MIAKA 63 YA UHURU : TANAPA YAWAHIMIZA WATANZANIA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania ( TANAPA) limeendelea kuwahimiza watanzania kushiriki katika Kupanda Mlima Kilimanjaro kwenye Kampeni ya TWENZETU KILELENI ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 1, 2024 Jijini Dar es Salaam, Afisa Uhifadhi Mkuu TANAPA, Mapinduzi Mdesa amesema upandaji wa Mlima utaanza Desemba 3, 4, na 5 ambapo Desemba 9 makundi yote ya upandaji yatakutana kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro ikiwa ni siku adhimu ya maadhimisho ya Uhuru.

“Utaratibu huu umekuwa ukifanyika, ambapo kila mwaka makundi ya maafisa wa jeshi la wananchi wamekuwa wakipanda na bendera ya Tanzania kwaajili ya maadhimisho hayo , kwahiyo kuanzia mwaka 2021 tukaanzisha kampeni ambayo imelenga kuhusisha watanzania wote kushiriki kupanda Mlima Kilimanjaro”. Amesema

Aidha amesema kuwa katika maadhimisho hayo, kutakuwa na njia tatu rasmi za kupanda mlima – Marangu, Machame, na Lemosho – ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Stawisha Uoto wa Asili Tanzania, Okoa Barafu ya Mlima Kilimanjaro.”

Nae Afisa Uhifadhi Daraja la I kitengo cha Utalii KINAPA, Vitus Mgaya amesema msimu wa tatu TANAPA iliweza kupanua wigo kwa kuongeza idadi ya njia kwani mara ya kwanza walikuwa wakitumia njia moja ambayo ni Marangu ambapo ni kampuni moja ilikuwa inahusika kuratibu shughuli za upandaji.

Amesema katika njia ya Marangu zitatumika siku sita kupanda mlima, njia ya Machame itatumia siku saba na njia ya Lemosho ni siku nane.

“Wapandaji ambao watatumia njia ya Marangu wataanza tarehe 5, watakaotumia njia ya Machame wataanza tarehe 4 na wale ambao watatumia njia ya Lemosho wataanza tarehe 3 lakini lengo ni wote kufika kileleni siku ya tarehe 9 Desemba”. Amesema

Kwa upande wa Makampuni ya waongoza watalii wamesema wapo tayari kutoa huduma nzuri kwa washiriki wote ambao watapanda milima kupitia njia zote ambazo watachagua washiriki kupanda.








Related Posts

en English sw Swahili