Mashirika ya kiutu yaonya juu ya kitisho cha njaa duniani – DW – 01.11.2024

  
Mashirika ya chakula ya Umoja wa Mataifa yameonya juu ya kitisho cha njaa kali zaidi katika maeneo 16 duniani ambayo yapo kwenye mizozo katika miezi ijayo. Maeneo hayo yanayotajwa kwenye ripoti hiyo ni pamoja na Palestina, Sudan, Sudan Kusini, Mali na Haiti. 

Migogoro ndiyo chanzo kikubwa cha ukosefu mkubwa wa chakula katika maeneo hayo yote yaliyoripotiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na Chakula na Kilimo na Mpango wa Chakula Duniani.

Hali mbaya ya hewa ni sababu kuu pia katika maeneo mengine huku ukosefu wa usawa wa kiuchumi na madeni makubwa katika nchi nyingi zinazoendelea yakiathiri uwezo wa serikali wa kuchukua hatua, Hayo ni kulingana na ripoti ya pamoja inayoangazia utabiri wa hali kuanzia Novemba 2024 hadi Mei 2025.

Soma zaidi. UN: Watu bilioni 1.1 wakabiliwa na umaskini

Hatua za kibinadamu zinahitajika haraka kuzuia njaa na vifo katika maeneo ya Palestina, Sudan, Sudan Kusini, Haiti na Mali, ilisema ripoti hiyo, kulingana na utafiti wa wataalamu kutoka mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu mjini Roma.

Njaa
Mataifa ya Sudan, Mali na Haiti yameorodheshwa kuwa katika hali mbaya zaidi ya njaa katika siku zijazoPicha: Mohamed Odowa/picture alliance/dpa

Huyu ni Maxwell Sibhensana, Naibu Mkurugenzi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo,FAO kwenye ofisi ya Dharura na Ustahimilivu amesema “Katika maeneo ambayo mizozo ndio kichocheo kikuu cha uhaba wa chakula na hitaji la kibinadamu, FAO inataka ufikiaji usio na kikwazo kwa idadi ya watu ambao wameathirika na kwamba watoa huduma za kiutu wanaweza kuwezeshwa kuwafikia watu hawa haraka iwezekanavyo. Na pia ufadhili upatikane  ili kuweza kuwsaidia watu wenye uhitaji wa haraka na wale wenye mahitaji ya muda mrefu  Na katika hali hii, FAO imekuwa ikitilia mkazo kilimo cha dharura.

Juhudi za haraka zinahitajika

Ripoti hiyo inasema bila juhudi za haraka za kibinadamu kuchukuliwa na hatua za pamoja za kimataifa juu ya kushughulikia mizozo inayoedelea duniani kutakuwa na ongezeko kubwa la ukosefu wa chakula na idadi kubwa ya watu watapoteza maisha kwa njaa.

Mataifa mengine yaliyo kwenye orodha hiyo ni Nigeria, Chad, Yemen, Msumbiji, Myanmar, Syria na Lebanon. Katika nchi hizo zote, migogoro ilikuwa ni ama chanzo kikuu cha njaa, au mchangiaji mkuu wa njaa.

Haiti
Raia wa Haiti wapo katika wakati mgumu kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya magenge ya kihalifu yaliyopelekea mamia ya maelfu kuyakimbia makazi yaoPicha: Clarens Siffroy/AFP

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yameongeza kuwa hayajafanya uchunguzi huo katika mataifa yote ingawa yalilenga kuzitazama nchi ambazo kwa sasa tayari ziko katika hali mbaya zaidi.

Soma zaidi.Mataifa yaomba mkutano wa dharura kuangazia hali katika Ukanda wa Gaza 

Mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa pili mfululizo wa kupungua kwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu, ripoti hiyo imebainisha huku mataifa kama Ethiopia, Yemen, Syria na Myanmar ufadhili ukipungua kwa asilimia 75.

Njaa kali inatarajiwa huko Gaza, Sudan na Haiti

Huko Gaza, ripoti inasema kuna hali mbaya zaidi kwa sasa ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 41 ya watu sawa na kusema watu 876,000, watakabiliwa na njaa kuanzia Novemba hadi mwishoni wa Aprili mwakani.

Nchini Sudan, mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita watakabiliwa na njaa katika kambi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini, ilitabiri ripoti hiyo.

Sudan
Wananchi wa Sudan wakiwa kwenye foleni ya kuaptiwa msaada wa chakulaPicha: Mohamed Khidir/Xinhua/picture alliance

Idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa na vifo inakadiriwa kuongezeka karibu mara mbili katika kipindi cha miezi minne kati ya Aprili na Julai 2024 dhidi ya kipindi kama hicho mwaka jana nchini Sudan. Lakini idadi hiyo inatarajiwa kuwa mbaya zaidi kuuanzia mwezi na kuendelea.

Soma zaidi. Mataifa ya kusini mwa Afrika yakabiliwa na janga la njaa

Machafuko nchini Haiti, pamoja na mzozo wa kiuchumi na vimbunga  vya mara kwa mara vinamaanisha kuwa hali ya njaa pia inatarajiwa kuwa mbaya zaidi.

Mzozo huko nchini Mali, ambapo ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani uliondoka mwaka 2023, huenda hali ya njaa ikazidi kuwa mbaya zaidi wakati makundi yenye silaha yakiendelea kuweka vizuizi kwenye miji na barabara vinavyozuia misaada ya kibinadamu, mashirika hayo yalisema.

Ripoti hiyo imehitimisha kuwa migogoro inawalazimu watu kukimbia makazi yao, kuvuruga maisha na mapato yao na hivyo kupunguza upatikanaji wa soko na kuwadumbukiza watu katikaa baa la njaa.

Related Posts