Sh21 bilioni kumaliza kero ya maji Buchosa

Sengerema. Huenda adha ya uhaba wa maji kwa wakazi wa Buchosa wilayani Sengerema ikamalizika baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh21 bilioni.

Miradi hiyo inahusisha uchimbaji wa visima na ujenzi wa miradi ya maji ya bomba ya Bugoro, Bupandwa, Kafunzo, Kazunzu na Bulyaheke.

Matumaini hayo yametolewa na Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo kuwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imeanza kuchimba visima na utekelezaji wa miradi ya maji ya bomba.

Shigongo amesema hivi karibuni kuwa katika utekelezaji wa ilani ya CCM kwa wananchi, atahakikisha Buchosa inaondokana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Halmashauri ya Buchosa yenye kata 21, vijiji 82 na vitongoji 411 ina wakazi 413,110.

Mkazi wa Kijiji cha Busweru, Kata ya Nyanzenda, Maria Juma ameieleza Mwananchi kuwa uchimbaji wa visima hivyo si tu utapunguza muda wa kusaka maji kwa wananchi wanaoishi kuzunguka visima hivyo, pia utaleta ahueni katika gharama za kununua maji na gharama za kujitibu kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

Maria amesema pia itasaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa yanayosambaa kutokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama hususani kichocho na homa ya matumbo.

“Visima ambavyo vimeshaanza kutoa huduma ni Kasisa, Mizuro na Bupandwa,” amesema.

Mkazi wa Kijiji cha Bugoro wilayani humo, Jonathan Athanas amesema licha ya kijiji hicho kupakana na Ziwa Victoria, bado maji ni ya shida na baadhi ya wananchi wamekuwa ama wakiuawa au kujeruhiwa na mamba na viboko wanapokwenda kuchota maji ziwani.

Amesema utekelezaji wa mradi wa maji ya bomba wa Bugoro utasadia kuondoa adha inayowakabili.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa, Idama Kibanzi alisema changamoto ya ukosefu wa majisafi imepata suluhisho kupitia uchimbaji wa visima na miradi ya maji ya bomba inayotekelezwa.

“Wakazi wa Buchosa walikuwa wanatumia maji ya Ziwa Victoria, visima vya asili na ya madimbwi ambayo yalikuwa yakihatarisha maisha yao na wengine kupoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba,” alisema.

Diwa wa Kata ya Lugata, Nduhelechi Mwebesa amesema utekelezaji wa miradi ya maji utapunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi.

Diwani wa Buhama, Peter Mbundu amesema miradi inatakiwa ielekezwe kwenye vijiji vinavyopakana na Ziwa Victoria ili kuwasaidia wananchi wasishambuliwe na mamba wanapokwenda kuteka maji ziwani.

Kupitia mpango huo, Serikali inatekeleza miradi saba ya mabomba ya maji na visima 22 kwa gharama ya zaidi ya Sh21 bilioni.

Kaimu Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Sengerema, Elisha Sembo amesema visima tisa kati ya 22 vimekamilika na kuanza kutoa huduma ya maji, huku vilivyobaki vikitarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba 2024 sambamba na miradi ya maji ya Bugoro, Kazunzu na Bulyaheke.

Amesema mradi wa Bupandwa utahudumia kata za Bupandwa, Katwe na Bangwe, huku mradi wa Lumeya utahudumu kata za Kalebezo na Nyehunge na imeanza kutoa huduma kwa wananchi.

“Tumetangaza zabuni ya miradi ya maji ya Maisome, Katoma, Ilenza na Iligamba, baada ya mkandarasi kupatikana utekelezaji utaanza mara moja ili kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi,” amesema.

Related Posts