Singida BS, Yanga ilibeba hadhi ya mechi ya ubingwa

WATETEZI wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamerejea kileleni mwa msimamo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya  Singida Black Stars, ila moja ya jambo la kufurahisha ni jinsi wachezaji wote walivyojitoa kuzipigania pointi tatu.

Bao la kiungo mshambuliaji, Pacome Zouzoua dakika ya 67 lilitosha kuifanya kukaa kileleni na pointi 24 baada ya michezo minane na kuishusha Singida iliyokuwa inaongoza kwa muda mrefu hadi nafasi ya pili na pointi 22 kufuatia kucheza mechi tisa.

Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa kina wa mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.

Ushindani wa mchezo huo ulianza mapema tu kutokana na nafasi za timu zote mbili ambapo Singida ilikuwa kileleni huku kwa upande wa Yanga ikiwa nafasi ya pili jambo lililoongeza msisimko, kwani zilikuwa hazijapoteza mechi yoyote msimu huu.

Kitendo cha timu hizo kushika nafasi ya kwanza na ya pili kiliufanya mchezo huo kuvuta hisia za mashabiki wengi kusubiri kuona ni nani atakayeibuka mshindi, huku Yanga ikitazamiwa kama itaendeleza rekodi bora jambo ambalo ililifanya tena.

Presha ya mchezo huo ilianza mapema tu kwani ndani ya dakika 30 za kipindi cha kwanza zilishuhudiwa kadi za njano saba zikitolewa na mwamuzi, Ally Mnyupe kutoka Morogoro, jambo lililoashirikia mechi hiyo ilikuwa na uhitaji kwa kila timu.

Ubora wa viungo wa Singida wakiongozwa na Josaphat Arthur Bada, Mohamed Damaro na Emmanuel Keyekeh aliyeingia kipindi cha pili, ilionyesha wazi ugumu wa mchezo huo kutokana na viwango vyao hadi sasa na kuweza kukabiliana na wale wa Yanga.

Nyota hao walikuwa mwiba mkali kwa viungo wa Yanga waliokuwa wanaongozwa na Khalid Aucho na Duke Abuya ambao mara nyingi walionekana kutumia nguvu kubwa kukabiliana nao, hali iliyoonyesha wazi ulikuwa ni zaidi ya mchezo wa fainali baina yao.

Ushindi huo kwa Yanga sio kwamba tu umeifanya timu hiyo kuongoza Ligi Kuu Bara msimu huu ila imeendeleza rekodi bora ya kutopoteza hadi sasa tangu mara ya mwisho kikosi hicho cha Kocha, Miguel Gamondi kilipofungwa mabao 2-1 na Azam FC Machi 17, mwaka huu.

Tangu Machi 17, Yanga imecheza jumla ya michezo 18 ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo imeshinda 17 na kutoka sare mmoja tu wa (0-0) dhidi ya JKT Tanzania, mechi iliyopigwa Aprili 24, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni.

Katika michezo hiyo 18 iliyocheza Yanga kwa kipindi hicho chote, safu ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 35, ikiwa na wastani mzuri wa kufunga mawili kwa kila mchezo, huku eneo la kujilinda likiwa limeruhusu nyavu zake kutikiswa matatu tu.

Mbali na hilo ila Yanga ndio timu pekee hadi sasa kati ya 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ambazo hazijaruhusu bao lolote, huku Simba na Azam FC zikifuatia kwa kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu, wakati Singida imeruhusu mabao manne.

Mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube ameendeleza ukame wa kutocheka na nyavu katika Ligi Kuu Bara na timu hiyo kwani licha ya juzi kuanza kikosi cha kwanza, ila nyota huyo alionekana kupitia wakati mgumu unaowafanya mashabiki kumtilia mashaka.

Dube aliyemaliza na mabao saba ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita wakati akiichezea matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, bado amekuwa katika kiwango kisichoridhisha ingawa ni jambo la kawaida kwa mshambuliaji yoyote kupitia changamoto.

Nyota huyo aliyejiunga na Yanga msimu huu, mara ya mwisho kufunga bao la Ligi Kuu Bara ilikuwa ni sare ya 1-1, dhidi ya Simba Februari 9, wakati huo akiichezea Azam FC ambapo hadi leo hajafunga tena na kuibua mijadala kuhusu kiwango chake.

AUSSEMS ABADILI GIA ANGANI

Wakati, Patrick Aussems anateuliwa kikiongoza kikosi hicho msimu huu, alianza vibaya na timu hiyo hasa katika michezo ya kujiandaa na msimu ‘Pre Season’, hali iliyosababisha wadau wa soka nchini kuanza kuingiwa na mashaka juu ya uwezo wake.

Aussems aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali ikiwemo Simba, alianza vibaya hali iliyotia mashaka kama kweli ataweza kukiongoza kikosi hicho katika michezo ya Ligi Kuu Bara, ingawa kwa sasa kila mtu kwa sasa anaheshimu kazi anayoifanya.

Sababu kubwa ya wadau wengi kutokuwa na imani na Aussems ni kutokana na ubora wa wachezaji wanaoichezea timu hiyo jambo lililowafanya kuamiani huenda asingeweza kuwaweka sehemu moja na kutengeneza kikosi cha ushindani kinachoonekana sasa.

Mbali na kutengeneza timu ya ushindani ila Aussems pia amefanya mabadiliko ya kiuchezaji ambayo yamewafanya baadhi ya wachezaji kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza, licha ya ubora na umaarufu waliokuwa nao.

Miongoni mwao ni mshambuliaji, Joseph Guede aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Yanga ambapo licha ya kucheza na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara ila ameshindwa kuingia moja kwa moja kushindania namba na Mkenya, Elvis Rupia.

Eneo jingine ambalo Aussems ameendelea kuliamini ni eneo la golikipa ambapo licha ya ubora na umahiri wa kipa, Mohamed Kamara aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Horoya ya Guinea ila ameshindwa kupenya kwa mzawa, Metacha Mnata.

Kocha Mkuu wa Singida, Patrick Aussems amesema licha ya kupoteza mchezo huo ila amefurahishwa na jinsi wachezaji wa timu hiyo walivyopambana, huku akiweka wazi bado wanaendelea kuishi katika malengo yao waliyoweka ya kuchukua ubingwa msimu huu.

Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema watu wanapaswa kuiheshimu timu hiyo kutokana na ubora inaoendelea kuuonyesha na sio kuongea kama wanavyofanya, huku akieleza ushindi huo ni muhimu na umewajengea hali ya kujiamini zaidi.

Related Posts