SERIKALI IMETEKELEZA MIRADI MINGI SEKTA YA AFYA-DKT. BITEKO

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza miradi mingi katika sekta ya afya inayolenga kuongeza ufanisi katika huduma za afya na kuboresha maisha ya Watanzania.

Sambamba na kulipongeza Kanisa Katoliki kwa juhudi zake za kutoa huduma za afya katika maeneo mbalimbali wakati ambao Serikali pia imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 1, 2024 Sengerema mkoani Geita wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa jengo la jipya la kisasa la upasuaji na mradi wa umeme wa jua katika hospitali ya Sengerema DDH iliyopo chini ya Kanisa Katoliki, Jimbo Katoliki la Geita.

Akitaja baadhi ya mafanikio ya Serikali katika sekta hiyo Dkt. Biteko amesema “ Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia imefanya kazi nyingi ikiwemo kujenga hospitali mpya 129, kukarabati hospitali kongwe 50, kujenga hospitali za wilaya 677 na zahanati 425. Nawaomba watu Sengerema na sisi wote kwa kujua wafadhili wametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hili na mradi wa umeme wa jua wamejinyima kwa ajili yetu hivyo tutunze miundombinu hii,”

Amesisitiza “Tutatibiwa sisi kutoka Kigoma na Kagera na wakati wa Covid 19 hapa palikuwa na msaada mkubwa haitakuwa sawa wakati mwingine wakija wakakuta tumepabadilisha na kuwa tofauti na lengo lao, tutunze vifaa hivi na majengo haya na tuwape moyo ili waweze kutusaidia katika maeneo mengine yenye uhitaji,”

Ameendelea kwa kuwashukuru wafadhili wa miradi hiyo na kuifanya hospitali hiyo kuwa bora na ya kisasa.“ Tunasheherekea mafanikio haya kwa sababu umisionari umelenga kuhudumia watu kiroho na kimwili, niwapongeze sana Kanisa Katoliki kwa kuunga mkono juhudi ambazo Serikali ingefanya, pamoja na kuhubiri watu kutenda mema na kuponya magonjwa yao na kuwaondoa kwenye umasikini hilo ni jambo muhimu,”

Aidha, Dkt. Biteko amebainisha kuwa Serikali inathamini mchango wa kanisa katika maendeleo ya watu.

Akizungumzia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, amesema inajengwa kwa msingi wa amani na usalama huku akiwaomba viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani na kuwaweka pamoja Watanzania ili waendelee kujenga nchi yao.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewaasa Watanzania kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na kufuata taratibu na sheria na kuwa uchaguzi huo usiwe sababu ya kuwagawa.

Naye, Mbunge wa Sengerema, Mhe. Hamis Mwagawa amemshukuru mtawa Dkt. Marie Jose na kumpongeza kwa kutoa huduma kwa wananchi na kusema kuwa hata wakati wa janga la Covid 19 pamoja na kuwashukuru wafadhili wote waliojitolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la upasuaji.

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Flavian Kassala amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza kutoka na ujio wa watawa sita na familia moja waliohitaji kujenga hospitali ambayo ingetoa huduma ya afya kwa wahitaji na baadaye hospitali hiyo ikawa teule hadi mwaka huu ambapo Serikali imejenga hospitali yake ya wilaya.

“ Tuna juhudi katika kuendesha huduma kwa gharama nafuu na tuna mfuko wa kusaidia wahitaji ambapo tunapata misaada kutoka Shirika la Marafiki wa Sengerema na Simba Health ambao walikuja na wazo la kuwa na chumba cha upasuaji chenye vifaa vya kisasa na sasa tumepata jengo hili ambalo litasaidia kutoa huduma za kisasa za upasuaji,” amesema Askofu Kassala.

Ameendelea kusema baada ya kuwa na jengo hilo lilikuja wazo kutoka Shirika la Marafiki wa Sengerema ambao ni madaktari wanafunzi kutoka Uholanzi la kupendekeza mradi wa umeme mkubwa wa jua ili pia usaidie kutumika katika mifumo ya CT scan na MRI.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Sengerema Sr. Dkt. Marie Jose amesema kuwa hospitali hiyo ina uwezo wa kulaza wagonjwa 22,000 na inatoa huduma za kibingwa kwa akina mama na watoto pamoja na kuwa sehemu ya kufanya mafunzo kwa vitendo kwa madaktari wanafunzi kutoka Hospitali ya Kanda ya Bugando.

“ Tumeanza kuboresha huduma zetu na idara ya mionzi ina mitambo mipya, tuna huduma ya watoto wanahohitaji huduma maalum na tuna umeme wa jua ambao ni wa uhakika. Leo ni siku ya furaha tuna jengo hili ambalo limegharimu shilingi bilioni 2.7 na mradi wa umeme wa jua umegharimu shilingi bilioni 1.7,” amesema Dkt. Jose.

Moja ya mfadhili wa jengo la upasuaji, Bibi. Doris Mars amesema kuwa walipopata wazo la ufadhili wa mradi huo yeye na familia yake waliamua kusaidia kwa kuwa mradi huo unalenga kuboresha maisha ya watu.

“ Mungu ametupa uwezo wa kusaidia wengine na Biblia Takatifu inatuambia kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wake hivyo tunaamini tutasaidia kuokoa maisha na kuwapa faraja watu wa Sengerema pia tunawashukuru wote walioto mchango wao katika miradi hii,” amesema Bibi. Mars.

Mwakilishi wa Sopowerful, Dkt. Koen Gelpke amesema kuwa uwepo wa jengo la kisasa ulihitaji pia umeme wa uhakikia ili kutoa huduma kwa wananchi na ndio sababu waliamua kujenga mradi wa umeme wa jua.

Awali Dkt. Biteko ameshiriki katika adhimisho la Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa jengo jipya la kisasa la upasuaji

Akihubiri katika misa hiyo , Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea, Damiani Denis Dalu amesema kuwa siku ya leo ni sikukuu ya watakatifu wote na ni sherehe kubwa katika liturijia na kuwa wanawakumbuka watakatifu wote.

Amefafanua kuwa watakatifu hao ndio waliofaulu na kuwekwa wafu ili kuwa kuelelezo cha watu wote kuwa maisha ya kumfuata yesu kristo yana tija mbinguni.

Askofu Dalu ameendelea kusema kuwa Kanisa Katoliki ni la kimisionari ambapo walitumwa mitume 12 dunia kote kwa ajili ya kuhubiri injili.

“ Wamisionari wa Afrika ndio waliohubiri injili eneo hili katika uinjilishaji wao walihakikisha kila wanapifika wanatoa huduma za afya, elimu na za kijamii kwa ujumla. Na hii ni Parokia ya Bikira Maria Afya ya Wagonjwa eneo hili wamisionari walifungua kituo cha wagonjwa na waliwajengea pia eneo kwa ajili ya kusali.” Amesema Askofu Dalu.

Amesisitiza “Tunamshukuru Mwasisi wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuenzi na kutambua huduma hizi kwa watu na Serikali kwa kuendeleza hili. Leo tunamshukuru Mungu na tuzidi kuombeana ili hiki tunachoenda nacho kikae sawa, tunashukuru kwa juhudi ambazo Serikali imezifanyq katika hospitali hii mwaka 2013 hadi 2015,”

Pia, Askofu Mkuu Dalu amewashukuru wafadhili kutoka nchini uholanzi kwa mchango wao katika hospitali ya Sengerema DDH “ Tunakoeleka ni kuzuri na tunawashukuru sana wafadhili wetu kwa uinjilishaji huu, tunamshukuru pia Askofu kwa urafiki kati ya dayosisi hizi na kutusaidia katika Sengerema Hospitali na kituo cha mafunzo.”

Related Posts