Mifumo minne ya Chama inayompa jeuri Gamondi

MOJAWAPO wa usajili uliogonga vichwa vya habari katika msimu huu ulikuwa ni wa aliyekuwa kiungo wa Simba, Clatous Chama kuihama timu hiyo aliyoichezea kwa misimu sita na kutua kwa wapinzani wao wakubwa na watani wa jadi, Yanga.

Chama aliyejiunga na Simba mara ya kwanza Julai 1, 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya kwao Zambia, amekuwa ni mmoja wa viungo bora nchini kwa muda mrefu na kitendo cha kujiunga na Yanga kimekuwa na manufaa makubwa kwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi.

Mwanaspoti linakuchambulia jinsi nyota huyo anavyompa jeuri Gamondi katika harakati za kuusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na mashindano mengine inayoshiriki timu hiyo ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho (FA).

Msimu uliopita Yanga ilipitia changamoto kubwa baada ya kuumia kwa kiungo Pacome Zouzoua, jambo lililosababisha pengo lake kuonekana katika baadhi ya michezo hasa ule wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Uwepo wa Chama, Stephane Aziz Ki, Pacome na Maxi  Nzengeli unampa wigo mpana Gamondi wa machaguo tofauti ambapo anaweza kutumia mfumo wa 4-3-3 ili kuendana na wachezaji hao na kutengeneza uwiano mzuri wa kushambulia na kuzuia.

Katika mfumo huo, Prince Dube ambaye hajaanza vizuri akiwa na kikosi hicho tangu asajiliwe msimu huu akitokea Azam FC, anaweza kusimama kama mshambuliaji wa kati akishirikiana na Pacome, Nzengeli au Clement Mzize ama Mudathir Yahya.

Gamondi anaweza kumtumia Mzize, Dube au Kennedy Musonda katika eneo la ushambuliaji, huku Khalid Aucho akisimama kiungo mwenye jukumu la kukaba wakati kushoto akicheza Chama na kulia Aziz KI kwa mfumo huo na kuleta matokeo chanya.

Nyota hao watakuwa huru kuchezesha timu, jambo litakaloifanya Yanga kutengeneza safu bora ya wachezeshaji kutokana na rekodi zao kwani wote wamekuwa wazuri katika kufunga na kutoa asisti kwa sababu ya ubora wao.

Mfumo mwingine ni wa 4-4-2 ambao una viungo wanne na ikiwa Gamondi atataka kuanza na wawili wenye uwezo wa kukaba, basi anaweza kuwatumia Aucho na Mudathir, huku Chama na Aziz Ki wakipeleka mashambulizi kwa wapinzao wao kupitia pembeni.

Ikiwa Gamondi atataka kuanza na kiungo mmoja  mwenye sifa nzuri za kuzuia zaidi, basi Aucho au Mudathir mmoja atasubiri benchi, hivyo kutoa nafasi kwa Pacome au Nzengeli kuungana na Chama na Aziz KI kwa ajili ya kunogesha katika eneo hilo.

Gamondi alitumia mfumo huu dhidi ya Mamelodi Sundowns katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kutumia washambuliaji wawili kiasili, ambapo Mzize na Joseph Guede walianza ingawa wote walikuwa na majukumu tofauti wakiwa uwanjani.

Jeuri nyingine ambayo Gamondi anaipata ni katika mfumo wa 4-2-3-1 ambao unatoa nafasi kwa mabeki wanne, viungo wawili wa ukabaji na watatu wanaoshambulia huku mshambuliaji wa kati akiwa mmoja ambaye anaweza kusimama Mzize, Musonda au Dube.

Katika safu ya viungo washambuliaji wanaweza kucheza Chama, Aziz KI na Pacome au Nzengeli, huku uwepo wa mshambuliaji wa kati ukimfanya Mudathir kushirikiana na Aucho ilhali Jonas Mkude na Salum Abubakar ‘Sureboy’ wakipambana kupenya.

Mfumo mwingine ambao Gamondi anaweza kuutumia ni wa 3-5-2 ambao unaweza kuwatumia mabeki watatu Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ pamoja na viungo watano ambao kazi yao kubwa itakuwa kusaidia pindi timu inaposhambuliwa.

Yanga inaweza kucheza hivyo ikimkosa beki wa kulia, Yao Kouassi huku ikitoa nafasi kwa Nzengeli kutokea  kulia kati ya viungo watano, mfumo ambao unaweza kumuona Chama, Aziz KI, Pacome Aucho na Mkongomani huyo wakicheza pamoja.

Katika mfumo huo pia wa 3-5-2, washambuliaji wanaoweza kusimama ni  Dube na Mzize, Musonda au Jean Baleke.

Yanga haijakosea kumsajili Chama kwani rekodi  zinambeba hata kabla ya kutua katika kikosi hicho cha Jangwani ambapo akiwa na Simba aliyoitumikia kwenye michezo 179 ya mashindano yote alifunga mabao 42 na kutoa asisti 60.

Rekodi tamu kwa nyota huyo ni za msimu wa 2022/2023 alipohusika katika mabao 18 akifunga manne na kuasisti 14 na ule wa 2020/2021 alipokuwa moto zaidi kufuatia kuhusika na mabao 23 akifunga manane na kuasisti 15.

Misimu ambayo namba za Chama katika Ligi Kuu Bara zilikuwa chini ni 2021/2022 aliporejea Simba akitokea RS Berkane ya Morocco ambapo alifunga mabao matatu huku 2019/2020 akifunga mabao mawili na kuchangia 10.

Katika msimu wake wa kwanza wa 2018/2019 akiwa na kikosi hicho cha Msimbazi alihusika katika mabao 16 ya ligi ambapo alifunga saba na kutoa asisti  tisa, huku akiipeleka timu hiyo robo fainali ya michuano ya klabu Afrika mara tano.

Michezo ya kimataifa imempa sifa na umaarufu mkubwa kutokana na kuibeba timu hiyo mabegani mwake hasa katika hali ambayo mashabiki walikuwa wamekata tamaa, huku akiwa amefunga mabao 15 na kuchangia sita kwenye mechi 44 za hatua ya makundi.

Ukiachana na rekodi hiyo akiwa na Simba hata alipojiunga na Yanga, ameendeleza moto uleule kwani katika mechi za awali za kufuzu hatua ya makundi nyota huyo alihusika na mabao manane kati ya 17 yaliyofungwa na kikosi hicho.

Yanga ilianzia hatua za awali kwenye michuano hiyo ikicheza mechi nne na kati ya hizo imefunga mabao 17 ikianza kuichapa Vital’O ya Burundi 4-0 ugenini, 6-0 nyumbani na pia ikiichapa CBE SA ya Ethiopia ugenini 1-0 ilhali nyumbani 6-0.

Katika mabao 17 Chama alifunga matatu na kutoa asisti tano, akikiwezesha kikosi hicho kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kuishia robo fainali.

Kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, nyota huyo amehusika na mabao mawili ya kikosi hicho akifunga moja na kutoa asisti moja.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alikaririwa akieleza kwamba, uwepo wa Chama umemuongezea balansi ya timu hiyo katika eneo la kiungo mshambuliaji, kwa sababu mbali na kusaidia tu kupeleka mashambulizi ila ana uwezo mkubwa pia wa kufunga.

“Mchezaji mzuri huwa anajieleza mwenyewe kutokana na kile alichokifanya au anachoendelea kukifanya, Chama ni mmoja wa wachezaji bora na kocha yoyote angetamani uwepo wake kwenye timu, ameongeza ubora wa kikosi chetu,” alikaririwa Gamondi.

Related Posts