Unazijua ndoa za sogea tuishi? Ndoa hizi ziko hivi, yeyote kati ya mwanamke au mwanamume anahamia kwa mwenzie na kuanza kuishi kinyumba bila kufuata taratibu za kisheria, kidini au hata za kimila.
Wapo wanaoishi hadi miaka 20, majirani zao wakijua ni mke na mume, wanazaa watoto na wengine kupata hadi wajukuu bila kufunga ndoa inayotambulika kisheria.
Baadhi yao safari huishia njiani kwa sababu mbalimbali, na hujikuta wameshindwana na kila mmoja kuamua kushika njia yake kwa amani.
Wapo wanaotenganishwa na kifo, mmoja anatangulia mbele ya haki, wakiwa wanaishi kama mke na mume.
Ndoa nyingi za ‘sogea tuishi’ zina visa na mikasa kama vilivyomsibu Naftari Joshua wa Magu mkoani Mwanza.
Joshua anakumbuka alivyolazimika kumlipia mahari mwanamke marehemu, ambaye enzi za uhai wake, aliishi naye kama mke na mume bila kufuata taratibu za kimila.
Akisimulia tukio hilo, anasema: “Mwanamke huyo alihama kwao na kuja kuishi wangu, niliona ni sawa tu kwa kuwa tulikuwa tunapendana, sikwenda kujitambulisha kwa wazazi wake, japo nilikuwa najulikana kwa baadhi ya ndugu zake kama mume wake.”
Anasema baada ya kuishi miaka mitatu kwenye ndoa ya ‘sogea tuishi’, mkewe akafariki kwa uzazi baada ya kupata kifafa cha mimba.
“Ilikuwa ni mtihani, alifia kwenye mikono yangu. Wazazi wake walinikana, walisema mtoto wao hajafa na hakuwa ameolewa, hivyo wanamtaka, kama sio wazee kukaa chini na kuelewana sijui ingekuwaje?
“Tulimlipia mahari marehemu, ndipo wazazi wake wakaridhia tuzike, tukio lile lilinipa funzo katika maisha.”
Mbali na kisa hicho, Jesca Naitoti yeye anaeleza namna alivyopotezewa muda na ndoa ya sogea tuishi na mwanamume aliyefikiri atakuja kuwa mumewe wa maisha.
“Nilichumbiwa na Agripa, sikuwa nikimpenda, moyo wangu ulikuwa ukimpenda mwanamume mwingine aliyeitwa Samwel,” anasema.
Anasema wazazi wake walimpenda zaidi Agripa, aliposhauriwa, aliamua kuondoka nyumbani kwao na kwenda kuishi na Samwel kinyumba bila kufuata taratibu.
“Tulikaa vizuri miezi miwili ya mwanzo, baadaye tukawa tunagombana, baada ya miezi mitano tulishindwana tukaachana, lakini tayari nilishapoteza nafasi kwa Agripa ambaye kipindi hicho naye alioa,” anasema Jesca kwa uchungu.
Hata hivyo, si kila mtu anakutana na visa na mikasa, mambo ni tofauti kwa familia ya Makene na mpenzi wake Anitha, ambao wana miaka 12 wakiishi pamoja kama mke na mume bila ndoa, wakiwa na watoto watatu.
Makene anasema mwanzo waliona ni sahihi, lakini kanisa lilikuwa likiwasisitiza umuhimu wa ndoa na Oktoba, mwaka huu watafunga ndoa yao na kutambulika rasmi kisheria na kidini kuwa mke na mume.
Tamu, chungu za sogea tuishi
Ofisa Usajili wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Joseph Mwakatobe anasema mnapokuwa hai na kuamua kutengana huwa haina tatizo kwenye maisha ya ‘sogea tuishi’.
Anasema mkiamua kupelekana mahakamani kila mmoja atapata sitahiki yake na maisha mengine yataendelea, hivyo dhana ya ndoa itatambulika hapo, kwamba mlikaa pamoja zaidi ya miaka miwili na mmeamua kuachana.
“Mmoja wenu anapofariki, dhana ya ndoa haipo tena kwa sababu huna cheti cha ndoa ambacho kinathibitisha mlikuwa mke na mume, lakini watoto watatambulika, aliyebaki hawezi kulalamika wakati anayemlalamikia hayupo duniani.
Mwakatobe anasema mazingira ya ndoa za sogea tuishi mara nyingi huleta shida pale mmoja anapofariki.
“Kuna watu wanaishi, majirani zao wanawaona wanaingia na kutoka, wakijua ni mke na mume na katika maisha ya kawaida, hakuna watu watawauliza kuhusu cheti cha ndoa, mtaishi tu, lakini ikitokea mmoja amefariki hapo ndipo kuna changamoto.
Anasema kwa mujibu wa sheria, yule mwenye nacho kilichoandikwa jina lake ndiye chake, aliyebaki hana chake hata kama mliishi miaka 30 mkachuma wote.
Mwakatobe anasema kisheria kinachokuthibitishia upo kwenye ndoa ni cheti, kama huna huwezi kuwa katika warithi, ikitokea huyo uliyeishi naye kama mkeo au mumeo amefariki, kama mna watoto hao ndio watarithi, lakini si huyo mwanamke au mwanaume aliyebaki, labda busara itumike tu.
“Huwa tunasisitiza watu wasiishi tu kama vile hakuna kifo, mmependana fungeni ndoa,” anasema akieleza kwamba kuna ndoa za dini au imani na za Serikali na zote lazima zifungishwe na mtu mwenye leseni ya kufungisha ndoa na zote zinapaswa kuwa na cheti cha ndoa.
Wakili kiongozi wa kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza, Alloyce Komba anasema staili ya sogea tuishi ndiyo ipo sana nyakati hizi.
“Watu wanaoana isivyo rasmi, kuna ndoa rasmi ambazo zipo kisheria na zile za mila, ikithibitika ndoa ya kimila ipo, kuna sheria inaelekeza iweje na ikitokea mkatengana kwa mfumo huo, haki ya kila mmoja itapatikana,” anasema Wakili Komba na kufafanua kwamba umiliki wa mali nao una vigezo vyake.
Anasema ikifikia kwenye mgawanyo, itaonyesha mali hiyo alichuma nani au ulimkuta mwenzako tayari ana mali zake na itaangaliwa mchango wako katika mali hizo.
Mwanasheria mwingine, Kamanda Fundikira anasema kama watu hao wamekuwa kwenye uhusiano, mmojawapo akamkuta mwingine na mali, hizo mali hazitamhusu mwingine.
“Kama walichuma pamoja wakiwa kwenye mahusiano, haijalishi walifunga ndoa au la, hizo mali ni za wote ili mradi tu waliishi pamoja.”
Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini anasema wenye ndoa za sogea tuishi wanaishi kinyume na maadili.
“Hawa wanazini, kiimani hawawezi kushiriki na sisi, huwa tunawaambia hamuwezi kukaa pamoja mkasema mnapendana kama hamjafunga ndoa.
“Unakuwa huna haki kwa mwenzako, ninachotaka kusema ni kwamba ndoa ni kitu muhimu, mkipendana basi itimizeni hiyo ahadi, sio mnaishi tu na kuzini,” anasema.
Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema wanaoishi kinyumba bila kuoana hawatambuliki na ni jambo ambalo halikubaliki.
“Katika Uislamu hatuna kitu kama hicho, hata ikitokea Muislamu mwenzetu akapitia changamoto hiyo, likatokea la kutokea huku kwetu halifiki kwa kuwa hatulitambui, labda waende kisheria.
“Huwezi kudai mirathi ya mke au mume ambaye hakukuoa, haijapata kutokea na kwenye imani yetu ya Kiislamu hiki kitu hakipo,” anasema Sheikh Kitogo.
Mchambuzi wa masuala ya uhusiano na malezi, Christian Bwaya anasema uhusiano ili udumu lazima pawepo kitu kama idhini ya jamii kuutambua na kuupa uhalali wa kisheria.
“Katika jamii yetu, huwezi kusema una uhusiano kama mnafanya siri na watu wenu wa karibu hawana habari. “Ndiyo maana tunafunga ndoa ambayo pia ina msingi wa kisheria.”
Anasema watu wanaoishi pamoja bila ndoa, ambayo ni ahadi ya kuwa pamoja inayotambulika na familia za pande zote, wanakuwa kwenye hatari ya kuwa na uhusiano unaokosa msingi wa kuwaweka pamoja.
Anasema wanapoamua kuwa na ndoa ya sogea tuishi wanasahau mvuto wa kimapenzi una msimu na kuna wakati utapotea.
“Urafiki nao unategemea mvuto huo, mkishakosha ahadi ya kuwa pamoja ni rahisi kuachana hisia zikipungua. Kwa hiyo hatari kubwa ya kuishi pamoja bila ahadi ya ndoa inayofahamika kisheria na jamii ni uwezekano wa kuachana pale mmoja wenu anapohisi hajisikii tena kuvutiwa na mwenzake.
Anasema, tafiti zinaonyesha kuwa wanaume ndio wanaoongoza kupungukiwa mvuto huo baada ya kuzoeana na mwanamke.
Katika mazingira haya, ni rahisi sana mwanamke kujikuta kwenye mazingira ya kuumizwa pale mwanamume anapoanza kujisikia hana tena mvuto kama ilivyokuwa awali.
Anasema uhusiano unapotiwa muhuri na ahadi ya kijamii na kisheria ya kuambatana, inakuwa rahisi wawili kushughulikia changamoto zao kila zinapojitokeza.
Akielezea tafiti za mahusiano, anasema upendo wa ndoa una pembe tatu, akimnukuu nguli wa tafiti za mahusiano ya kudumu ya kimapenzi, Profesa Robert J. Sternberg, aliyesema mapenzi yanayotegemewa kudumu yanahitaji pembe tatu ili yachanue na yasiishie njiani.
“Kwanza, ni ule mvuto wa kimapenzi unaowafanya wawili wautofautishe uhusiano wao na mahusiano mengine.” Kwa kawaida, mvuto wa kimapenzi hupotea na kurudi kutegemeana na mazingira mbalimbali na hivyo hauwezi kuwa msingi mkubwa wa kudumisha mahusiano.
“Pili, ni ule ukaribu unaowafanya wawili watake kufahamiana zaidi na kuimarisha urafiki. Tunafahamu bila urafiki watu wawili hawawezi kuotesha mizizi uhusiano wao. Mnapokosa urafiki mnakosa kufahamiana na hivyo hawawezi kuwa na vingi vinavyowaweka karibu.
Anasema la tatu na la muhimu ni ile ahadi ya kuambatana inayoweka mazingira ya watu wawili wanaopendana kuamua kutokuachana.
Akitoa ushauri kwa vijana wanaokutana na wapenzi wapya, anasema ni kujipa muda kidogo wa kuupitisha uhusiano wao kwenye pembetatu ya kufahamiana kwanza kabla ya kuupeleka uhusiano kwenye ngazi ya tatu ya ahadi ya kuambatana.
“Hili linaweza kufanyika bila kuishi pamoja na linaepusha maumivu pale mvuto wa kimapenzi unapozorota kama tulivyoeleza. Unapoishi na mtu bila ahadi ya kuambatana, maana yake unakuwa umevuka hatua muhimu ya mahusiano ya kudumu.”
Anasema ni busara kufahamiana na kuhusisha familia kwanza kabla ya kufanya maamuzi ya kuishi pamoja.
“Hasara nyingine ni mahusiano kuvunjika wakati watu tayari wana watoto na madhara yakawafikia na watoto pia.
“Hatusemi kwamba ndoa hazivunjiki, na kwamba mkianza na ndoa mahusiano hayatavunjika, lakini tunachokisema hapa ni kwamba unapokuwa kwenye mahusiano yaliyopitia hatua hizi tatu kwa maana ya mvuto, ukaribu na ahadi ya kuambatana, uwezekano wa kuumizana unakuwa mdogo zaidi ukilinganisha na uhusiano unaokosa kimoja wapo kati ya hivi vitatu.