Mo ambwaga Mkude kesi madai ya Sh1 bilioni

MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya madai ya fidia ya Sh1 bilioni iliyofunguliwa na kiungo wa Yanga, Jonas Mkude dhidi ya kampuni ya Mohamed Enterprises (Tanzania) Limited.

Hukumu ya kesi hiyo namba 192 ya mwaka 2023 ilitolewa Juzi, Jumatano, Oktoba 30, 2024 na Jaji Phillip Butamo aliyeisikiliza baada ya kuridhika kuwa mdai, Mkude, ambaye ni kiungo wa Yanga hakuweza kuthibitisha madai yake.

Katika kesi hiyo, Mkude alikuwa akiidai kampuni hiyo inayoongozwa na rais wa Heshima na mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji (Mo Dewji) fidia ya Sh1 bilioni kwa madai ya kutumia picha ya sura yake katika matangazo ya biashara zake bila ridhaa yake.

Katika hati yake ya madai pamoja na ushahidi wake, Mkude aliyewahi kutumikia Simba kabla ya kuhamia Yanga, alidai kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikitumia picha ya sura yake katika matangazo ya kibiashara ya huduma na bidhaa zake bila ridhaa yake.

Alidai kuwa kampuni ilikuwa ikitangaza matangazo hayo kupitia mitandao yake ya kijamii ya Instagram, Facebook na Twitter (sasa X) nchini na duniani kote.

Mkude alidai kuwa Julai 12, 2023, akiwa amejiunga na Yanga wakati akijiandaa na mechi ya soka iliyokuwa mbele yao alibaini kuwepo kwa matangazo ya kibiashara yenye picha ya sura yake katika mitandao hiyo ya kijamii ya kampuni hiyo.

Alidai kuwa aliyapiga picha na kuyahifadhi kisha baadaye aliyachapisha kwa uchunguzi zaidi na kwamba siku hiyohiyo alianza kupokea simu na ujumbe wa maneno kwa njia ya simu kutoka kwa watu mbalimbali wakipongeza kwa fursa hiyo.

Mkude alidai kuwa mkataba wake na Yanga ulikuwa unamzuia kujihusisha na taasisi au klabu nyingine yoyote bila kupata kwanza ridhaa ya Yanga na kwamba kama kuna timu ya soka ilitaka kufanya naye kazi ilipaswa kuilipa Yanga Dola 100,000 za Marekani.

Kutokana na hali hiyo alifungua kesi hiyo dhidi ya kampuni hiyo akidai kuwa kwa kitendo hicho ilikiuka haki zake mbalimbali ikiwemo haki ya faragha na kuingilia haki zake za kiuchumi isivyo halali na akaomba malipo ya fidia ya kiasi hicho pamoja na nafuu nyinginezo.

METL katika utetezi wake pamoja na mambo mengine ilidai kuwa ina haki ya kutumia picha ya sura yake Mkude akiwa amevaa jezi za Klabu ya Simba kutangaza bidhaa zake chini ya mkataba wa udhamini na masoko kati yake kampuni dada yaani A-One Product and Bottlers Limited na Simba.

Hivyo ilidai kuwa haiwajibiki kumlipa Mkude kiasi cha fidia alichokuwa anakidai wala mrabaha kama alivyodai kwenye hati ya madai na ikaomba kesi hiyo itupiliwe mbali.

Jaji Butamo baada ya kusikiliza pande zote katika hukumu yake hiyo amesema kuwa baada ya kuchanganua ushahidi wa pande zote amebaini kuwa picha za mdai, Mkude, kampuni hiyo ilizipata wakati akiwa mwajiriwa wa Klabu ya Simba kwa mkataba wa miaka miwili.

Baada ya kurejea mkataba wa ajira yake Mkude na Simba, Jaji Butamo amesema kuwa mmiliki halali wa picha za Mkude zilizotumika katika matangazo ya bidhaa za kampuni hiyo yaani Mo-Chungwa, Mo Xtra na Mo Tangawizi ni Simba.

Jaji Butamo amefafanua kuwa amefikia uamuzi huo kwa kuwa zilichukuliwa akiwa amevaa jezi za Simba wakati wa mkataba wa ajira yake na mwenyewe Mkude aliridhia picha hizo kutumiwa na Simba ambayo iliingia mkataba wa makubaliano ya kibiashara na kampuni dad ya mdaiwa (METL), yaani A-One Product and Bottlers.

Amesema kwa kuwa A-One iliingia mkataba wa makubaliano ya kibiashara na Simba, METL ilikuwa na haki ya kutumia picha hizo kibiashara na kuwa Mkunde mwenyewe aliridhia zitumike na Simba kibiashara na kwa hivyo hakuwezi kuwa na madai ya matumizi ya picha zake isivyo halali.

“Hivyo mdaiwa akiwa mdhamini wa Simba, akiwa na mamlaka ya kuchukua na kutumia picha za wachezaji wa Simba ni mmiliki halali wa sura/picha za mdai,” amesema Jaji Butamo.

Jaji Butamo amesema kuwa kwa kuwa Mkude aliridhia picha zake kutumia na mwajiri wake wa awali, Simba madai yake ya fidia Kwa matumizi ya picha hizo kibiashara hayana msingi.

“Ushahidi uliotolewa na wadaiwa (pande zote) kama ulivyofafanuliwa katika hukumu hii unaonyesha kuwa mdai ameshindwa kuthibitisha kesi yake kwa kiwango kinachotakiwa kisheria. Hatimaye kesi hii inafutiliwa mbali kwa gharama,” amehitimisha Jaji Butamo akimaanisha kuwa Mkude anatakiwa kuilipa METL gharama za kesi hiyo.

Related Posts