts