Ruto amwapisha Profesa Kindiki kuwa Naibu Rais Kenya

Nairobi. Hatimaye Profesa Kithure Kindiki ameapishwa kuwa Naibu Rais mpya wa Kenya mbele Jaji Mkuu Martha Koome, akichukua nafasi ya Rigathi Gachagua, aliyeondolewa madarakani na Bunge.

Sherehe ya kuapishwa kwake imefanyika asubuhi ya leo Ijumaa Novemba mosi, 2024 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, ikishuhudiwa na Rais William Ruto, pamoja na wageni  wengine mashuhuri.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Mawaziri Hassan Joho, Davis Chirchir, Opiyo Wandayi, Julius Ogamba, Justin Muturi, na Aden Duale.

Wengine waliokuwepo ni Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki, Cecily Mbarire wa Embu, Paul Otuoma (Busia), Stephen Sang wa Nandi, na Abdi Guyo wa Isiolo.

Rais William Ruto amempongeza Profesa Kindiki baada ya kula kiapo cha ofisi hiyo.

Kuanzia saa 12:30 asubuhi, mamia ya Wakenya walifika KICC kushuhudia tukio hilo. Misururu mirefu ilionekana wakati wananchi wakijipanga kuingia eneo la KICC, huku kukiwa na ulinzi mkali.

Wakati wa hafla hiyo, wananchi walipiga picha za kumbukumbu wakijivunia tukio hilo la kihistoria. Wengine wamevaa rangi za bendera ya taifa na kupeperusha bendera za Kenya huku wakiwakaribisha viongozi mashuhuri waliofika eneo la tukio.

Hatua ya kumwapisha Kindiki imekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu kuondoa amri ya kusitisha kuapishwa kwake, iliyotokana na aliyekuwa Naibu Rais, Rigath Gachagua.

Baada ya Gachagua kuondolewa na Bunge la Kitaifa, Baraza la Seneti lilisikikiza shauri lake, kupiga kura na kufikia uamuzi wa kumwondoa kwenye wadhifa huo.

Related Posts