Mahakama yatupilia mbali kesi ya Saqware

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali kesi ya madai ya Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (Tira), Baghayo Saqware dhidi ya Hospitali ya Salaaman na Mkurugenzi wake, Dk Abdi Hirsi, baada ya kujiridhisha ameshindwa kuthibitisha madai yake.

Katika kesi hiyo ya madai namba 167/2021 Saqware alikuwa akiiomba Mahakama hiyo iwaamuru wadaiwa wamlipe Sh78 milioni,  kwa madai kuwa  walivunja mkataba wa huduma ya ushauri wa kitaalamu aliyoitoa katika hospitali hiyo.

Pia aliomba amri ya kulipwa gharama ya hasara mapato, fidia ya jumla, riba na nyinginezo ambazo Mahakama itaona zinafaa kuzitoa.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi, aliyesikiliza kesi hiyo katika hukumu yake aliyoisoma jana Alhamisi, Oktoba 31, 2024 alitupilia mbali kesi hiyo baada ya kuridhika kuwa mdai huyo hakuweza kuthibitisha madai yake.

Katika hukumu hiyo aliyoisoma kwa ufupi, Hakimu Mushi alisema alijielekeza katika hoja mbili tu zilizotokana na ushahidi wa pande zote ambazo ni kama wadaiwa walivunja mkataba na nafuu ambazo wadaiwa wanastahili.

Sakware katika ushahidi wake alidai Aprili 11, 2020 akiwa mtaalamu wa masuala ya bima na utawala alisaini mkataba na wadaiwa wa kutoa ushauri kwa makubaliano ya kulipwa Sh6 milioni kwa mwezi, au asilimia 40 ya mapato baada ya makato yote.

Alidai hata hivyo hakulipwa kama walivyokubaliana, hivyo Juni 7, 2021 aliandika barua kudai malipo ambayo hayakufanyika, hivyo akaamua kufungua kesi.

“Nilifanya kazi ya mshauri elekezi kupitia simu, semina, vikao na kuwashauri kwa namna iliyokuwa inafaa lakini walienda tofauti na mkataba unavyosema hawakuwahi kunilipa kwa miezi 13,” alidai Saqware katika ushahidi wake.

Hakimu Mushi katika hukumu yake amekubaliana na utetezi wa wadaiwa kuwa mdai hakuweza kuthibitisha kama alifanya kazi kwa muda wa miezi 13 na kwamba hakulipwa chochote.

Hakimu Mushi alidai mdaiwa hakuweza kumuita mfanyakazi yeyote kutoka katika hospitali hiyo, aliyepo kazini au hata ambaye alishaacha kazi kuthibitisha madai yake kwamba aliwahi kufanya kazi hiyo ya ushauri hospitalini hapo kama alivyodai.

Pia alisema mdai, Saqware hakuwasilisha nyaraka yoyote kuthibitisha hizo semina alizodai alikuwa akizitoa kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo, katika kutekeleza jukumu lake la kimkataba la kutoa ushauri wa kitaalamu.

Ingawa wadaiwa katika ushahidi wao walikiri kuingia mkataba huo na Saqware na kwamba waliuvunja baada ya yeye kwenda kinyume na makubaliano, lakini Hakimu Mushi katika hukumu hiyo alisema mkataba huo haukuvunjwa.

“Pamoja na kwamba wadaiwa wanadai waliuvunja mkataba lakini Mahakama hii inaona mkataba huo haukuvunjwa kwa sababu hakuna majukumu ya kimkataba aliyofanya kwa miezi hiyo 13,” alisema Hakimu Mushi na kufafanua:

“Kwa hiyo ili uvunje mkataba lazima uwe umetimiza majukumu. Kwa hiyo swali la kwanza Mahakama inaona wadaiwa hawakuvunja mkataba, hivyo mdai asingeweza kulipwa.”

Katika hoja au swali la pili yaani nafuu aliyostahili, Hakimu Mushi alisema kwa kuwa hakuna alichofanya mdai, hakuna anachoweza kulipwa.

“Hivyo mdai ameshindwa kuthibitisha madai yake na shauri hili kinatupiliwa mbali kwa gharama”, alihitimisha huku yake hiyo Hakimu Mushi akimaanisha kuwa mdai Saqware anapaswa kuwalipa wadaiwa gharama za kuendesha kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, Saqware aliwakilishwa na wakili, Mliyambelele Ng’weli huku wadaiwa wakiwakilishwa na Wakili Juma Nassoro.

Kwa upande wake, Saqware alikuwa na mashahidi wawili yeye mwenyewe na msambaza nyaraka wa Mahakama ambaye aliwapelekea wadaiwa notisi ya kusudio la kuwafungulia kesi hiyo ya madai.

Upande wa wadaiwa ulikuwa na mashahidi wanne akiwemo mdaiwa wa pili, Dk Hirsi ambaye ndiye aliyezungumzia mkataba baina yao na mdai.

Dk Hirsi katika ushahidi wake alidai walifahamiana na Saqware mwaka 2019, wakati huo akifanya kazi Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (Tira), baada ya kuwa na mgogoro wa malipo kuhusu bima ambao Saqware aliusuluhisha.

Alidai waliingia mkataba na Saqware mwaka 2020 baada ya kutoka Tira kwa ajili ya kufanya kazi katika hospitali hiyo.

Dk Hirsi alidai alikuwa anafanya kazi kila siku kwa nafasi ya meneja, kwa niaba ya mkurugenzi, lakini mkataba uliandikwa kuwa anafanya kazi kama mashauri kwa kuwa alidai alikuwa anatarajia kurudi Tira.

Pia Dk Hirsi alidai kabla ya kuanza kazi rasmi Julai Mosi, 2020 Saqware alitakiwa afanye kazi kwa kipindi cha miezi miwili ya matazamio.

Hata hivyo alidai mkataba wake ulisitishwa Aprili 30, 2020 kutokana na makosa yaliyoisababishia hospitali hiyo hasara.

Related Posts