Mwelekeo bajeti 2025/26 ni Sh55.06 trilioni

Dodoma. Serikali inakadiria kukusanya na kutumia Sh55.06 trilioni kwa mwaka 2025/26, ikitaja maeneo sita ya kipaumbele ikiwamo kugharamia maandalizi ya uchaguzi mkuu mwakani.

Hayo yamesemwa leo Novemba Mosi, 2024 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipowasilisha bungeni mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26.

Amesema kati ya fedha hizo mapato ya ndani ni Sh38.9 trilioni kwa mwaka 2025/26 ikilinganishwa na maoteo ya Sh34.6 trilioni ya mwaka 2024/25.

Amesema kati ya fedha hizo Sh55.06 trilioni, matumizi ya kawaida ni Sh38.6 trilioni na ya maendeleo ni Sh16.4 trilioni.

Dk Mwigulu amesema misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo inakadiriwa kuwa Sh1.02 trilioni, mikopo nafuu Sh5.6 trilioni na mikopo ya kibiashara kutoka vyanzo vya ndani na nje Sh9.4 trilioni.

“Ongezeko hilo limezingatia misingi ya uchumi jumla, mikakati na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kuimarisha ukusanyaji wa mapato,” amesema.

Kuhusu maeneo ya kipaumbele, Dk Mwigulu amesema ni uendelezaji wa miundombinu, uimarishaji wa sekta za uzalishaji na huduma za jamii.

Mengine ni usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, kuboresha usimamizi na mifumo ya kitaasisi ili kuimarisha utawala bora na kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa makundi maalumu.

Kwa upande wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25, Dk Mwigulu amesema katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024/25, Serikali imekusanya Sh11.5 trilioni kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje na kati ya fedha hiyo Sh7.9 trilioni ni mapato ya ndani, sawa na asilimia 99.4 ya lengo la Sh7.9 trilioni.

Amesema misaada na mikopo nafuu ilifikia Sh1.37 trilioni, mikopo ya kibiashara kutoka masoko ya ndani ilifikia Sh1.6 trilioni na mikopo ya kibiashara kutoka nje ilifikia Sh593.65 bilioni.

“Katika utekelezaji wa kipindi hicho ilitolewa ridhaa ya Sh11.6 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Ridhaa ya matumizi ya Sh114.20 bilioni iligharamiwa kwa mkopo wa muda mfupi kutoka Benki Kuu ambayo yapo ndani ya kiwango kinachokubalika kisheria,” amesema.

DP World yamwaga mabilioni

Akiwasilisha bungeni mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2025/26, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ametaja mafanikio 10 yaliyopatikana tangu Kampuni ya DP World ianze kufanya kazi katika Bandari ya Dar es Salaam Aprili, 2024.

Amesema baadhi ya mafanikio ni kampuni hiyo kuwekeza Sh214.425 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya kisasa, ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na usanifu na usimikaji wa mfumo wa Tehama wa kisasa wa uendeshaji wa bandari.

Amesema kiasi hicho ni sawa na asilimia 31 ya Sh675 bilioni wanazotakiwa kuwekeza kwa kipindi cha miaka mitano.

Profesa Kitila amesema mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miezi mitano tangu kampuni hiyo ianze kuendesha gati 0-7 katika Bandari ya Dar es Salaam, Serikali imeshakusanya Sh325.3 bilioni.

“Mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP World, ikijumuisha tozo ya pango 6, tozo ya mrabaha, na warfage (ardhia),” amesema.

Amesema kutokana na kuongezeka kwa mapato na kupungua kwa gharama za uendeshaji kutokana na maboresho yaliyofanyika, Serikali kupitia TPA imeanza uwekezaji katika miradi yenye thamani ya Sh1.922 trilioni kwa kutumia makusanyo yanayopatikana.

SGR yazalisha ajira 180,176

Profesa Kitila amesema hadi kufikia Septemba 2024, reli ya kisasa ya SGR ilisafirisha abiria 645,421 na kuingiza mapato ya Sh15.695 bilioni.

Amesema hadi Septemba 2024 miradi 519 imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) katika ushoroba wa reli yenye kuvutia mtaji wa Dola za Marekani bilioni 4.59 ikitarajiwa kuzalisha ajira 115,566.

Miradi hiyo amesema ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, baadhi ikiwa imekamilika na kuanza uzalishaji.

Profesa Kitila amesema hadi sasa mradi umeshazalisha ajira zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 150,000 zisizo za moja kwa moja.

Amesema ajira hizo zimetengeneza pato la Sh358.74 bilioni.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Oran Njeza amesema katika uchambuzi wamebaini hadi Juni 2024, deni la Serikali lilikuwa Sh96.88 trilioni.

Amesema deni hilo ikilinganishwa na Sh81.98 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2023 ni sawa na ongezeko la asilimia 18.18 (Sh14.90 trilioni).

“Katika deni la sasa la Sh96.88 trilioni, deni la ndani lilikuwa Sh31.95 trilioni na deni la nje lilikuwa Sh64.93 trilioni. Uchambuzi wa kamati umebaini kwamba mpaka sasa deni la Serikali ni himilivu kwa kipindi kifupi, cha kati na kirefu,” amesema.

Amesema ongezeko la deni hilo limesababishwa na kushuka kwa thamani ya shilingi na kupokea mikopo mipya kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo.

Amesema licha ya deni la Serikali kuwa himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu, kamati inaishauri Serikali kufanya baadhi ya mambo ili kuhakikisha linaendelea kuwa himilivu.

Ametaja mambo hayo kuwa ni kuongeza wigo na ukusanyaji wa mapato ya ndani ili yawe na uwezo wa kugharimia deni.

Njeza ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Vijijini amesema mikopo yote inayopatikana ni vema Serikali ikaielekeza katika miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.

“Kutoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu na yenye masharti ya kati ili kupunguza mzigo wa riba pamoja na muda mfupi wa neema ambao unaambatana na mikopo ya kibiashara na kutafuta vyanzo vingine bunifu vya mapato kama vile hatifungani za kijani, miundombinu, na diaspora,” amesema.

Njeza amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watu ilikuwa milioni 61.7 na inakadiriwa kuwa, ifikapo mwaka 2035 idadi nchini itakuwa milioni 87.5 kutokana na ongezeko la watu la asilimia 3.2 kila mwaka.

“Ongezeko hili la idadi ya watu nchini haliendani na ukuaji wa uchumi. Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha kwamba ongezeko la watu linaendana na ukuaji wa uchumi kwa sababu hivi sasa kati ya watu 100 watu 87 ni tegemezi,” amesema.

Amesema kamati inaishauri Serikali kutenga bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kufanya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya ili kupata takwimu ya hali ya umasikini nchini kwa kuangalia viashiria vyote 17.

Njeza amesema taarifa iliyopo hivi sasa ya hali ya umasikini ni ya mwaka 2017/18, hivyo imepitwa na wakati.

Related Posts