Mataragio: Changamoto ya kujaza gesi iishe

Dar es Salaam. Huenda msongamano kwa ajili ya kujaza gesi kwenye magari ukafikia ukomo baada ya Serikali kuagiza kituo mama kilichopo eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kikamilike mwezi ujao.

Kukamilika kwa kituo hiki kutawezesha utendaji wa vituo vingine vidogo vinne vitakavyokuwa vikichukua gesi hapo kwa ajili ya kuhudumia magari katika maeneo watakayokuwa wanatoa huduma, ikiwemo Mikocheni eneo la Cocacola, Muhimbili na Kivukoni.

Maagizo haya yametolewa wakati ambao kituo kingine cha kujaza gesi kinachomilikiwa na kampuni ya mafuta ya Meru kimefunguliwa Oktoba 24, mwaka huu katika Barabara ya Mandela.

Kuzinduliwa kwake kumeifanya sasa Dar es Salaam kuwa na vituo vinne vya kujaza gesi baada ya vile vya awali vya Ubungo, Uwanja wa Ndege na Tazara.

Akitoa maagizo hayo leo Novemba mosi, 2024, Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio ameagiza ujenzi wa kituo hicho kufanyika usiku na mchana ili kuhakikisha kinakamilika Desemba mwaka huu kama ilivyopangwa.

“Tunahitaji itakapofika Desemba hiki kituo kiwe kimekamilika, kuna maendeleo makubwa sana tangu Julai hadi sasa, tunategemea watamaliza kabla ya mwisho wa mwezi huu na nimetoa maelekezo kazi hii ianze kufanyika usiku na mchana,” amesema.

Wakati ujenzi ukiwa katika hatua za mwisho kwa mujibu wa Dk Mataragio, vifaa viko kwenye meli na vitapokewa katikati ya Desemba ili kituo kiweze kukamilika na kuzinduliwa.

“Nia yetu kama wizara na TPDC (Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania) ni kuhakikisha tunazindua hiki kituo kabla mwaka huu haujaisha,” amesema.

Kuzinduliwa kwake kutasaidia kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katika vituo vinne vya sasa vinavyotoa huduma ya kujaza gesi.

 “Mtaona vituo vichache tulivyonavyo vina foleni ndefu sana, ujio wa kituo hiki utaondoa hiyo adha. Kwani kituo hiki kitakuwa na uwezo wa kushindilia gesi na kusafirishwa kwenda vituo vingine vinavyojengwa ndani na nje ya Dar es Salaam,” amesema Dk Mataragio.

Mbali na hilo, Dk Mataragio amesema ujenzi wa kituo hicho unaenda sambamba na ununuzi wa magari kwa ajili ya kuuza gesi mtaani (mobile stations) ambazo zitauza gesi katika maeneo ambayo hayana miundombinu ya kujaza gesi.

Kuhusu hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi wa TPDC, Emmanuel Gilbert amesema, “mpaka sasa majadiliano na wawekezaji sita yanaendelea kwa ajili ya kuchukua gesi katika kituo hiki (Chuo Kikuu) na kwenda katika maeneo yao kwa ajili ya kujaza gesi katika magari,” amesema.

Kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia magari manane kwa wakati mmoja na ikiwa kitaendeshwa kwa saa 18 kwa siku magari 1,500 huweza kuhudumiwa.

Gesi kwenye magari inaelezwa hupunguza gharama kwa zaidi ya asilimia 50 kwani inauzwa kwa Sh1,150 kwa kilo ikilinganishwa na petroli ambayo kwa lita moja huuzwa Sh3,011.

Unafuu huo ndio uliochochea ongezeko la watu 4,500 kuunganisha gesi kwenye vyombo vyao vya moto lakini changamoto wanayokabiliana nayo ni upungufu wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari.

Tanzania inakadiriwa kuwa na futi za ujazo za gesi asilia trilioni 230, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5 kulingana na taarifa za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi tayari imeanza kuchimba gesi katika visiwa vya Songosongo wilayani Kilwa, mkoani Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara.

Nishati hiyo pia hutumika kuzalisha umeme na kuendesha mitambo ya baadhi ya viwanda nchini, kutumia kama nishati majumbani pamoja na kwenye magari na kwa kiwango kikubwa inaelezwa itakuwa suluhu ya panda shuka ya mafuta kwa madereva.

Related Posts