Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, mwaka huu, wanapaswa kutambua kuwa yapo makosa yakifanyika yanaweza kusababisha mtu kushtakiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo, mtu yeyote atakuwa ametenda kosa la uchaguzi endapo ataharibu orodha ya wapigakura au nyaraka zozote zinazohusiana na uchaguzi.
Makosa mengine ni iwapo atatoa taarifa za uongo, ili apige kura au kugombea nafasi ya uongozi ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa, akijiandikisha zaidi ya mara moja kwenye orodha ya wapigakura, na akipiga kura zaidi ya mara moja kwa wagombea wa nafasi moja.
Makosa mengine ni iwapo atatishia wapigakura au wagombea, ili kuvuruga uchaguzi, akifanya kampeni siku ya uchaguzi, akionyesha ishara au kuvaa mavazi yanayoashiria kumtambulisha mgombea au chama cha siasa katika eneo la mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura.
Mengine ni iwapo mtu atamzuia msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, msimamizi wa kituo, mjumbe wa kamati ya rufani au mtumishi wa umma aliyeteuliwa kusimamia uchaguzi kutekeleza majukumu yake.
Pia iwapo atakiuka masharti ya kiapo chake chini ya kanuni, akipatikana na karatasi za kupigia kura zaidi ya moja kwa nafasi moja inayogombewa, akivuruga ratiba ya mikutano ya kampeni za uchaguzi au akivunja masharti ya kampeni za uchaguzi, akifanya jambo lolote kinyume cha kanuni za uchaguzi.
Mengine ni iwapo atakutwa na silaha kinyume cha sheria kwenye eneo la uteuzi wa wagombea, mikutano ya kampeni, eneo la usikilizaji wa rufaa, kituo cha kuandikisha wapigakura au kituo cha kupigia na kuhesabu kura, au atatangaza matokeo ya uchaguzi kabla hayajatangazwa na msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi au msimamizi wa kituo kwa mujibu wa kanuni.
Kwa mujibu wa kanuni, mtu yeyote atakayepatikana na hatia kwa kosa lolote atahukumiwa adhabu ya faini isiyozidi Sh300,000 au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja (faini na kifungo).
Kanuni zinaeleza mtu yeyote atakayetumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayoashiria unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika uchaguzi atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia ataadhibiwa kwa mujibu wa taratibu za maadili.
Ofisa Habari wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa anasema wananchi wanapaswa kutambua kanuni hizo ambazo hazionyeshi kupendelea upande wowote.
“Wananchi wanatakiwa kuheshimu hilo kwa sababu kupiga kura zaidi ya mara moja kwa mgombea wa nafasi moja ni kosa la jinai, unaposisitiza demokrasia ichukue mkondo wake ni lazima kuheshimu taratibu za uchaguzi,” anasema.
Anasema mhusika awe wa upinzani au wa chama tawala, anatakiwa kuheshimu uchaguzi wa haki kwa kupiga kura mara moja katika nafasi moja.
“Shughuli hiyo inapaswa kuanza katika hatua ya kujiandikisha, unatakiwa kujiandikisha mara moja na jinai yoyote, Serikali ichukue mkondo wa sheria. Watanzania tuheshimu taratibu hizo,” anasema.
Anasema dhamira ovu ni moja ya sababu zinazowafanya watu kujikuta katika makosa hayo.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe anasema kuwa kanuni ni jambo muhimu na kila utaratibu unaofanyika unapaswa kuzizingatia.
“Anayevunja kanuni na ikathibitika, afikishwe kwenye vyombo vya dola. Pia kanuni zinapaswa kuwa wazi, si mtu kuziweka mfukoni halafu anarukia watu. Zinapaswa ziwe wazi watu waelewe kwa sababu wanafanya uchaguzi nchini kwao,” anasema.
Rungwe anasema kanuni zinapaswa kufuatwa na vyama vyote si kwa vile vya upinzani pekee, ili kudumisha ustawi wa demokrasia.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu anasema kutunga kanuni zenye viashiria vya kijinai katika uchaguzi ni kutisha watu, kwani ilitakiwa ubaki mfumo wa faini pekee.
Anasema kwa kuwa kanuni zilishapitishwa, lazima zifuatwe katika uchaguzi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga anasema kuvunja kanuni ni kosa na kuna adhabu zake.
“Uchaguzi una taratibu zake zilizowekwa na tume na miongozo mingine, wito wangu shughuli ya uchaguzi haihusiani na vyama pekee, bali zinahusu maisha ya watu, ni muhimu kujali taratibu zilizopo,” anasema.
Bananga anasema viongozi wa vyama vya siasa na asasi nyingine za kiraia zinapotoa elimu kwa umma zinapaswa kutii sheria, ili kupata uchaguzi ulio huru na salama.
“Tunataka watu wapate uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa, siku ya uchaguzi ni hatari kufanya siasa, kwa kuwa kuna kipindi maalumu, kikiisha watu waheshimu,” anasema.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.