Dar es Salaam. Boniface Jacob, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, ameelezea safari yake ya kipekee kuelekea ushindi wa nafasi hiyo huku akiwa gerezani, baada ya kukamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya mtandaoni.
Kupitia mahojiano maalumu na Mwananchi, Jacob, maarufu kama Boni Yai, amesimulia changamoto na maamuzi magumu aliyofanya ili kuiruhusu Chadema Kanda ya Pwani kuendelea na uchaguzi, ambao awali alitaka uahirishwe hadi hatima ya dhamana yake ipatikane.
Hatimaye, akiwa gerezani Segerea, alifahamishwa na mahabusu wenzake kuhusu ushindi wake, alioshinda kwa asilimia 77.
Boni Yai pia ameweka wazi mikakati yake ya kuimarisha Chadema, hasa katika maeneo yenye changamoto za kiusalama na mwamko mdogo wa kisiasa ndani ya Kanda ya Pwani unayohusisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Boni Yai alikamatwa Septemba 18, mwaka huu katika mgahawa wa Golden Folk uliopo Sinza Makaburini, jijini Dar es Salaam.
Amesema ukamataji wake ulikuwa na purukushani za hapa na pale kati yake na polisi, na ulizua tafrani kwa wapita njia na wateja waliokuwa wakipata huduma katika mgahawa huo.
Jioni ya Septemba 19, alipandishwa kizimbani katika Mahakama Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka mawili ambayo aliyakana na kupelekwa mahabusi Gereza Segerea kutokana na dhamana yake kuwekewa pingamizi na polisi kwa kilichoitwa usalama wake.
Gerezani huko aliingia akiwa mwananchama wa kawaida wa Chadema na alipoachiwa Oktoba 7, 2024 tayari alikuwa na kofia ya mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ambayo pia inampa ujumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Ataka uchaguzi uahirishwe
Kwenye mahojiano aliyofanya na wahariri waandishi wa Mwananchi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Boni Yai anasema kutokana na mwenendo wa kesi yake kutoeleweka, awali aliwatuma mawakili wake wakiombe chama hicho kiahirishe uchaguzi ambao awali ulikuwa umepangwa kufanyika Septemba 28, ili kusubiri hatima ya adhama yake.
Anasema chama kilikubaliana naye na kuuahirisha, lakini baada ya kuona dhamana yake inachelewa kupatikana na ushauri alioupata mahabusu aliamua vinginevyo.
“Na kule gerezani wafungwa na mahabusu wakanishauri nikiombe chama kiendelee na mchakato wa uchaguzi lasivyo nisingetoka.
“Akili za watu wa jela, waliniambia nikisema niendelee na msimamo wa uchaguzi kutofanyika, nitakaa kwa muda mrefu gerezani, badala yake walinishauri niache mchakato uendelee, bila kujali kama nitashinda au la,” anasema Boni Yai.
Baada ya hatua hiyo, anasema walipokwenda mahakamani na dhamana yake ikagonga mwamba, palepale aliwaeleza mawakili wake wawasiliana na chama tena ili kuruhusu uchaguzi kufanyika, ukafanyika naye akaibuka kidedea.
Kwenye uchaguzi huo, Boni Yai aliwateua Herny Kileo (mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kinondoni) na Ernest Mgawe (mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kibamba) kusimamia shughuli zake za kampeni.
Boni Yai anasema licha ya kuwa na matumaini ya kuibuka kidedea kutokana na maandalizi aliyoyofanya, siku ya uchaguzi Jumamosi Oktoba 5, alikuwa na wasiwasi kwa sababu alikuwa gerezani.
“Wakati uchaguzi unafanyika sikupata matokeo kwa wakati, nilitarajia mchana ningejua, lakini nilipata wasiwasi kwa sababu taratibu za gereza kuanzia saa tisa alasiri tunatakiwa kulala.
“Hadi muda huo naingia sehemu ya kulala hakuna habari yoyote niliyokuwa nimeipata kuhusu matokeo, na hadi saa 3 usiku nilipolala sikuelewa chochote,” anaendelea kusimulia.
Siku iliyofuata (Jumapili), asubuhi, Boni Yai anasema alikwenda kuangalia runinga, lakini hakufanikiwa kuona vichwa vya habari vya magazeti ili kujua kama ameshinda katika uchaguzi huo kwa kuwa muda kupitia magazeti ulikuwa umekwisha.
Hata hivyo, anasema kuna watu (mahabusu na wafungwa) walimfuata alipokuwa wakishangilia na kumwita “mwenyekiti, mwenyekiti”, akajiuliza, ‘hawa wamepata wapi taarifa au wamejuaje?’
“Walininyanyua juu juu, nawauliza nimeshinda kwa kura ngapi? Hawakujua zaidi ya kusema nimeshinda kwa asilimia 77. Waliniambia mimi na timu yangu yote tumeshinda, walinipongeza sana,” anasema Boni Yai.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 5, Boni Yai alipata kura 60, sawa na asilimia 77, dhidi ya Gervas Lyenda aliyepata kura 17, sawa asiliamia 23.
Alivyopenya kwenye uchaguzi
Katika maelezo yake, Boni Yai, anasema hakuwa na wasiwasi wa kushinda kutokana na maandalizi yake kuanzia katika mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu.
“Namba zangu (wapigakura) zilikuwa vizuri tangu narudisha fomu, waliniunga mkono kwa asilimia kubwa, kingine Pwani kwa muda mrefu walikosa mtu wa amshaamsha ambaye akisimama kweli unasema Chadema imesimama.
“Lakini kingine, nilikuwa najua shida ya Wanapwani kwamba walitaka uongozi uliochangamka, sio uliopooza,” alisema Boni Yai.
Kwa miaka minne, Kanda ya Pwani imekuwa chini ya Baraka Mwago kama kaimu mwenyekiti tangu Novemba 19, 2019 aliposhindwa uchaguzi Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, aliyekuwa mwenyekiti wa kanda hiyo kabla ya kurejea CCM.
Boni Yai anasema jambo jingine lililombeba na kuibuka kidedea katika mchakato huo, ni historia yake ya mapambano yaliyofanikiwa.
“Mgombea alikuwa ndani (mahabusu) lakini sifa zake zilikuwa nje. Uzuri historia yangu ilinibeba, Boniface ni mpiganaji, kiongozi, nimekuwa kamati kuu kwa nyakati tofauti. Siku ya kurudisha fomu niliwaambia nataka Kanda ya Pwani iweje, hivyo sikushangaa kuambiwa nimeshinda, ingawa nilipokea matokea nikiwa benchi gerezani,” alisema huku akipongeza maboresho makubwa yaliyofanyika ikiwemo suala la usafi na uwepo wa televisheni inayowawezesha kufuatilia matukio mbalimbali asubuhi.
Akijibu swali aliloulizwa, harakati zake mitandaoni zimewezaje kuathiri mienendo yake ya kimaisha, meya huyo wa zamani wa Ubungo, alisema harakati za kutetea haki za binadamu kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii, si jambo jepesi kwa kuwa anashughulika na watu moja kwa moja, hivyo mtindo wa maisha lazima ubadilike.
“Hakuna jambo lolote lisilokuwa na athari, kwanza mfumo wangu wa maisha umebadilika kutokana na hizi harakati za kuwa mstari wa mbele kupigania haki za binadamu. Mfumo wangu wa ulinzi umebadilika, hivi sasa kuna baadhi ya maeneo siwezi kuyatembelea.
“Pia, siwezi kukaa baa au sehemu za starehe hadi alfajiri kama ilivyokuwa zamani, kabla matukio ya watu kupotea na kutekwa hayajarejea. Zamani nilikuwa naweza kukesha hadi asubuhi, lakini sasa siwezi, sio salama kwangu,” anasema.
Jambo jingine, Boni Yai alisema kuna watu wenye nia njema, wanaume na wanawake, wanaweza kumtafuta kutaka msaada, lakini katika maisha ya uanaharakati, si rahisi kwake kuonana na kila mtu.
“Nimebadilisha mfumo wangu wa kula, siwezi kula kila sehemu au kutembea kila eneo, hata iwe mchana, kwa sababu naonekana kuwa tishio kwa watu wanaofanya vitendo visivyofaa katika jamii,” anasema.
Mbali na hilo, anasema mazingira ya biashara zakenayo yamebadilika, hivi sasa amewaachia watu jukumu la kusimamia shughuli hizo kutokana na yeye kukumbwa na misukosuko ya hapa na pale kutokana na harakati hizo.
“Nimepata hasara pia, kila baada ya miezi mitatu lazima ninunue simu mpya kwa sababu nikikamatwa naziacha polisi. Hivi sasa nina simu nne zinashikiliwa na Jeshi la Polisi. Pia, mawakili wanaosimamia kesi zangu nawalipa, siyo bure, hii ni hasara pia,” anasema.
Alipoulizwa mikakati yake kwenye wadhifa huo mpya, hususan katika Wilaya za Mkurunga, Rufiji, Bagamoyo na Kibiti ambako Chadema inaonekana dhaifu, licha ya kukiri suala hilo kwa ujumla, alisema maeneo ya Bagamoyo, Chalinze, Mafia, Kibaha Mjini na Vijijini kuna mwamko mkubwa kama ulivyo kwenye majimbo ya Dar es Salaam.
Alisema shida kubwa ya Mkoa wa Pwani ni hali duni ya kiuchumi na kukosekana kwa elimu ya uraia itakayowafanya wananchi kuamini kuna vyama mbadala vitakavyosemea changamoto zinazowakabili.
“Operesheni zilizojitokeza huko za Kibiti, Rufiji na Mkuranga zimewatia hofu watu kufanya shughuli za kisiasa, jambo lililowatia hofu wananchi wa maeneo hayo,” alisema.
Boni Yai alisema ili kuimarisha chama hicho, katika maeneo hayo atahakikisha anatoa elimu ya uraia kwa wananchi wa Kibiti, Mkuranga na Rufiji ili waweze kujiamini na kuwaongezea ujasiri wa kushiriki shughuli za kisiasa kwa sababu sheria inaruhusu.
“Katika uongozi wangu nitahakikisha wananchi wanarudi katika hali ya maisha ya kawaida, nitafanya mikutano na vikao vingi ili kuwapa ujasiri na morali.
“Kuna watu wana uwezo wa kugombea uongozi katika maeneo yale, lakini wanahofia usalama wao, kwamba wakionekana wanaipinga CCM, watakuwa katika mazingira magumu,” anasema Boni Yai.
Mbali na hilo, atahakikisha viongozi wakubwa wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu na wajumbe wa kamati kuu wanakwenda katika maeneo hayo kufanya mikutano ya hadhara mara kwa mara badala kuishia Mkoa wa Dar es Salaam.
Usikose sehemu ya pili ya mahojiano haya kesho akielezea ‘surprise’ ya Chadema mwaka 2025 kuhusu mgombea urais.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.